Endelezeni ari na moyo wa huruma na mapendo kama Wasamaria wema
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa
Jubilei ya huruma ya Mungu yanafungwa rasmi kwa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme
wa Ulimwengu: hapo tarehe 20 Novemba 2016. Hii itakuwa ni siku ya furaha na
shukrani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kulijalia Kanisa kipindi cha neema
na baraka. Ni siku ya kumkabidhi Kristo Yesu, maisha na utume wa Kanisa na
ulimwengu mzima, ili kila mtu ajitahidi kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu
hapa duniani.
Jumapili tarehe 13 Novemba 2016,
Malango ya huruma ya Mungu kwenye Makanisa makuu na Madhabahu yamefungwa rasmi.
Kardinali Agostino Vallin, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, kwa niaba ya Baba
Mtakatifu Francisko amefunga lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Yohane wa Laterano. Katika mahubiri yake, amewataka waamini kutafakari
mambo ya nyakati kwa kuwa macho dhidi ya manabii wa uwongo; majanga asilia,
vita na kinzani; dhuluma na mauaji; matunda ya dhambi za wanadamu.
Katika mazingira katika haya,
waamini wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu,
tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hatima na
mustakabali wa maisha ya mwanadamu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyejifunua
kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma wa Baba, mwaliko kwa kujiaminisha kwake
ili kuchota mwanga, utulivu na amani, ili kukutana na Baba mwenye huruma katika
maisha. Jubilei ya huruma ya Mungu umekuwa ni muda uliokubalika kwa waamini
kushuhudia imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na
kimwili, mwaliko wa kuendelea kumwilisha huruma hii katika uhalisia wa maisha
ya watu.
Huruma ya Mungu ni mahali ambapo
waamini wanakimbilia kuonja upendo wa Baba wa milele anayeganga na kuponya
madonda ya udhaifu wa binadamu; anawasimamisha wale walioteleza na kuanguka,
ili kuwategemeza katika kutenda mema. Huruma ya Mungu ni kiini cha maisha na
utume wa Kanisa kwani inafumbata; upendo, huruma, rehema na msamaha. Ikiwa kama
waamini wanatembea katika jicho la huruma ya Mungu, wataweza kuwa ni chemchemi
ya furaha kwani historia nzima ya wokovu inafumbatwa katika huruma ya Mungu.
Yesu mwenyewe aliifunua huruma hii
kwa wagonjwa, maskini, wadhambi na wale wote waliokuwa wanatengwa na
kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Fumbo la Pasaka ni kielelezo cha hali ya juu
kabisa cha huruma ya Mungu kwa mwanadamu! Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu
umekuwa ni muda muafaka wa kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na
kimwili, ili kuwaonjesha wengine furaha, faraja, huruma ili hatimaye, kuweza
kujichotea msamaha unaobubujika kutoka kwa Mungu.
Kardinali Vallin anawataka waamini
kujenga na kuimarisha ndani mwao subira, huruma, upendo na msamaha kama
ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma. Waamini wanapopokea huruma ya Mungu, wawe na
ujasiri pia wa kuwaonjesha jirani zao upendo na huruma ya Mungu, kwa kuwarejeshea
tena utu wao uliochakaa kutokana na dhambi kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu
anayesimuliwa kwenye Injili. Huruma ni fadhila ambayo imewekwa mikononi mwa
Wakristo, licha ya udhaifu wao wa kibinadamu, ili kuwakirimia amani na
utulivu wa moyo. Huruma inakuwa ni dira na mwelekeo wa maisha ya waamini kama
ushuhuda wa imani tendaji!
Kama hazina ya maadhimisho ya Mwaka
Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanahamaishwa na Mama Kanisa
kuhakikisha kwamba wanaonesha upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama alivyofanya Msamaria mwema.
Waamini washirikiane na Mashirika
ya Misaada ya Kanisa katika kuganga na kuponya majeraha ya binadamu kwa mafuta
ya faraja na mshikamano kadiri ya uwezo na nafasi ya kila mwamini, bila
kuwageuzia maskini na wale wanaoteseka kisogo.
Kardinali Agostino Vallin, mwishoni
anawataka waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa urafiki na udugu ili
kuvunjilia mbali kuta za ubaguzi na utengano; mambo amabayo kimsingi ni kichaka
cha unafiki kinachoficha ubinafsi.
Watu wajenge utamaduni wa upendo na
kuishi katika misingi ya haki katika mahusiano ya kijamii, ili kujenga na
kudumisha mafungamano kati ya watu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.
Hakuna maoni:
ReplyDelete