Iweni chachu ya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa!
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa
Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa pia ni fursa kwa waamini kufanya hija
inayowakumbusha kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makao ya
kudumu. Ili kuweza kulifikia Lango la huruma ya Mungu kuna haja ya kuwa na
majitoleo pamoja na kufanya sadaka, kama chemchemi ya wongofu wa ndani; kwa
kushikamana na kuiambata huruma ya Mungu, tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo
vya huruma ya Mungu kwa watu wake!
Mahujaji kutoka katika Nchi za
Scandinavia, Jumanne, tarehe 15 Novemba, 2016 wameadhimisha Ibada ya Misa
takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye
kusalimiwa na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewatakia heri na baraka katika
maadhimisho ya Siku ya Jubilei ya familia ya Mungu kutoka Holland, kielelezo
cha umoja wa Kanisa katika Nchi za Scandinavia pamoja na Khalifa wa Mtakatifu
Petro.
Mwaka wa huruma ya Mungu
umewawezesha waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na Kristo Yesu, Uso wa
huruma ya Baba wa milele, ushuhuda wa Fumbo la upendo wa Mungu usiokuwa na
kifani. Hii ni chemchemi ya uzima wa milele. Watu wote wanahitaji kuonja na
kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, kwani anaokoa, anawajalia maisha
mapya na kupyaisha maisha yao, ili waweze kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu. Kwa
njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waamini wanaonja wema wa ukombozi wa Mungu.
Sakramenti ya Upatanisho ni mahali
ambapo waamini wanapokea zawadi ya msamaha na huruma ya Mungu na huo unakuwa ni
mwanzo wa mabadiliko katika maisha ya waamini na chachu ya mabadiliko pia
katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini
kufungua nyoyo zao ili ziweze kupambwa na huruma ya Mungu, ili wao pia waweze
kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, tayari kuwashirikisha wengine,
msamaha na kushuhudia wema na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Walimwengu wana njaa na kiu ya
kutaka kuonja wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Kumbe, waamini hawa
wanaweza kuwa ni vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuzima kiu ya watu hawa sanjari
na kuwasaidia watu kumgundua Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Kama mitume na
wamissionari wa Yesu wanaweza kumwagilia jamii kwa kutangaza na kushuhudia
Injili inayojikita katika upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.
Comments
Post a Comment