WANACHUO 2,739 WASITISHIWA MIKOPO
BODI
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesitisha kwa muda
mikopo kwa wanafunzi 2,739 walioshindwa kujitokeza wakati wa kuhakiki
wanufaika wa mikopo hiyo.
Aidha,
imetoa siku saba kuanzia jana kwa wanafunzi ambao hawakuhakikiwa kwenda
kuhakiki katika vyuo vyao, vinginevyo mikopo yao itafutwa na kutakiwa
kurejesha kiasi walichokopeshwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Jerry Sabi,
alisema hatua hiyo imetokana na kuwatilia shaka wanafunzi walioshindwa
kujitokeza kuhakikiwa.
“Tumesitisha
mikopo kwa wasiohakikiwa kwa sababu hatujui kama ni wanafunzi halali au
hewa. Tunataka kuwahakiki pia kwa kuwa hatujui kama wakati tunahakiki
wengine walikuwa wagonjwa au wamerudia mwaka au wana sababu nyingine,”alisema.
Mei
mwaka huu, Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako, aliagiza kufanyika uhakiki kwenye taasisi za
elimu ya juu nchini kubaini kama kuna uwepo wa wanafunzi wasiostahili
kupata mikopo.
Kuanzia
Mei 30, mwaka huu, HESLB ilifanya uhakiki katika vyuo 26 na tayari
imeshafanya uchambuzi wa uhakiki kwa vyuo 18 kati ya hivyo.
Akizungumzia
uhakiki huo, Sabi alisema ulifanywa na timu maalumu iliyoundwa na Bodi
kwa kuhakikiwa mwanafunzi husika na kubaini kuwa wanafunzi 2, 739
hawakujitokeza kuhakikiwa. Aliongeza kuwa, Uchambuzi katika vyuo vinane
unaendelea.
Hata
hivyo, bodi hiyo haikueleza ni wanafunzi wangapi walihakikiwa katika
vyuo ambavyo kazi ya uhakiki imefanyika. Alisema bodi itafanya uhakiki
wa awamu ya pili ili kujiridhisha kabla ya kuwatangaza kuwa ni wanafunzi
hewa na fedha ambazo zitakuwa zimeokolewa kutokana na kuwabaini
wanafunzi hao.
Alisema
majina ya wanafunzi ambao hawakujitokeza kuhakikiwa wakati wa uhakiki
vyuoni yamewekwa kwenye tovuti ya Bodi na pia katika vyuo ambavyo
vitafanya utaratibu wa awamu ya pili ya uhakiki.
Alivitaja
vyuo vilivyohakikiwa, kufanyiwa uchambuzi wa awali na idadi ya
wanafunzi ambao hawakujitokeza kuhakikiwa kwenye mabano kuwa ni Chuo
Kikuu cha Dodoma (763), Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (126), Chuo Kikuu
cha Mtakatifu Augustino- Mwanza( 232), Chuo Kikuu cha Mzumbe (66) na
Chuo Kikuu cha Teofilo Kisaji-Mbeya (130).
Vingine
ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino-Mbeya (21), Chuo cha Mtakatifu
Yohane- Dodoma (262), Chuo Kikuu cha Mkwawa (103), Chuo Kikuu cha Iringa
(100) na Chuo Kikuu cha Tiba-Bugando (43), Chuo Kikuu cha Arusha (55),
Chuo Kikuu cha Jordan (128), Chuo Kikuu cha Makumira- Arusha (98), Chuo
Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (385), Chuo cha Ufundi Arusha (22), Chuo
Kikuu cha Waislamu-Morogoro (130), Chuo cha Uhasibu (57) na Chuo Kikuu
cha Mount Meru (17).
Sabi alisema kutokana na kuwepo wanafunzi ambao hawajajitokeza, muda wa uhakiki umeongezwa hadi Agosti, mwaka huu.
Comments
Post a Comment