Ask.Mapunda: Mkiongozwa na Roho Mtakatifu hamtaishi kwa mazoea
ASKOFU Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida
amewaasa waamini kumpokea Roho Mtakatifu kwa furaha na shukrani, huku
wakikubali maisha yao kuongozwa na Roho Mtakatifu, ambaye anafanya mabadiliko
katika utume na maisha.
Ameeleza
hayo hivi karibuni, alipofanya ziara ya kichungaji katika Parokia ya Kristo
Mfalme ya Kibaoni iliyopo Singida, ambapo pia amewapa Sakramenti ya Kipaimara
waamini 229 wengi wakiwa ni watoto na vijana.
Askofu
Mapunda ameeleza kuwa Kipaimara hukamilisha sakramenti za kumwingiza muumini
katika ukristo, hivyo wanaopokea sakramenti hiyo kwao ni neema na furaha; kwa
kuwa Roho Mtakatifu yule yule aliyewashukia mitume, ndiye wanayempokea hata hii
leo.
Aidha
Askofu Mapunda amewaasa waamini kuwa wapya katika maisha ya huruma,
kusameheana, utakatifu na hivyo kutafuta kwanza ufalme wa mbingu.
“Tupambane
na makandokando ya maisha, hatuna sababu ya kuogopa majaribu, vishawishi na
mateso. Mungu ndiye anayetia nguvu kwenye udhaifu hadi uongofu kwenye dhambi”,
amesema Askofu Mapunda.
Parokia ya
Kibaoni imefikisha mwaka moja tangu izinduliwe mwaka 2015 na Askofu Mapunda
ambaye pia amefikisha mwaka moja tangu kusimikwa kuwa Mchungaji Mkuu wa jimbo
hilo.
Awali
parokia hiyo ilikuwa ni kigango cha Parokia ya Kanisa Kuu ya Moyo Mtakatifu wa
Yesu, Singida. Ndani ya kipindi cha mwaka moja zimezinduliwa parokia mbili mpya
katika mji wa Singida nyingine ikiwa ni Parokia ya Mtakatifu Yosef Mfanyakazi
iliyoko Mandewa, na hivyo kuwa na parokia 3 hadi sasa mjini.
Parokia ya
Kibaoni ina waamini 3,150, vigango 14, jumuiya ndogondogo 51 vyama vya kitume
11 na makatekista 18. Mapadri wanaohudumu katika parokia hii ni Paroko Patrick
Nkoko, na wasaidizi wa Paroko Padri
Patrick Njiku na Padri Pasian Mwanga.
Katika
kipindi cha mwaka moja kuna wakatekumeni 78, waliopata sakramenti ya ubatizo ni
472, ndoa 33, mpako wa wagonjwa 10, waliopokelewa ukatoliki 62, waliorudi kwa
msamaha 14 na waliofariki ni 13. Aidha parokia ina waseminari 2 katika seminari
ya Mtakatifu Wiliam Diagwa, 5 katika seminari ya Mtakatifu Patrisi Dung’unyi.
Taasisi za
kijimbo zilizopo ndani ya mipaka ya parokia ni pamoja na sekondari ya Mpinda
(wavulana), chuo cha ualimu cha Mtakatifu Bernard na sekondari ya Mtakatifu
Karoli Boromeo (mchanganyiko). Parokia inatekeleza miradi mbalimbali ikiwamo
ukamilishaji ujenzi wa Kanisa la Parokia, ujenzi wa nyumba ya mapadri, ujenzi
wa makanisa vigangoni, ununuzi wa gari kwa ajili ya huduma za kichungaji na
ufundishaji dini.
Comments
Post a Comment