Askofu Nzigilwa: Watunzeni Watawa
Askofu msaidizi wa jimbo kuu
katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa ametoa wito kwa walei wote
kuwa ni jukumu lao kuwalea na kuwatunza watawa popote walipo.
Akizungumza katika mahubiri ya misa
takatifu iliyofanyika katika parokia ya Mtakatifu Annastazia na Frolian iliyopo
Kigamboni Kimbiji(Kidagaa) jijini Dar es salaam, Askofu Nzigilwa ametoa wito
kwa waamini kwa kushirikiana na majimbo kuwa bega kwa bega na watawa jambo
ambalo litasaidia kurahisisha kazi ya kuitangaza injili.
Askofu Nzigilwa ambaye alikuwa
mgeni rasmi parokiani hapo katika uzinduzi wa nyumba mpya za watawa (masista)
amewataka walei wa Kimbiji (kidagaa) kuwapokea watawa hao na kuwapa ushirikiano
wa hali na mali katika kazi mbalimbali za kijamii na kiimani.
Parokia ya Mtakatifu Annastazia
na Frolian inaongozwa na Paroko Luchano na msaidizi wake padri Justus Rugaiyukamu
ambapo kwa kipindi kirefu wamekuwa peke yao parokiani hapo.
Parokia hiyo inajumuisha vigango
vinne ambavyo ni Mbutu, Buyuni, Puna na Ngobanya.
Askofu Eusebius Nzigilwa pia
ametoa sakramenti ya kipaimara kwa vijana wanne parokiani hapo.
Comments
Post a Comment