“Utandawazi uwe na kiasi” Ask. Msonganzila
Askofu
wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila amewakumbusha watawa na
mapadri kuweka mipaka ya dhati kati yao na Mungu, na kuacha kutumia muda
mwingi katika utandawazi huku kiapo chao kikiwa ni uaminifu, unyeyenyekevu na
kuwa na maisha ya sala.
Askofu Msonganzila ameyasema hayo wakati wa ibada ya kufunga
lango la Huruma iliyofanyika katika Kanisa la Kiabakari ambapo mahujaji
kutoka sehemu mbalimbali wamefika kanisani hapo, kwa ajili ya kumshukuru Mungu
kwa mambo mengi aliyowatendea katika kipindi chote cha kuadhimisha ibada
Takatifu ya Huruma ya Mungu.
Askofu Msonganzila amesema utandawazi unaonekana
kuwachukulia muda mwingi baadhi ya mapadri na watawa hadi kusababisha muda wa maisha
ya sala ya kila siku kupungua kutokana na kutumia muda mwingi katika
utandawazi ambapo amewasihi kujitahidi kuepuka mazingira yoyote ambayo yanaweza
kuwa kikwazo kwao na kuwafanya kutokuwa karibu na Mungu.
“ Kiapo chenu ni uaminifu kwa Mungu ukichanganya maisha hayo
mliyonayo itakuwa ni masikitiko makubwa sana,wekeni mipaka ya dhati kati yenu
na mitandao, kwa kuongeza maisha ya sala kila siku na kupokea
Huruma ya Mungu kwa kusaidiana ninyi kwa ninyi, kutoachana na kuheshimiana
ninyi wenyewe,” amesema Askofu Msonganzila.
Amesema kuwa ni kitu cha msingi sana kuacha dhambi na
pia hakuna sababu ya kuona aibu kuiacha, kwa kuwa dhambi imekuwa kikwazo
kikubwa kwa watu wengi kutoingia mbinguni, hivyo kuna kila sababu ya kuiacha na
kuwa karibu na Mungu kwani mara nyingi watu wameonekana wema,
wapole, wenye unyenyekevu kwenye jumuiya na kanisani kumbe
upole huo na utakatifu huo unafunikwa kwa ngozi ya kondoo ndani ni simba huku
moyoni ikiwa imejaa chuki, ubinafsi na uchoyo.
Aliongeza kuwa mapadri na watawa hawana budi kuepuka
roho za chuki, hasira, ubinafsi bali wajitahidi kuonja huruma ya Mungu
kila mahali, hasa sehemu za kazi kwa kudumisha upendo wa kweli katika
maisha yao ya kila siku.
Paroko wa parokia ya Kiabakari Padri Woicheck amemshukuru Baba
Askofu wa Jimbo hilo kwa kukubali parokia yake kuwa kituo kikubwa cha
Hija ambacho kina lengo la kupokea makundi mbalimbali ya mahujaji kutoka
ndani na nje ya Jimbo ya Musoma.
Comments
Post a Comment