KUHUSU TALAKA: SOMA KWA MAKINI ALICHOMAANISHA PAPA FRANSISKO
Katika mahakama kuu ya ndoa ya
Kanisa Katoliki, yaani Rota Romana, kumefanyika warsha kwa
maaskofu, kuhusu taratibu mpya za uendeshaji wa kesi za ndoa. Warsha hiyo
imefanyika tangu tarehe 17 mpaka 19 Novemba 2016. Taratibu hizo mpya zinalenga
kuharakisha kesi za ndoa na kwa gharama nafuu, ili kuwasaidia waamini walei
ambao ndoa zao ni batili waweze kushughulikiwa kwa wakati na kupatiwa ufumbuzi
kadiri ya misingi ya mafundisho ya Kanisa.
Wakati warsha hiyo ikiendelea, Baba
Mtakatifu Francisko, aliwatembelea maaskofu washiriki hao jioni ya siku ya
Ijumaa, tarehe 18 Novemba, na kuwakumbusha kwamba, ingawa wao ni walimu wa
imani kutokana na hadhi waliyonayo ya uaskofu, ni muhimu kujinoa mara kwa mara,
ili kujibu mahitaji ya wana wa Mungu, wanaotafuta majibu katika Neno la Mungu,
katika kweli ya imani.
Kama ambavyo Mwenyeheri Paulo VI
anafundisha katika Barua yake ya Kitume, Evangelii nuntiandi,
yaani Utangazaji wa Injili, ni lazima kuihubiri Injili kwa namna
ambayo ni halisi kadiri ya hali na mahitaji ya watu. Uinjilishaji usiwe wa
kupambapamba au kulembalemba, bali uingie katika kina cha maisha ya watu, mpaka
kwenye mizizi ya kila wanachofanya, na uinjilishaji huo uanze kwa kumlenga
mwanadamu na kuhitimisha katika mahusiano kati ya wanadamau, na kati ya
wanadamu na Mungu (Rej., Evangelii nuntiandi, 20). Kwa misingi
hiyo hiyo ya kumuweka mwanadamu kuwa kiini cha uinjilishaji, ndiyo sababu
warsha hiyo imeendeshwa katika mahakama hiyo kuu ya ndoa, ili kutafuta wokovu
wa roho za waamini.
Mtume Petro anafundisha juu ya
huduma msingi ya Askofu katika Kanisa: Mlichunge lile kundi la Mungu
mlilokabidhiwa, mlitunze sio kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo
Mungu. Fanyeni kazi hiyo sio kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote.
Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa
hilo kundi. (Rej., IPetro 5: 2-3). Wosia huo unaangaza utume mzima
wa Askofu, ukiwasilisha mamlaka ya kiroho kuwa huduma kwa ajili ya wokovu wa
watu. Kwa mtazamo huo, anahimiza Baba Mtakatifu Francisko, ni lazima kuondoa
vikwazo vyote vinavyozuia waamini wengi kuhudumiwa katika mahakama za
Kanisa. Vikwazo mfano vya kiuchumi au kimikakati na utendaji.
Kufuatia mahusiano yaliyopo kati ya
haki na ukarimu, Sheria za Kanisa haziwezi kukwepa Kanuni yake msingi,
yaani wokovu wa roho za watu. Mahakama za Kanisa ni watumishi wa lengo hilo la
mwisho, lengo linaloakisi Huruma ya Mungu. Kanisa linasafiri katika hija kama
mama anayependa na kukumbatia wote, kama msamaria mwema.
Kanisa linajimwilisha katika kila
hali ya kila mtu, wakiwemo maskini na wanaowekwa pembezoni mwa jamii, hata
ndani ya Kanisa, mfano waliotengana katika ndoa na kujikuta katika mahusiano na
mwenza mwingine tena. Ndani ya Kristu wanamkuta Mchungaji Mwema na Hakimu wa
haki. Hivyo wachungaji makuhani wanapaswa kujituma kuwajali kwa mafundisho na
upendo waamini wote. Taratibu hizo mpya za uendeshaji kesi za ndoa majimboni,
zilitolewa tarehe 15 Agosti 2015, na Baba Mtakatifu Francisko, katika Barua
binafsi, yaani motu proprio, Mitis Iudex Dominus Iesus,
maana yake Bwana Yesu Hakimu wa Haki, akielekeza kupunguza baadhi
ya taratibu zilizokuwa zinapelekea kesi za ndoa kuchukua muda mrefu, na kutumia
gharama kubwa. Kwa taratibu za sasa, Askofu jimbo anayo haki ya kuwa na
mahakama ya ndoa yenye mahakimu watatu wanaoshughulikia kesi moja kwa pamoja
wakisaidiana ili kuhakikisha kwamba ukweli wala mafundisho ya Kanisa
havipotoshwi wala kupindishwa wakati wa kesi. Lakini pia kwa baadhi ya kesi
zenye ushahidi dhahiri usioleta mashaka, uwezekano wa kuwa na hakimu mmoja
Padre.
Katika taratibu hizo, ingawa
maandalizi na uendeshaji wa kesi za ndoa utafanywa na maafisa wa mahakama,
Askofu jimbo mwenyewe ni hakimu kisheria, katika kuthibitisha hukumu ya mwisho
juu ya ubatili wa ndoa husika. Taratibu hizo mpya, bado zinadai kuzingatia
mafundisho msingi ya Kanisa kwamba, ndoa iliyo halali haivunjwi, bali
zinatangazwa batili zilizo batili, tofauti na upotofu uliotolewa na baadhi ya
watu kwamba talaka zimeruhusiwa katika Kanisa Katoliki. Kwa baadhi ya kesi,
Askofu jimbo atazame uhalisia wa maisha ya kiroho ya wahusika baada ya
kutengana, na kuamua inavyofaa ili kuokoa roho zao.
Maafisa wa mahakama za majimbo wawe
wameandaliwa vema kisheria, yaani wawe na utaalamu wa kutosha, na kwa kila kesi
wahakikishe wanafikia uhakika na ukweli kimaadili wanapotoa hukumu. Mahakama ya
Askofu Mkuu itabaki kuwa Mahakama ya Rufaa kwa majimbo yaliyo chini yake,
kadiri ya sheria ya zamani. Mahakama kuu ya ndoa Rota Romana,
inabaki kuwa Mahakama kuu ya rufaa na pia Mahakama ya kesi ya awali iwapo
mwamini ataomba hivyo kwa baadhi ya kesi.
Baraza la Maaskofu Katoliki kwa
kila nchi, lione uwezekano wa kuchangia gharama za mahakama hizo, pale inapowezekana,
ili kupunguza mzigo kwa waamini wasioweza kugharamikia kesi zao.
Hata hivyo Askofu jimbo, aweke
utaratibu utakaowezesha waamini kuchangia gharama za mahakama ya jimbo.
Taratibu hizi tangu zimetolewa hazikuwa zimeeleweka vizuri kwa baadhi ya
Mahakama, hivyo Mahakama kuu ya ndoa, Rota Romana, imeandaa
warsha kwa ajili ya maaskofu wawakilishi toka nchi mbali mbali, ili kutoa
dukuduku na kuweka majibu sahihi ya uendeshaji wa taratibu hizo mpya. Baba
Mtakatifu Francisko kawaasa maaskofu hao kujiaminisha katika uweza wa Roho
Mtakatifu kwenye utendaji wao, kwani ni Roho huyo ndiye mwenye kuliwezesha na
kulitakatifuza Kanisa.
KWA hisani ya: Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Comments
Post a Comment