Ask. Lebulu: Tuwapende hata wale wanaotupiga vita
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Mhashamu Josaphat Lebulu amesema kuwa huruma
ya Mungu inatoa fursa kwa wanadamu kudumu katika upendo, kwa kuwapenda hata
wale wanaowapiga vita, kama Mungu alivyo tayari kuwasamehe wema na wabaya.
Ameeleza hayo wakati wa
Adhimisho la Misa Takatifu ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya
Mungu jimboni Arusha, lililofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu
Thereza, na kuhudhuriwa na mamia ya waamini wa jimbo hilo.
Askofu Lebulu amesema kuwa
baada ya kufungwa kwa yubilei hiyo, waamini wanaalikwa kutoka na kuionesha
huruma ya Mungu kwa watu wote hasa wanaoihitaji zaidi. Ametoa rai kwa waamini
hao kuitambua huruma ya Mungu, inayotenda kazi kati ya watu na ndani ya watu.
“Leo tunafunga yubilei ya
huruma na siyo kufunga huruma ya Mungu. Tunafunga yubilei na sasa tuendelee
mbele tukiwa kama watu tuliofaidi huruma ya Mungu. Tuendelee na hamasa
tuliyoionja katika fursa mbalimbali kama makongamano na hija” ameeleza Askofu
Lebulu.
Aidha Askofu Lebulu ametoa rai
kwa waamini kuwa tayari kusamehe wengine, na kupokea msamaha kutoka kwa wenzao,
ili waweze kuushinda ubaya kwa wema.
Pia amewatoa mashaka waamini
ambao wanajihoji iwapo watadumu katika mema waliyoyachuma ndani ya mwaka wa
huruma ya Mungu, na kuwaambia kuwa hawana budi kujipa moyo na kusonga mbele kwa
kuwa Kristo wanayemtumaini ameushinda ulimwengu.
Comments
Post a Comment