WAWATA WAASWA KUJITOA KWA HALI NA MALI
CHAMA cha kitume cha wakina
mama wa Kanisa Katoliki Tanzania(WAWATA)
kimetakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika uinjilishaji kwa kujitoa kwa hali na
mali na kuwafikia waamini wengi zaidi.
Akizungumza katika tamasha lililoandaliwa na WAWATA dekania ya Ubungo na
kufanyika katika Parokia ya Mtakatifu Gaudence Makoka jijini Dar-es-salaam,
Mwenyekiti wa WAWATA dekania ya Ubungo Bi.Judith Mndolwa amewataka WAWATA
popote walipo katika parokia, kanda, dekania na jumuiya kuacha kuwa watu wa
matukio pekee kwa kuhudhuria matamasha na kusahau wajibu wao.
Ameongeza kuwa WAWATA
wanapaswa kukutana mara kwa mara, kushauriana, kujitoa kwa wahitaji na pia wawe
na moyo wa msamaha.
Pia amebainisha kuwa ni jukumu la
WAWATA kuhakikisha kuwa vijana wa kike kuanzia miaka 14-18 wanaandaliwa kuwa
mbadala katika utume hapo baadaye.
Katika tamasha hilo WAWATA
walikuwa wakisherekea mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu na kumuenzi somo wao
ambaye ni mama Bikira Maria na Mgeni rasmi katika tamasha hilo alikuwa Padri
Sahayaraj Michael CMF Paroko wa Parokia ya Kimara. Wageni wengine waliohudhuria
ni pamoja na mapadri Evarist Tarimoi, Padri John Slinger wa Parokia ya Tandale
pamoja na watawa.
Kwa upande wake Padri
Sahayaraj Michael katika mahubiri wakati wa ibada ya misa takatifu katika tamasha hilo amewataka WAWATA kuwa na
utii, utulivu na upole kwa maana mwanamke mtulivu ni tunu ya Bwana (Yb Sira 26;13-14) na pia
amewataka wajue wajibu wao katika familia na wasisahau familia zao kwa ajili ya
Malimwengu (Petro 3;1-4).
Kuhusu changamoto ya fedha
inayowakabili WAWATA, mgeni rasmi amewashauri kujitoa wao kwa wao kulingana na
kazi zao kwani kufanya hivyo kutawafanya wafikie malengo.
Kutokana na ushauri
mzuri wa mgeni rasmi Padri Sahayaraj Michael CMF harambee ilifanyika kwa ajili
ya kutunisha mfuko wa WAWATA dekania, hivyo zikapatikana fedha tasilimu shilingi
345,550, ahadi za WAWATA parokia 13 shilingi 3,900,000 na wageni waalikwa
mbalimbali na watu binafsi ahadi shilingi 1,465000 na kufanya jumla ya fedha
tasilimu kuwa 955,750, ahadi 5,365,000 na jumla kuu shilingi 6,320,750.
Pia WAWATA wamefanya matendo ya
huruma kwa chama cha kitume cha Vicent
wa Paulo kwa ajili ya wahitaji mbalimbali
Parokia ya Makoka ambapo wametoa mchele kilo 100, maharage kilo 100, sukari
kilo 100, chumvi kilo 50 na sabuni za kufulia na kuogea vyote vikiwa na thamani
ya shillingi 660,000.
Philipo Josephat, Dsm
inapendeza sana akina mama kujitokeza katika kumtumikia Mungu, Kwani inatia moyo hata katika kizazi hiki ambacho hakimjui Mungu. mama akiwa mtumishi mzuri wa Mungu basi hata mtoto atafuata malezi mazuri ya mama! kwa upendo wa kristo tunamtumikia na kuwajibika!
ReplyDelete