Ask. Mlola: Huruma ya Mungu ni nguzo kuu ya Kanisa
ASKOFU
wa Jimbo Katoliki Kigoma Mhashamu Joseph Mlola, ALCP/OSS amesema kuwa Huruma ya
Mungu ni nguzo kuu ya Kanisa, kwa kuwa hiyo ndiyo njia inayomuunganisha Mungu na mwanadamu.
Ameeleza hayo wakati wa Ibada
ya Misa ya kufunga Mwaka wa Huruma ya
Mungu Kijimbo iliyofanyika Parokiani Kasulu, iliyohudhuriwa na wawakilishi
kutoka parokia mbalimbali zilizomo Jimboni Kigoma.
Askofu Mlola amesema kuwa
huruma inafungua moyo wa mtu katika matumaini kwa kutambua kwamba, daima
anapendwa, licha ya mapungufu na udhaifu wake wa Kibinadamu.
“Huruma ya Mungu ni sheria
makini inayojikita katika moyo wa mwanadamu na nguzo inayolisimamisha Kanisa.
Katika hili Papa Fransisko naye anakazia umuhimu wa nguvu ya Mungu. Anakiri
kwamba, huruma ya Mungu ni ya milele na kwamba, mwanadamu daima ataendelea kuwa
chini ya jicho la huruma ya Mwenyezi Mungu” ameeleza
Aidha amebainisha kuwa upendo
ni kielelezo cha utendaji wa Mungu na unakuwa ni kielelezo cha kuwatambua
watoto wake wa kweli. Ameasa kuwa wakristo wote wana changamoto ya kumwilisha
huruma, kwani wao wamekuwa ni watu wa kwanza kuonja huruma, kwa kupata msamaha
wa dhambi zilizotendwa, kumbe ni jambo la msingi kwa wakristo kutambua fursa
hii.
“Mara nyingi watu wanadhani
kwamba, si rahisi kuweza kusamehe, lakini ikumbukwe kwamba, msamaha ni chombo
ambacho kimewekwa mikononi mwa binadamu wadhaifu, ili kuweza kupata utulivu
moyoni, ili hatimaye, kuishi kwa furaha” amesema.
Comments
Post a Comment