PAPA FRANCISKO AENDELEA KUAMINI KATIKA MAJADILIANO YA KIDINI
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu analihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linakuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani kwani huruma ya Mungu inavuka mipaka ya Kanisa na kumwambata kila mwamini. Waamini wa dini ya Kiislam wanamtambua Mungu kuwa ni Muumbaji, mwingi wa huruma na mpole.
Hizi ni sifa za Mwenyezi Mungu zinazowasindikiza na kuwategemeza waamini wa dini ya Kiislam katika udhaifu wao wa kibinadamu. Waamini wa dini ya Kiislam wanaamini kwamba huruma ya Mungu haina mipaka kwani malango ya huruma ya Mungu yako wazi kwa kila mtu anayetaka kuikimbilia na kuiambata katika maisha yake. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu iwe ni fursa ya kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya waamini wa dini mbali mbali, ili kujenga msingi wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa lengo la kutaka kufahamiana na kuelewana zaidi.
Majadiliano ya kidini yasaidie kufuta kiburi na jeuri; udhalilishaji, ukatili na ubaguzi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani na maridhiano kati ya watu! Katika mahojiano maalum na Jarida la “Vita Nueva” linalochapishwa nchini Hispania, Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anasema, majadiliano ya kidini ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee majadiliano ya kidini yanayolenga kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Waamini wa dini mbali mbali wajitahidi kujenga madaraja ya watu kukutana na kuheshimiana ili kujenga umoja, urafiki na udugu licha ya tofauti zao za kidini, ambazo zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama amana na utajiri mkubwa katika maisha ya watu. Hapa mwaliko ni kushirikiana kwa dhati kabisa ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Lengo ni kudumisha misingi ya amani na utulivu, kikolezo kikuu cha ustawi na maendeleo ya watu.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa ni kiongozi mwenye mvuto kwa waamini wa dini mbali mbali kutokana na ushuhuda wa imani yake inayomwilishwa katika matendo anasema Askofu Ayuso Guixoit. Amekuwa mstari wa mbele kuwapigania wanyonge na maskini pamoja na kuendelea kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti. Majadiliano ya kidini yanapata umuhimu wa pekee kwa nyakati hizi kutokana na ukweli kwamba kuna watu wengi ambao wameathirika kutokana na mipasuko, nyanyaso na dhuluma za kidini kutokana na baadhi ya waamini kuwa na misimamo mikali ya maisha.
Kuna dhuluma, nyanyaso na ubaguzi kwa misingi ya kidini, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kumbe, waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kusimama kidete kulinda, kutetea, kudumisha na kujenga familia ya binadamu inayojikita katika umoja, upendo, msamaha na upatanisho unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya mwanadamu. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, yanawasaidia waamini kushuhudia imani na utambulisho wao, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kutetea mafao ya wengi, udugu na mshikamano ili kujenga dunia iliyo bora zaidi.
Askofu Ayuso Guixot anakaza kusema majadiliano ya kidini yanapania kukuza amani, utulivu na usalama, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, inasaidia kumaliza vita na mipasuko ya kidini, ili kujenga haki na amani sehemu mbali mbali za dunia. Hapa waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuangaliana kwa jicho la huruma na upendo; kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini, lakini kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, ni watoto wa Baba mwenye huruma.
Majadiliano ya kidini si dhana inayoelea katika ombwe, bali ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kila siku; katika maisha ya kijamii kwa kuthamini na kuheshimu taratibu, kanuni na miiko ya waamini wa dini nyingine. Kutambua utu na heshima ya binadamu na haki zake msingi kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Viongozi wa kidini wawe na ujasiri wa kuzuia, kukemea na kulaani vitendo vinavyofanywa na waamini wa dini zao kinyume cha utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu.
Baba Mtakatifu anahimiza majadiliano ya kidini ili kujenga jamii inayowakumbatia na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi kwani ubaguzi ndio chanzo kikuu cha chokochoko, uhasama na mipasuko ya kijamii. Waamini washirikiane na kushikamana dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko mintarafu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani ni mwendelezo wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wengine waliofuatia.
Askofu Ayuso Guixot anasema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao kuhusu majadiliano ya kidini “Nostra Aetate” wanaonesha umuhimu wa majadiliano ya kidini kama mbegu na chemchemi ya amani na utulivu katika ya Jumuiya ya kimataifa. Mwenyeheri Paulo VI alikazia majadiliano ya kidini; Yohane Paulo II akaanzisha utamaduni wa amani kati ya waamini kwa kuitisha mkutano wa Assisi uliofanyika kunako mwaka 1986, miaka thelathini iliyopita. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akalitaka Kanisa kufanya majadiliano ya kidini katika ukweli na upendo kwa kuheshimu tofauti ili kujenga umoja na udugu wa kweli!
Comments
Post a Comment