‘Teknolojia ya habari iwe fursa ya uinjilishaji’
IMEELEZWA
kuwa kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kunapaswa kuwa chachu
ya kupanuka kwa shughuli za uinjilishaji kupitia mitandao ya kijamii.
Hayo yameelezwa hivi karibuni
katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kwa
wana mawasiliano kutoka nchi wanachama wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Afrika Mashariki (AMECEA), yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
White House, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini Jijini Dar es
salaam.
Akifungua rasmi mafunzo hayo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania, Askofu Bernadin Mfumbusa, ameeleza kuwa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano imerahisisha upatikanaji na kubadilishana taarifa huku mitandao ya
kijamii ikigeuka kuwa sehemu ya maisha ya mwanadamu.
Aidha Askofu Mfumbusa, ambaye
pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, amekumbusha juu ya umuhimu wa kutumia
vyombo vya habari hasa mitandao ya kijamii katika kuinjilisha, kujenga madaraja
na kuimarisha jamii katika nyanja mbalimbali.
“Ujumbe wa Papa Fransisko
katika Siku ya 50 ya Upashanaji Habari Duniani, ambao ulikuwa na dhima ya
‘mawasiliano na huruma; makutano yenye tija’, unatualika sote kutathmini
uhusiano uliopo baina ya mawasiliano na huruma. Papa anasema kuwa mawasiliano
yana nguvu ya kujenga madaraja, kuwezesha watu kukutana na kushirikishana, na
hivyo kuimarisha jamii” ameeleza.
Kwa upande wake Padri Gallus
Marandu, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
ameeleza kuwa kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kunapaswa kusaidia
jitihada za kushirikishana maadili ya Injili kwa ajili ya kuendeleza dhamira ya
Kanisa katika uinjilishaji.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na
wana mawasiliano kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Tanzania, Kenya, Uganda,
Malawi, Ethiopia, na Zambia.
Comments
Post a Comment