MSEMAJI MKUU VATICAN ANG'ATUKA


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Padre Federico Lombardi, SJ., la kutaka kung’atuka kutoka madarakani kama msemaji mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu amemteua Dr. Greg Burke, kuwa msemaji mkuu wa Vatican. Kabla ya uteuzi huu, Dr. Burke alikuwa ni msemaji msaidizi wa Vatican. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Dr. Poloma Garcìa Ovejero kuwa msemaji msaidizi wa Vatican. Uteuzi wa viongozi hawa wawili unaanza hapo tarehe 1 Agosti 2016.
Itakumbukwa kwamba, Dr. Gregory Joseph Burke alizaliwa tarehe 8 Novemba 1959 huko St. Louis, Marekani. Akasoma katika shule za Wayesuiti na kuhitimu masomo yake kunako mwaka 1983 katika Fasihi kutoka Chuo Kikuu cha Colombia, New York, Marekani, baadaye akajiendeleza katika tasnia ya Uandishi wa habari, huku akijiunga na Shirika la Kazi ya Mungu, “Opus Dei”.
Kwa miaka mingi alikuwa ni mwandishi wa habari wa “United Press International” huko Chicago, “Reuters” na Jarida la “Metropolitan” hadi pale alipotumwa mjini Roma kama mwandishi wa Jarida la “National Catholic Register”. Kunako miaka 1990 alianza kushiriki katika kuandika makala kwenye Jarida la “Time” na mwakilishi wa Time kiasi cha kufanikiwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1994 kutangazwa na Jarida hili kuwa ni Mtu maarufu sana kwa mwaka huo.
Kuanzia mwaka 2001 alianza kuandika habari kama mwakilishi wa Kituo cha Televishen cha Fox News kutoka Roma. Na kunako mwaka 2012 akateuliwa kufanya kazi katika Sekretarieti kuu ya Vatican kama mtaalam mshauri wa masuala ya mawasiliano ya jamii. Kuanzia tarehe 21 Desemba 2015 akateuliwa kuwa ni Msemaji msaidizi wa Vatican.
Wasifu wa Dr. Paloma Garcìa Ovejero unaonesha kwamba, alizaliwa tarehe 12 Agosti 1975 huko Madrid, Hispania. Kunako mwaka 1998 akajipatia shahada ya uzamili katika tasnia ya habari kutoka Chuo kikuu cha Complutense, Madrid, Hispania. Kajiendeleza zaidi katika taaluma ya mikakati ya mawasiliano kwenye Chuo kikuu cha New York Marekani. Kuanzia mwaka 1998 alikuwa ni mwandishi wa habari katika kituo cha “Cadena Cope, Radio Espanòla kama Mhariri mkuu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU