Kanuni za kuzingatia kuhusiana na vitega uchumi vya watawa
Kongamano la Pili la Kimataifa
kuhusu uchumi, lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya
Kitawa na Kazi za kitume lililofunguliwa hapo tarehe 25 Novemba 2016 limefungwa
rasmi, Jumapili tarehe 27 Novemba 2016 kwa kutoa mwongozo unaopaswa kufanyiwa
kazi na watawa kwa siku za usoni ili kuendelea kuwa waaminifu kwa karama za
Mashirika yao, huku wakiwa na mwelekeo mpana zaidi kuhusiana na masuala ya
kiuchumi.
Kardinali Joao Braz de Aviz,
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume
amewakumbusha watawa kwamba, wanapaswa kuwa makini zaidi na masuala ya
kiuchumi, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia weledi, ujuzi, mang’amuzi na
historia ya Mashirika yao, ili kuendelea kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za
Kiinjili hata katika masuala ya kiuchumi. Lengo ni kuendelea kuwa waaminifu kwa
karama za Mashirika haya, lakini kwa kusoma alama za nyakati pamoja na
kuangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya uchumi na
maendeleo pamoja na athari zake kwa utu na heshima ya binadamu.
Kardinali Joao Braz de Aviz anakaza
kusema, Mashirika ya Kitawa yamewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu,
afya na maendeleo endelevu ya binadamu. Hapa kuna haja ya kuwa makini na Sheria
za Kanisa pamoja na Sheria za Nchi husika; mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa
upembuzi yakinifu ili kuweza kuleta mabadiliko yanayokusudiwa kadiri ya
Mafundisho ya Kanisa kwa wakati huu. Hapa maamuzi ya sera, mikakati na
utekelezaji wake yanapaswa kufanywa na Shirika zima na wala si maamuzi ya mtu
mmoja au kikundi cha watu wachache, ili kuweza kujenga uwajibikaji wa pamoja.
Ikumbukwe kwamba, rasilimali fedha
na watu ni mali ya Kanisa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa
kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wajumbe wa kongamano
baada ya kujadili kwa kina na mapana kuhusu: karama, uaminifu na mwelekeo mpya
wa masuala ya kiuchumi, waliunda kikosi kazi kilichokuwa kinawajumuisha:
wanasheria, wachumi na wataalam mbali mbali ili kuweza kutoa mapendekezo ambayo
yatawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa
siku za usoni katika sekta ya afya, elimu na maendeleo endelevu sehemu mbali
mbali za dunia!
Kongamano hili ni matunda ya
maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, uliowachangamotisha watawa kuwa kweli
ni cheche za matumaini kwa kusikiliza Neno la Mungu pamoja na kufikiri, kuamua
na kutenda mintarafu dhana ya Sinodi inayoendelea kushika kasi katika maisha na
utume wa Kanisa, ili kuwa na maamuzi fungamanishi. Nadhiri za kitawa anasema
Sr. Nicla Spezzati, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya
Kitawa na Kazi za kitume, ni kioo cha maisha, utume na mahusiano yao na
walimwengu mintarafu karama za Mashirika yao. Huu ni mwaliko wa kujenga na
kuimarisha mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii. Watawa wawe mstari wa mbele kulinda na kutetea utu,
heshima, haki, ustawi na mafao ya wengi kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume
wao. Utajiri wa karama na rasilimali fedha na watu, visaidie kupambana na baa
la umaskini na changamoto zinazowakabili maskini na wale wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii.
Askofu mkuu Josè Rodriguez
Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za
kitume amewasilisha mambo makuu matano yanayopaswa kuzingatiwa na Mashirika ya
Kitawa na Kazi za kitume kuhusiana na masuala ya uchumi na vitega uchumi. Mosi,
Uaminifu kwa karama maana yake ni kuendeleza utume pamoja na kuwa na matumizi
sahihi ya rasilimali ya Shirika kwa ajili ya huduma kwa karama.
Pili, utunzaji bora wa mali ya
Kanisa. Watawa wanapaswa kuwa makini katika kulinda mali ya Kanisa ili kuweza
kujitosheleza katika mahitaji yao msingi pamoja na maendeleo ya Shirika kwa
siku za usoni. Tatu ni mwendelezo wa vitega uchumi vya Shirika hapa ieleweke
kuwa ni mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu ili kuhakiki pamoja na kuwa
makini ili kuangalia ikiwa kama miradi husika inaweza kujiendesha, kwa
kuendelea kuwa waaminifu kwa karama pamoja na uwiano mzuri wa kiuchumi.
Nne, uwajibikaji wa kutoa taarifa:
kwa kuonesha malengo na mbinu mkakati zitakazotumiwa ili kufikia malengo husika
kwa kuzingatia: Sheria za Kanisa na Sheria za nchi pamoja na kuhakikisha
kwamba, taarifa zinatolewa kwa wakati muafaka kuhusu utekelezaji wa miradi na
vitega uchumi vilivyopo! Tano ni ufukara, yaani kutumia rasilimali vitu na
fedha kwa lengo na nia husika pamoja na kuhakikisha kwamba, wanaondokana na
dhana ya kuwa ni wamiliki wa mali husika, bali wasimamizi na waratibu wa
rasilimali ya Kanisa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa kina
unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo
anahitimisha kwa kusema kwamba, kuna vigezo vingine vinavyoweza kuongezwa
kutokana na hali halisi ya Shirika husika, vitega uchumi na kazi zinazoendeshwa
mintarafu mahali na mazingira; sheria zilizopo na utekelezaji wake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.
Comments
Post a Comment