“iishini imani katoliki” Askofu Mkuu Paulo Ruzoka
Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo kuu katoliki Tabora amewaasa
waamini wote kuishi Imani katoliki katika kuwajali watu wenye shida mbalimbali
katika jamii ili kuendelea kuuenzi mwaka wa huruma ya Mungu katika maisha yao.
Kauli hiyo ameitoa katika eneo la mlima wa Maongozi ya
Huruma ya Mungu Ifucha katika parokia ya Ipuli Jimboni Tabora wakati wa
kuhitimisha mwaka wa huruma ya Mungu kijimbo.
Kabla ya adhimisho la Misa Takatifu Askofu Mkuu Paulo
Ruzoka, mapadri, watawa na waamini walipanda mlimani na kubariki msalaba
mtakatifu ambao unaashiria uwepo wa huruma ya Mungu kupitia Kristo Yesu aliye
uso wa huruma ya Mungu kwa wanadamu wote.
Mara baada ya Kubariki msalaba mtakatifu, Misa Takatifu
iliadhimishwa na mahubiri yake yakalenga uzinduzi wa kituo hicho cha Hija kuwa
waamini wote wanaalikwa kufika eneo hilo ili kusali, kutafakari maisha yao ili
kuwa tayari kumrudia Mungu na kupata utulivu ndani ya nafsi zao.
Aidha Askofu Mkuu Ruzoka amesema dunia ya leo na watu wa leo
wanakosa amani na utulivu wa roho matokeo yake ni hasira mioyoni mwa wanadamu
hivyo ni vema waamini wakafika eneo hilo na kusali ili wapate utulivu au wapoze
roho zao na ndiyo maana halisi ya neno IFUCHA NG'HOLO tuliza roho au poza roho.
Akitoa mahubiri yake wakati wa Misa Takatifu , Askofu Mkuu
amesema kanisa mama au mzazi anayesaidia waamini kuitwa watoto wa Mungu kupitia
sakrament za kanisa, hivyo waamini wapokee sakramenti kwa moyo wa imani na
uchaji ili ziwasaidie katika safari yao ya kumwendea Mungu.
Sambamba na hilo Askofu Mkuu amewakumbusha mapadri wote kuwa
makini wanapoadhimisha sakramenti hizo hasa sakramenti ya Kitubio ambayo kwayo
waamini wanapokea huruma ya Mungu anayechukua mizigo yao kwa upole na
unyenyekevu.
Katika sherehe ya kuhitimisha mwaka wa Huruma Mungu Kijimbo,
pia sherehe ya familia ya Mungu kwa wanajimbo ilifanyika ambapo waamini
walichangia fedha na vitu ili kusaidia gharama mbalimbali za uendeshaji wa
ofisi ya Askofu.
Katika adhimisho hilo la Misa Takatifu pia wageni mbalimbali
walialikwa wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi na waamini wa dini na
madhehebu mbalimbali toka mkoani Tabora na wenyeji wa eneo hilo la kijiji.
Matarajio ni kuwa kila mwaka tarehe na mwezi huo waamini
wote wa Jimbo kuu Tabora watakuwa wakienda hija katika eneo hiloEneo hilo
ambalo limewekwa chini ya usimamizi wa watakatifu Yohana Paulo wa pili na
Terezia wa Calcata.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tabora Manispaa Mwl Queen Mlozi
akiongea kwa niaba ya Serikali amesema hitimisho la mwaka huu wa huruma lisaidie
wananchi kuacha vitendo viovu hasa mauaji yanayoiweka Tabora kuwa kinara kwa
mauaji ya walemavu wa ngozi albino, wazee na vikongwe kwa imani za kishirikina.
Pia amewahimiza wana Tabora wajiepushe na matukio ya
ujambazi, mimba za utotoni kwa watoto wa kike na kuwapa nafasi sawa ya kusoma
kama ile ya watoto wa kiume na kuwataka wazazi kuwaruhusu watoto wa kike kupewa
nafasi ya kuvaa kile alichokiita magauni manne kwa utaratibu wa serikali.
Mkuu wa huyo wa Wilaya amewaomba wana Tabora kujipanga ili
kunufaika na ujio wa barabara za lami, huduma bora za reli, ujio wa ndege za
serikali, na uhamiaji wa makao makuu ya serikali Dodoma vyote vimsaidie mwana Tabora
kuboresha maisha yake, kutoka alipo na kwenda mbele.
Pia amethibitisha kwamba serikali ya Tanzania inatambua
michango ya afya, elimu, maji na huduma zote za jamii zinazotolewa na kanisa na
kwamba serikali ipo tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika.
Comments
Post a Comment