‘Hifadhini vizuri nyaraka za kanisa’
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila
amewakumbusha maparoko wa Jimbo hilo kuhakikisha wanatunza kumbukumbu muhimu na
nyaraka zote za kanisa, ili kuondoa migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza baina
ya walei na wahudumu wa Kanisa.
Ameyasema hayo
wakati wa Misa Takatifu ya uzinduzi wa Parokia mpya ya Huruma ya Mungu Kigera,
iliyofanyika Kanisani hapo, sambamba na kutabaruku Altare, kubariki waamini,
kanisa na vitu vyote vilivyomo ndani na nje ya kanisa hilo.
Askofu
Msonganzila amesema kuwa makanisa mengi yamekuwa yakiingia migogoro na wananchi
(walei) kutokana na kutokuwepo kwa nyaraka muhimu za kanisa kutokana na
maparoko ambao ndio wasimamizi wa eneo husika, kutotunza nyaraka hizo vizuri,
kwa ajili ya kukumbukumbu za baadaye.
Amezitaja nyaraka
muhimu ambazo maparoko wanapaswa kuhakikisha zinatunzwa vizuri kuwa ni pamoja
na kitabu cha wabatizwa wote pamoja na
wasimamizi wao, kitabu cha waliopata kipaimara pamoja na waliopata kumunyo ya
kwanza, kitabu chenye taarifa zote za waliofunga ndoa na kuwapatia vyeti vyao
kwa kuwa vyeti ni mali ya Serikali,v itabu vya mahesabu ya Parokia (yaani
mapato na matumizi) kwa kufuata sheria
zote za Serikali kuhusu wahudumu wa taasisi wanaolipwa mishahara pamoja na
kutoa risiti.
Pia kitabu
kinachoonyesha mali ya kanisa inayohamishika na isiyohamishika, kuweka alama za
mipaka ya eneo lote la kanisa, kwani baadhi ya walei wana tabia ya kuingia
katika eneo la kanisa mara wanaposikia kuwa kanisa limekuwa parokia ili kuibua
migogoro, sambamba na kupiga picha za kumbukumbu wakati mabwana ardhi wanaweka
alama za mipaka ya kanisa haraka.
Hata hivyo
amewapa angalizo maparoko hao kuwa wakristo wengi hasa wakatoliki wamekuwa
mbele sana katika mizozo mikubwa ya masuala ya ardhi katika maeneo ya kanisa
hivyo hawana budi kuwaeleza ukweli wa mambo waamini wao bila kuwaficha japokuwa
wapo watakaopenda kuambiwa ukweli na ambao hawatapenda kuambiwa ukweli, ila cha
msingi wahakikishe wanayafanya hayo.
Comments
Post a Comment