Wakristo washikamane kujibu kilio cha walimwengu!
Ni jambo la furaha kubwa kutolea
ushuhuda wa Roho wa Bwana kwa kuunganika pamoja wafuasi wa Kristo. Roho
Mtakatifu ni Roho anayeita, anayekusanya, anayeangaza na kutakasa Kanisa zima
la Kristo. Leo hii Roho Mtakatifu anauonesha muujiza wake tena katika tukio kubwa,
ambapo Wakristo wote wanakusanyika kwa nguvu yake, kama ilivyokuwa kwa Kanisa
la kwanza mjini Yerusalem. Hii ni sehemu ya hotuba ya Askofu Munib Younan, Rais
wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kilutheri duniani, katika tukio la
kiekumene nchini Sweden, Jumatatu [31 Oktoba 2016].
Askofu Younan anasema kuwa,
mkusanyiko huo wa Kiekumene ni ushuhuda tosha kwamba, juhudi za pamoja za
kidini zinaweza kujenga jamii ya amani na haki, na kutokomeza chuki na
machafuko. Juhudi za kidini zinaposhiriki katika harakati za umoja na upatano,
dini itanyanyua hali njema za jumuiya za wanadamu. Amesema kuguswa na ushuhuda
uliotolewa na baadhi ya washiriki, kuhusu mahangaiko ya watu duniani, na kwamba
kila mmoja anapaswa kuguswa, sababu kama afundishavyo Mtume Paulo: ndugu mmoja
akipata mateso, jumuiya nzima hupata maumivu, na mmoja akiwa na mafanikio, ni
furaha ya jumuiya nzima [Rej., IWakorintho 12:26]
Mabadiliko ya tabia nchi
yanamuathiri kila mtu, kwa kuanzia na wanyonge zaidi. Kanisa lina nafasi kubwa
ya kutetea haki za kijamii na jinsia katika tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.
Hivyo kawaalika washiriki wote kutochoka wala kukaa kimya katika kutetea haki.
Ameipongeza Serikali ya Colombia na wote walioshiriki katika kutafuta Amani na
wapiganaji wa msituni guerrillas. Kawaalika wananchi wote wa Colombia
kuipa sasa nafasi Amani itawale nchini mwao, ili watu waishi kwa haki na kwa
kuheshimu utu wa mwanadamu. Kwa sababu hiyo wasiipe tena nafasi biashara ya
silaha.
Askofu Younan kawatia moyo pia
wakimbizi wa Burundi na Kenya kuendelea kuombea Amani na kushiriki kadiri ya
nafasi katika kujenga Amani ya kudumu, katika maeneo yao na dunia nzima. Askofu
Younan amesimulia kwamba yeye pia ni mkimbizi wa kipalestina, na wazazi wake
wanatokea Beer Sheva. Akisimulia kumbukumbu za nyakati za nyuma, kawashukuru
jumuiya ya Kiinjili ya kilutheri iliyotenda utume Yerusalemu na kuwasaidia
wakimbizi wengi wakati akiwa mkimbizi. Katoa mwaliko kuendelea kujali wakimbizi
na kuhakikisha wanapata kila mahitaji na kila furaha kwa kuheshimu pia utu wa
kila mmoja.
Ameelezea kwamba, pamoja na ukweli
kuwa haombei Wakristo kufa mashahidi, bado anawatia moyo wote wanaoishi katika
jumuiya ambamo Wakristo wanateswa, wazingatie ujumbe wa Kristo anayewaalika
wasiogope [Rej., Luka 12, 32]. Amewaalika wote kutotulia mpaka Amani itawale
duniani. Makanisa kwa kushirikiana na wote wenye mapenzi mema, watetee haki na
kuhangaikia Amani. Kawaalika pia kuombea Israeli ili Wapalestina na Wayahudi
waweze kuishi kwa Amani, na dini za Kikristo, Kiislamu na Kiyahudi waishi kama
ndugu nchini Israeli.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.
Comments
Post a Comment