KUELEKEA SIKU YA 31 YA VIJANA DUNIANI
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kumi na tano ya kitume nchini Poland kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “heri wenye rehema maana hao watapata rehema” kuanzia tarehe 26 – 31 Julai 2016 atapata nafasi ya kuzungumza na vijana, waamini na viongozi wa Serikali ya Poland. Huruma ni dhana inayofumbata: faraja, msamaha pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine; mambo ambayo yamefafanuliwa vyema kwenye Sala ya Vijana wakati wa maadhimisho haya.
Hii ni nchi ya 23 kutembelewa na Papa Francisko, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye alibahatika kutembelea Poland mara tisa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Mwaka 2006, miaka kumi iliyopita akatembelea Poland, ili kufuata nyayo za Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka mjini Roma, Jumatano tarehe 26 Julai 2016 na kurejea tena mjini Vatican hapo tarehe 31 Julai 2016. Atakapowasili, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, siasa na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Poland.
Huu ni ufafanuzi ambazo umetolewa na Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 20 Julai 2016 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland. Akiwa kwenye Makao makuu ya Jimbo kuu la Cracovia, Baba Mtakatifu kila siku jioni atakuwa anawasalimia vijana wanaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kama alivyozoea kufanya Mtakatifu Yohane Paulo II.
Alhamisi, tarehe 28 Julai 2016 Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Jimbo kuu la Czestochowa kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Tarehe 29 Julai 2016 Baba Mtakatifu atatembelea na kuwasalimia watoto wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Cracovia na baadaye atakwenda kwenye kambi za mateso huko Auschwitz na Birkenau, ambako anasema anataka kukaa peke yake ili kupata nafasi ya kulia na kusikitika kutokana na ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Hii itakuwa ni siku rasmi ya kuwakaribisha vijana nchini Poland.
Hii itakuwa ni kumbu kumbu pia ya miaka 75 tangu Mtakatifu Marximilliano Maria Kolbe alipohukumiwa kifo, shuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana pia na wahanga waliosalimika mateso ya Kinazi. Baba Mtakatifu atasikiliza kwa makini Zaburi ya 130: Toka vilindini nimekulilia Bwana! Kwa lugha ya Kilatini Zaburi hii inajulikana kama “De profundis”. Zaburi hii itaimbwa na Rabbi wa Kiyahudi na kutafsiriwa na Padre Mkatoliki anayewakilisha familia za Kikristo zilizosaidia kutoa hifadhi kwa Wayahudi wakati wa mateso na madhulumu ya Vita kuu ya Pili ya Dunia.
Ijumaa tarehe 29 Julai 2016 itakuwa ni siku ya kuadhimisha Njia ya Msalaba ambayo itawasaidia vijana kutafakari kuhusu matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Sakramenti ya Upatanisho inayowawezesha waamini kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; atashiriki chakula cha mchana na wawakilishi kumi na wawili wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea huko Lagiewniki, eneo ambalo lina kumbu kumbu za kihistoria za maisha ya Mtakatifu Faustina Kowalska, mtume hodari wa Ibada ya Huruma ya Mungu pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuonesha uhusiano wa karibu kati ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016. Hiki ndicho kiini cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Poland.
Zaidi ya vijana millioni moja na nusu wanatarajiwa kuhudhuria katika maadhimisho haya huko Cracovia na tayari kuna umati mkubwa wa vijana ambao uko njiani kuelekea nchini Poland, huku wakiwa wanasindikizwa na Wakleri kutoka katika nchi zao. Baba Mtakatifu atawasili kwenye Uwanja mkubwa wa Blomia, Mjini Cracovia huku akiwa ameandamana na vijana walemavu watakaokuwa kwenye Treni ya umeme changamoto ya kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote.
Baba Mtakatifu atabariki nyumba mbili kwa ajili ya maskini na wazee nchini Poland, kumbu kumbu endelevu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Nyumba zote hizi ziko takribani kilometa 12 kutoka katika eneo la Uwanja wa Huruma ya Mungu nchini Poland. Lugha itakayotumika wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakuwa ni Kipolandi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment