Kard.Pengo: Kufunga Mwaka wa Huruma ni kufungua milango ya msamaha
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo amesema kuwa, kufunga Yubilei ya Huruma ya Mungu ni kufungua
upya Huruma ya Mungu kwa wanadamu.
Mwadhama ameeleza hayo hivi
karibuni wakati wa Misa Takatifu ya kufunga Yubilei ya Huruma ya Mungu katika
Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
“Tumefunga mwaka wa Huruma ya
Mungu, ikiwa ni kufungua upya mahusiano yetu na Mungu. Ni kufungua milango ya
Huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu na mahusiano kati ya mwanadamu na
mwanadamu. Kujitambua kwamba sisi ni wakosefu na kwamba tunahitaji Huruma ya
Mungu kwa unyenyekevu, "amesema Kardinali Pengo.
Aidha Kardinali Pengo amewaasa waamini kuwa, Yubilei ya Huruma ya Mungu kilikuwa kipindi cha kujifunga, kutafakari Huruma ya Mungu. Hivyo kufunga mwaka huo Mtakatifu haimaanishi kutupilia mbali Huruma ya Mungu, bali kuiishi kwa matendo yanayoonyesha kuwa wanatambua Huruma hiyo.
“Injili ya Luka inaonesha mfano
wa watu wawili, mfarisayo na mtoza ushuru. Mfarisayo alijiona hahitaji Huruma
ya Mungu hivyo ana mastahili zaidi kuliko mtoza ushuru. Akajigamba akisema
anamshukuru Mungu kwani hayuko kama mtoza ushuru . Anasali, anafunga kuliko
wenzake, mwishowe akarudi nyumbani akiwa hana haki mbele ya Mungu.
Mtoza ushuru alijiona mnyonge
asiye na mastahili mbele ya Mungu hivyo akamuendea Mungu akijiona hana sifa ya
kukaa mbele ya Mungu akaomba Mungu amsamehe dhambi zake. Yesu anasema aliondoka
akiwa na haki mbele za Mungu zaidi kuliko mfarisayo.
Hiyo ndiyo maana ya Yubilei ya Huruma ya Mungu. Kujiona kuwa hatuna mastahili mbele ya Mungu. Tunahitaji kuomba Huruma ya Mungu na wanadamu wenzetu. Kuwa tayari kuomba msamaha na kutoa msamaha. Kuipa thamani Sakramenti ya kitubio.
Milango ya msamaha inafunguliwa upya katika Kanisa kwa ajili ya maisha yetu yote.
Kuja mbele ya Mungu na kusema, Ee Mungu unihurumie mimi ni mwenye dhambi. Anayejiona kinyume na hilo ni mfarisayo na anaishi kinyume bila neema ya Mungu,"ameeleza Kardinali Pengo.
Amewaasa waamini kuwa na huruma
ya kuwasamehe wengine hasa wale waliowakosea vikubwa zaidi. Amesema kuwa
kusamehe kunampa mwanadamu nafasi ya kuona kuwa hata yeye anahitaji kuhurumiwa
na Mungu na wengine.
Amewaasa mapadri kuwa tayari kutoa Sakramenti ya kitubio kila siku na kwa muda wowote kwani milango ya Huruma ya Mungu imefunguliwa upya kwa wanadamu.
Comments
Post a Comment