MTAKATIFU MARIA GORETTI SHUHUDA WA HURUMA NA MSAMAHA WA KWELI

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha ibada kwa Mtakatifu Maria Goretti, Shahidi ambaye alipokuwa kufani alimsamehe mtesi wake. Ibada hii kwa majimbo mengi nchini Italia ilianza kwa bidii zaidi kunako mwaka 1995 na maadhimisho ya Mwaka huu ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayowataka waamini kujikita katika toba, wongofu wa ndani na msamaha ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya binadamu.
Baba Mtakatifu katika ujumbe aliowaandikia Askofu Mariano Crociata wa Jimbo Katoliki Latina - Terracina-Sezze - Priverno na Askofu Marcelo Semeraro wa Jimbo Katoliki Albano,Italia anawatakia heri na baraka katika kukuza na kudumisha Ibada kwa Mtakatifu Maria Goretti, ambaye Kanisa linafanya kumbu kumbu yake kila mwaka ifakapo tarehe 6 Julai.
Tarehe 2 Julai 2016 waamini watafanya maandamano ya hija ya maisha ya kiroho kutoka katika Madhabahu ya Bikira Maria Mama Yetu wa Neema huko Nettuno hadi kwenye madhabahu ya nyumba ambamo Mtakatifu Maria Goretti aliuwawa kikatiliki huko Le Ferriere. Lengo ni kufuata nyayo za maisha ya Mtakatifu Maria Goretti, Shahidi kwa kuongozwa na tema ya “huruma kama Baba” inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anakumbusha kwamba umaskini ni kati ya mambo yaliyoifanya familia ya Mtakatifu Maria Goretti kuhama ili kutafuta maisha bora zaidi, akakumbana na ugonjwa wa Malaria na umaskini, mambo ambayo hata leo hii bado yanaendeea kuwaandama watu wengi. Mama Assunta alijitahidi kuhakikisha kwamba, familia yake inapata mahitaji msingi kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, Mtakatifu Maria Goretti aliwalea na kuwatunza wadogo zake pamoja na kuangalia nyumba yao.
Mtakatifu Maria Goretti alijiandaa vyema kupokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha yake. Kutokana na umbali uliokuwepo kutoka nyumbani hadi Kanisa, Maria Goretti alilazimika kukomunika mara chache kwa juma, lakini nyakati zote alizopata nafasi ya kukomunika, alijiandaa kikamilifu kama njia pekee ya kuonesha upendo wake wa dhati kwa Yesu wa Ekaristi. Papa Pio XII kunako mwaka 1950 wakati alipokuwa anamtangaza kuwa Mtakatifu alisema, Ubikira wa Maria Goretti ulifunikwa kwa damu ya mashuhuda wa imani.
Baba Mtakatifu anasema, anashangazwa sana na ujasiri wa imani uliooneshwa na Mtakatifu Maria Goretti wakati alipokuwa kufani, alimsamehe mtesi wake na kumwombea maisha ya uzima wa milele. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu anasema, kusamehe makosa ni ushuhuda dhahiri wa upendo wenye huruma na kwa Wakristo ni wajibu ambao hawawezi kuukwepa, ingawa wakati mwingine si rahisi kusamehe. Na bado msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono ya waamini ambao wanaelemewa na udhaifu, ili kuwajalia moyo mkunjufu. Ni huruma na msamaha vilivyomsindikiza Mtakatifu Maria Goretti kwa amani na utulivu wa ndani wakati wa kifo chake na huo ukawa ni mwanzo wa toba na wongofu wa ndani kwa watesi wake na hatimaye, akajiachilia mikononi mwa upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu, anawaalika waamini pamoja na wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa: toba, wongofu wa ndani, huruma na msamaha, ili kweli waamini hawa waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao. Huu ni muda muafaka kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia furaha ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.
Ni wakati wa Mama Kanisa kuchuchumilia mambo msingi katika maisha ya kiroho, kwa kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Msamaha ni fadhila inayofumbata maisha mapya na kutia ujasiri wa kuangalia wakati ujao kwa matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo mambo msingi ambayo anawatakia waamini hawa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu katika majimbo yao, wanapoadhimisha kwa namna ya pekee, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Maria Goretti, Bikira na Shahidi, mfano bora wa kuigwa katika umwilishaji wa huruma wakati wa mateso na kifo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI