Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa makini kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa; tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Kimsingi hili ndilo lililokuwa lengo kuu la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uliohitimishwa kwa Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 20 Novemba 2016. Haya yamesemwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatatu tarehe 21 Novemba 2016, kama sehemu ya mchakato wa uzinduzi wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Misericordia et misera” “Huruma na haki”.
Huu ni waraka wa kitume uliondikwa na Baba Mtakatifu kama sehemu ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma na Mungu inayopaswa kuendelezwa katika maisha ya waamini kama kielelezo cha huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka. Huruma ya Mungu inayojionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa lakini kwa namna ya pekee kabisa Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa.

Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba,  Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Hapa Mapadre wahubiri wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanaandaa mahubiri yao vyema na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayojikita katika: ukarimu, ushuhuda wa maisha, msukumo wa kichungaji, uwazi na utayari wa kutoa huduma ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Mapadre sasa wanaweza kuwaondolea watu dhambi ya utoaji mimba.

Askofu mkuu Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: Uso wa huruma “Misericordia vultus” na “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” ni nyaraka zinazoweza kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini ukuu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto anasema Baba Mtakatifu ni kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kwa njia hii, Kanisa litaendelea kuwa kweli ni shuhuda wa huruma ya Mungu na utambulisho wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi kwa waamini kurejea katika mambo msingi ya imani, maisha ya kiroho, sala, tafakari na hija. Ijumaa ya huruma ya Mungu, imekuwa ni siku ya pekee ya kuweza kuonja shida, magumu na changamoto ya watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kielelezo cha Kanisa linalosikiliza kilio cha watu na kuwajibu kwa wakati muafaka!

Askofu mkuu Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kamwe hayakulenga kuwa ni kichocheo cha utalii wa ndani na nje ya Italia, hasa wakati huu wa athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kwa wale waliotarajia kufaidika kiuchumi kwa sasa “wataisoma namba”. Zaidi ya waamini millioni 21 kutoka katika mataifa 156 wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapa mjini Roma. Lakini pia ikumbukwe kwamba, kuna mamillioni ya waamini waliovuka malango ya huruma ya Mungu majimboni mwao, kwani Jubilei ya huruma ya Mungu lilikua ni tukio la kiulimwengu  na wala si tu kwa ajili ya Roma.

Takwimu za jumla zinaonesha kwamba, kati ya waamini wa Kanisa Katoliki millioni 900 hadi 950 wamevuka malango ya huruma ya Mungu majimboni mwao. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamekuwa yakifuatiliwa na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa njia ya mitandao mbali mbali ya kijamii. Hapa anasema Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella kumekuwepo na ufanisi mkubwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” amewathibitisha Wamissionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuwaondolea waamini vikwazo na vizingiti vilivyokuwa vinawazuia kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya wongofu wa ndani, toba, msamaha na upatanisho. Mapadre kwa nguvu ya Sakramenti waliyoipokea sasa wameongezewa madaraka ya kuweza hata kusamehe dhambi ya utoaji mimba ambayo hapo awali ilikuwa imeachwa rasmi kwa Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lengo ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki.

Waraka wa kitume “Misericordia et misera” ni mwaliko wa kumwilisha huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii kwa njia ya umoja na mshikamano wa upendo. Kuanzia sasa, Kanisa linapenda kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini ndiyo maana kila mwaka Jumapili ya XXXIII ya Mwaka wa Kanisa itaadhimishwa Siku ya Maskini Duniani ili kutoa nafasi kwa Kanisa kutafakari kuhusu maskini ambao kimsingi ni amana, hazina na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Lengo kuu ni kujenga misingi ya haki jamii kwani hakuna haki na amani ya kweli, ikiwa kama bado kuna makundi makubwa ya Maskini wanaoteseka kwa njaa, magonjwa, utupu na upweke katika maisha.

Huruma ni kielelezo makini cha imani na ushuhuda wa Kikristo. Huu ni mwaliko wa kutafakari dhana ya umaskini duniani kwa kutumia miwani ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga utamaduni wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu, kwa kuwathamini, kuwajali na kuwasaidia kadiri ya uwezo na fursa zilizopo anahitimisha uzinduzi wa Waraka huu wa kichungaji “Misericordia et misera” Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI