SIKU YA HAKI YA MTOTO DUNIANI
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni wakati wa Katekesi yake aliwataka wadau mbali mbali katika Jumuiya ya Kimataifa yaani familia na taasisi mbali mbali kuhakikisha kwamba watoto wanalindwa na kuendelezwa ili kamwe wasitumbukie wala kutumbukizwa katika nyanyaso na utumwa mamboleo. Ni matumaini yake kwamba, Jumuiya ya Kimataifa italinda haki msingi za watoto ikiwa ni pamoja na uhai wao, elimu, afya na malezi bora, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.
Jumapili tarehe 20 Novemba 2016 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Haki ya Mtoto Duniani na Jijini Roma, kunaadhimishwa siku hiyo, ikiwa ni kumbukumbu ya Mkutano mkuu wa mwaka 1989 wa Umoja wa Mataifa kupitisha makubaliano ya haki msingi za watoto. Haki hizo ni pamoja na kutobaguliwa, haki ya kuzaliwa na kuishi, haki ya kukua, na haki ya kusikilizwa.
Tangu mwaka 1988 Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Italia, Caritas Roma imekuwa na harakati za kusaidia watoto walio katika hali ngumu za maisha. Kwa miaka hii, kiasi cha watoto 7,850 wamepata huduma katika nyumba za kuhudumia wahitaji na katika familia. Kwa sasa Caritas Roma ina Nyumba 3 kwa ajili ya watoto wadogo kabisa na Nyumba 2 kwa ajii ya vijana wadogo. Pamoja na watoto wa asili ya Italia kuhudumiwa katika makazi hayo, kuna wengi wanaohudumiwa ambao ni watoto wahamiaji na wakimbizi wanaoingia Italia bila wazazi wala walezi, asilimia kubwa ni kutoka nchi ya Misri.
Kwa siku ya maadhimisho ya kimataifa ya haki za watoto, Caritas Italia imeandaa Nyaraka kwa ajili ya kutetea haki msingi za watoto wahamiaji ambao hawakusindikizwa na yeyote walipoingia nchini Italia. Caritas Italia wanasisitiza kutetea haki za watoto hao kwa kuzingatia machafuko ya nchi wanakotoka, ugumu wa maisha na matumaini yao kwa siku za usoni. Kwa muda wa juma zima, Caritas Italia itaendesha warsha katika vituo vyake vya watoto wahamiaji Jijini Roma, kwa wafanyakazi, watu wakujitolea na wadau wote wenye kutetea haki za watoto. Katika warsha hizo, kutakuwa pia na ushuhuda kutoka kwa baadhi ya watoto hao.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Comments
Post a Comment