Papa hajaruhusu talaka - Ask.Niwemugizi
Ametoa tu mwongozo wa kuendesha kesi za ndoa zisizo halali
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara Mhashamu
Severine-Niwemugizi ameeleza kuwa, Kanisa Katoliki haliwezi kuruhusu talaka
wala kuvunja ndoa yoyoye halali.
Akofu Niwemugizi ambaye ni
mtaalamu wa Sheria za Kanisa (Canon law) ameyasema hayo hivi karibuni wakati
akizungumza na gazeti Kiongozi kuhusu utaratibu mpya Papa Fransisko alioutoa
kuhusu kuendesha kesi za ndoa ya Kanisa Katoliki.
“Papa Fransisko ambaye
ndiye kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani pamoja na mamlaka aliyonayo hawezi
kamwe kuruhusu talaka wala kutoa shauri la kuvunja ndoa halali kwani kufanya
hivyo ni kwenda kinyume na Maandiko Matakatifu yanayosema, “Aliyoyaunganisha
Mungu mwanadamu asitenganishe,” ameeleza Askofu Niwemugizi huku akifafanua
zaidi kuwa;
“Jamii imepokea kwa hisia
tofauti matamko mbalimbali ya Papa Fransisko kuhusu ndoa. Wengi wametaka
kumtafsiri Papa kwa kutoa majibu wanayotaka kuyasikia lakini siyo maana halisi
ya Papa. Lengo lake si kutoa talaka.
Papa ametoa mwongozo mpya
wa namna ya kuendesha kesi za ndoa ambazo zilifungwa kinyume na taratibu za
Kanisa Katoliki na hizo ndizo mahaka za Kanisa Katoliki zinazishughulikia ili
kuzitambua rasmi kwamba zilikuwa si halali.
Kanisa halivunji ndoa kamwe
bali linaangalia uhalali wa ndoa ilivyofungwa. Hatuwezi kuibadilisha Biblia kwa
kutenganisha watu waliounganishwa na Mungu licha ya changamoto walizonazo.”
Vizuizi vya ndoa
Akizungumzia juu ya ndoa kuwa
halali, Askofu Niwemugizi amefafanua kuwa, Kanisa lina taratibu na miongozo ya
ndoa.
Sheria za Kanisa can 1083-1125 zinaeleza
utaratibu, uhiari na vizuizi vya ndoa. Huko kuna ufafanuzi juu ya vizuizi 12
vya kufunga ndoa.
Baadhi ya vizuizi hivyo
ni umri wa kufunga ndoa, mtu
kulazimishwa kufunga ndoa, kukosea mchumba ikiwa na maana kuwa, mtu anataka
kufunga ndoa na mchumba wake anayempenda lakini analetewa mwingine aidha kwa
matakwa ya wazazi, jamii nk. ama mapacha wanaofanana nk.
Udanganyifu, pengine mwenzake
alikuwa ameshafunga ndoa na mtu mwingine nk. Ndoa kati ya muumuni mkatoliki na
muumini wa dhehebu lingine.
“Hapa nieleweke kuwa, kila
dini ama dhehebu lina utaratibu wake wa ndoa. Taratibu za Kanisa Katoliki
zinamuelekeza muumini wa Kanisa Katoliki anayetaka kufunga ndoa na muislamu,
mluteri ama dhehebu lingine kupata kibali kutoka kwa askofu wake wa jimbo ili
kwenda kufunga ndoa kwenye dini ama dhehebu lingine nje ya Kanisa Katoliki.
Asipofanya hivyo akaenda kufunga ndoa huko bila kibali ama ruhusa ya Kanisa
hiyo ndoa inatambuliwa kuwa si halali.”
Kizuizi kingine ni kufunga
ndoa na mtu wa karibu wa mwenzi wa ndoa. Ikitokea wanandoa wawili mmoja akaenda
mbali na mwenzake huku nyuma mwenzake akaamua kufunga ndoa na ndugu wa mume ama
mke wake, hiyo ndoa haikufungwa kwa uhalali.
Kufunga ndoa kwa masharti.
Mfano mtu anafunga ndoa ili waishi wawili tu hataki watoto. Ama wanaoana tu ili
wapate watoto. Wasipopata kinakuwa chanzo cha migogoro. Hivyo Kanisa halitambui
ndoa ya masharti.
Askofu Niwemugizi ameeleza
kuwa, Baba Mtakatifu hawezi kukiuka sheria za ndoa na kama akitaka lazima
abadilishe sheria zote za ndoa, miongozo na taratibu zake suala ambalo si
jepesi kwani Kanisa lina taratibu zake. Hata hivyo Papa hawezi kuruhusu talaka.
Kutengua ndoa isiyo halali
Askofu Niwemugizi amelezea
pia mchakato wa mahakama za Kanisa kutangaza ndoa kuwa si halali.
Amesema kuwa, wale wenye
migogoro ya ndoa kulingana na vizuizi 12 vya kufunga ndoa kama ilivyoelezwa
awali wanapaswa kutoa taarifa kwenye mahakama za ndoa ya Kanisa Katoliki.
Mahakama hiyo
itashughulikia suala hilo kwa vigezo na shahidi mbalimbali kulingana na kanuni
za Kanisa. Wakijiridhisha na kuona kuwa ndoa ilifungwa kinyume na taratibu,
watatangaza kuwa ndoa haikuwepo.
Baada ya kutangaza, kama
walikuwa wanamiliki mali, wamepata watoto, mahakama hiyo ya Kanisa inawaelekeza
kwenye mahakama ya kiraia ili waweze kuachanishwa na kusaidiwa namna ya kugawa
mali na kutunza watoto ili wapate haki zao.
Hata hivyo amekubali
utaratibu uliotolewa na Baba Mtakatifu wa namna ya kuendesha kesi za ndoa
akisema ni utaratibu unaoeleweka utakaosaidia kurahisisha mchakato mzima wa
kesi za ndoa.
Comments
Post a Comment