KUANZA MAJILIO-TAFAKARI


Kesheni kwa vile hamjui siku wala saa ajayo Bwana. Hii ndiyo dhana inayotuongoza katika kuanza majilio. Tunaalikwa kuwa macho, kukesha. Swali ambalo twaweza ulizana – ni kwa nini siku hii ya ujio Bwana inawekwa siri? Mt. Efrem wa Syria anasema – ili tuwe macho, tukikesha. Lakini jibu lingine ni kuwa Mungu atufahamu sana na ikiwa tuna taarifa rasmi ya ujio wake hakika tusingestahimili hilo. Sasa huku kutokujua saa kutufanye tujipange na si kubaki wazembe. Hii itupe nafasi ya kutumia muda wetu vizuri na kutafuta maana halisi ya maisha.
Dante anasema muda unapita, na mtu hatambui hilo. Kuna msemo wa kifaransa usemao ‘utajiri wote wa ulimwengu hauwezi kurudisha nyuma dakika moja iliyopotea’. Naye mwanafalsafa mmoja anasema maisha ni kama luninga – vipindi huja na kupita lakini luninga inabaki pale pale. Dunia inabaki lakini mwanadamu anapita.  Mt. Teresa wa Avila anasema usisumbulie na lo lote, usitishwe na lo lote. Kila kitu kinapita. Mungu pekee abaki. Zaidi sana lakini sisi tunaoamini tunavuka dhana hii ya kupita tu na kuimarishwa na imani inayotutia matumaini makubwa. Tunasoma katika 1Yoh. 2:17 kuwa – ulimwengu utapita na tamaa zake, lakini afanyaye atakalo Mungu atadumu milele. Hii ina maana kuwa yuko adumuye milele, yaani Mungu na kuna njia itufanyayo tudumu milele kama tukifanya mapenzi yake Mungu, tukiishi imani na kumfuata yeye.
Ndugu zangu kipindi cha majilio ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini.Tunakumbuka nini? Tunamkumbuka Yesu Kristo aliyejifanya mtu - tunatafakari uwepo wake na maisha yake hapa duniani kama Mungu na mwanadamu akaupa umaana uwepo wetu sisi – hadhi ya kimungu, akatuonesha maana ya maisha ya Kimungu - eti Mungu akawa mwanadamu. Tumshukuru Mungu.
Tunatumaini nini? Tunatumaini ujio mtakatifu aliotuahidia, jumuiya takatifu na utu uliofungamanishwa na upendo wa Mungu. (Angalia Pope Benedict XVI (Joseph Card Ratzinger) “seek that what is above” 1986 ….. Memory Awakanes Hope. Kumbukumbu zinaamsha matumaini. Tunakumbuka kuwa Mungu amekuja kwetu, akakaa nasi na tunahusisha matumaini yetu kwamba Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu. Katika kipindi cha majilio tunakumbuka matendo makuu ya Mungu na tunatumainia upendo mkuu wa Mungu. Ni kipindi cha kumbukumbu kinachotuwajibisha sana. Hata kama tumepoteza matumaini lakini kumbukumbu ya kimungu bado ipo. Ni muda wa kujirudi kama tutakuwa tumepotoka. Kukumbuka na kutumaini.
Sir Isaac Newton alikuwa mwanasayansi maarufu na alikuwa na mbwa aitwaye diamond. Newton alitumia miaka minane kuandika kitabu chake maarufu cha sayansi. Asubuhi moja baada ya kuamka alikwenda sebuleni na kukuta kitabu chote kimekuwa majivu. Kumbe diamond alikuwa amevuta kitambaa na mshumaa wa mezani na kitabu chote kikawaka moto. Kwa hahika kazi yote ya miaka minane ikawa imepotea, imewaka moto. Hata hivyo hakumkasirikia mbwa wake ambaye hakujua anachofanya. Mara akakaa chini na kuanza tena kukiandika upya. Akakumbuka nia yake na akatumaini kuwa ataweza kuandika upya.
