Ask. Ruzoka: Vijana ni mashahidi wa imani
ASKOFU Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki
Tabora amewaasa waamini wa Parokia ya Kipalapala kuishi maisha ya Upendo na
moyo wa ustahimilivu katika familia zao.
Ametoa rai
hiyo hivi karibuni alipoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Sakramenti ya
Kipaimara kwa watoto 112 parokiani hapo
Akitoa
mahubiri katika Misa hiyo Askofu Ruzoka amewaomba watoto na vijana waliopewa
Sakramenti hiyo kuishi maisha ya kusameheana, kwani katika maisha ya pamoja
kuna uwezekano mkubwa wa kutofautiana, hivyo inapotokea kukoseana na chuki
jambo la msingi ni kusameheana na kuanza maisha upya.
Akifananisha
dhambi ya wana wa Israeli na kosa alilofanya Mfalme Daudi, Askofu Ruzoka
amesema kuwa hao walitenda dhambi lakini hawakukata tamaa, bali walitubu. Amewaasa waamini kukimbilia huruma
ya Mungu pale wanapotambua kuwa wametenda dhambi.
“Hata kama
tukitenda dhambi sisi siyo wa kwanza wala wa mwisho. Sisi ni viumbe dhaifu,
hivyo kutenda dhambi kupo, cha msingi ni kuchukua hatua baada ya kutenda
dhambi. Tusipende kutulia katika maisha
ya dhambi” ameeleza Askofu Ruzoka.
Aidha
Askofu Ruzoka amewaonya watoto na vijana hao kujiepusha na dhambi ya ubaguzi,
na kuwa hawapaswi kuwatofautisha binadamu wenzao kwa misingi ya chimbuko lao
kwani hakuna myahudi wala myunani, bali wote ni wa Mungu.
Askofu
Ruzoka pia amewataka watoto hao waende kuwa mashahidi wa Imani, wajiepushe na
chuki, masengenyo, waende wakamshuhudie Kristo katika mazingira yao.
Pia
amewaasa watoto na vijana hao kufanyia kazi ndoto zao, wasiishi kwa mapigo ya
moyo bali waishi kwa malengo katika maisha yao.
Ibada hiyo
pia imehudhuriwa na Paroko wa Kipalapala Padri Thomas Mambo, Gombera wa
Seminari Kuu Kipalapala Padri Herman Kachema, Kaimu Gombera Padri Philipo
Ntulama, na Padri Andrea Mlele, mlezi wa vijana nyumba ya malezi
Kipalapala.
Comments
Post a Comment