Dante Gabriel Rossetti alikuwa mwanamashairi na msanii maarufu wa karne ya 19. Siku moja alitembelewa na mtu mmoja mzee. Huyo mtu alichukua mkononi michoro ambayo alipenda Rossetti aione na kumwambia kama ilikuwa na thamani yo yote. Rossetti aliiangalia kwa makini na akagundua kuwa haikuwa na thamani yo yote. Kwa unyenyekevu akamweleza ukweli huo yule mzee kuwa haina thamani yo yote. Taarifa hiyo ilimsikitisha sana yule mzee. Hata hivyo yule mzee akamwomba tena Rossetti muda kidogo aangalie picha nyingine alizokuwa ameweka kwenye mfuko mwingine. Rossetti aliangalia na baada ya muda akavutiwa na picha hizo. Rossetti akamwuliza yule mzee mchoraji ni nani na kama alikuwa mtoto wake au la. Huyu anatakiwa apewe msaada wa kila hali ili aendelee mbele, alisema Rossetti. Yule mzee akamwambia kuwa ni picha alizochora miaka arobaini iliyopita akiwa bado kijana. Kwa masikitiko makubwa yule mzee akasema kwa hakika kama angepata maneno ya faraja wakati ule leo hii angekuwa mchoraji maarufu.
Ndugu zangu, katika mantiki hii hatuna budi kuhuisha kumbukumbu zetu na kuishi kwa matumaini makubwa. Ni wajibu wa kila mmoja kwa mwingine. Upo wajibu mkubwa mbele yetu, wa kila mmoja wetu wa kuwa msaada wa kumbukumbu hii na matumaini haya kwa wale tunaomwamini Mungu. Ili wengine wakiona jinsi tunavyoishi kwa matumaini wayakumbuke mapenzi yake Mungu kwetu. Tunasoma katika 1Thes. 5:6-8 kuwa – ‘kwa hiyo tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe na kuwa na kiasi. Maana wenye usingizi hulala usiku, na walevi hulewa usiku. Lakini sisi wana wa mchana tuwe na kiasi; imani na mapendo ziwe kwetu kama ngao ya kifuani; na matumaini ya kuokoka yawe kama kofia yetu ya chuma kichwani’.
Tututafakarishwe na ushuhuda wa Kanali Davenport – wakiwa kwenye kikao cha baraza la wawakilishi huko Marekani ghafla anga likawa giza. Kwa hamaki wajumbe wote wakatizama madirishani wakidhani kuwa ni mwisho wa dunia. Mara ikasikika sauti ya wajumbe wakitaka kikao kiahirishwe. Davenport alisimama akasema, ndugu wajumbe labda siku ya hukumu imefika au bado. Kama ni bado basi hakuna haja ya kuahirisha kikao cha baraza. Ila kama ndo imefika basi nachagua inikute nikitimiza wajibu wangu. Naomba mishumaa iwashwe. Wajumbe wote wakaitika ujumbe, mishumaa ikawashwa na kikao cha baraza kikaendelea.
Kuwa macho ni kuishi maisha hai ya imani huku tukimtumikia Mungu, tukimfuata yeye na kubaki katika neema yake. Mifano ya injili itupe changamoto ya kubaki waaminifu hata kama Bwana mwenyewe kasafiri kwa muda. Hata sisi hatuna namna nyingine ya kumngoja Bwana zaidi ya kubaki wafuasi waaminifu. Tunapoanza kipindi hiki kipya cha mwaka tujitahidi kuwa macho katika roho tukiishi maisha ya ushuhuda wa imani yetu na tukimtumikia Mungu kwa matendo yetu mema kwamba muda wo wote ajapo Bwana atukute tukiwa tayari kuingia katika utukufu wake.
Tumsifu Yesu Kristo
Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI