MAUAJI YA KUSIKITISHA:PAPA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI
Mapema,Baba Mtakatifu Francisko, alipewa taarifa nyingine ya kusikitisha juu ya mauaji ya kikatili kwa Padre na waamini kadhaa kutekwa nyara wakati wakihudhuria Ibada ya Misa mapema Jumanne hii Julai 26 , 2016, Kaskazini mwa Ufaransa . Na pia alipokea habari za kusikitisha za mauaji yaliyotokea katika kituo cha walemavu cha Ujapani.
Papa Francisko baada ya kupewa taarifa ya mauaji Padre Jacques Hamel mwenye umri wa miaka 84 na utekaji nyara uliofanyika katika kanisa la Mtakatifu Etienne-du-Rouvray la Rouen Ufaransa , mara alipeleka salaam zake za rambirambi kwa Askofu Mkuu Dominique Lebrun wa Jimbo Kuu la Rouen, ambamo ameonyesha masikitiko yake, na kwamba anawaweka wote pamoja na wahalifu mbele ya hukumu ya Mungu.
Msemaji wa Vatican, Padre Federico Lombardi, amesema pamoja na maumivu na hofu zinazotokana na "vurugu hivi za kusikitisha, Papa Francisko katika salaam zake za rambirambi, hajaonyesha chuki kwa waliohusika na unyama huo, lakini amesema anawakumbyuka wote katika maombi yake, hata wauaji .
Padre Federico Lombardi ameyaita mauaji haya kuwa ni vurugu za kijinga zisizokuwa na manufaa kwa yeyote ila ni ufedhuli wenye kuongeza tu uhalifu kwa maisha ya binadamu ,na kuleta hofu kwa watu bure. Na inasikitisha zaidi kwamba, vurugu hizi zinafanywa hata katika maeneo matakatifu ya Ibada , mahali ambako upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka unahubiriwa kwa watu wote. Haya ni mauaji ya kikatili.
Polisi wa Ufaransa wakithibitisha tukio hili, wametaja watu wawili waliokuwa na silaha na visu, waliingia kanisani wakati wa Misa, na walimshambulia Padre Hamel kwa kumkata kooni. Kwa bahati mmoja wa wamini aliweza kuwatoroka washambuliaji hao na kuitaarifu Polisi ambao mara walichukua hatua haraka za kuwadhibiti wahalifu na katika purukushani hiyo, washambuliaji hayo wote wawili waliuawa. Na muumini mwingine aliyekuwa katika Ibada hiyo hali yake ni mbaya amelazwa hospitalini.
Wakati tukio hili linatokea, Askofu Mkuu Dominique Lebrun wa Jimbo Kuu la Rouen, tayari alikuwa Krakow, Poland, ambako ameandamana na Mahujaji vijana kutoka jimbo kuu lake, kwa ajili ya kuhudhuria adhimisho la Siku ya Vijana Duniani.
Katika mahojiano amesema angependa kurudi nyumbani kwa ajili ya msiba huu.Na kwamba, Kanisa Katoliki, halina silaha nyingine zaidi ya sala na mshikamano wa udugu miongoni mwa watu wenye mapenzi mema. Na kwamba, yeye akiweza kurudi nyumbani tokea Krakow Poland, mamia ya vijana kutoka Jimbo lake wataendelea kubaki huko. Na kwamba yeye anapenda kurudi nyumba si kwa sababu ya hofu za ghasia lakini kama jambo la ustaraabu wa upendo, kushikamana kwa karibu zaidi na watu walioumiza kiroho.
Aidha Jumanne hii, Baba Mtakatifu Francisko amepeleka ujumbe wa rambirambi, uliotiwa sahihi na Katibu wa Vatican, Kardinali Parolin, kufuatia mauaji yaliyofanyika katika kituo cha Walemavu cha Tsukui Yamayurien Japan.
Rambirambi za Papa zimetumwa kwa Askofu Mkuu Peter Takeo Okada wa Jimbo Kuu la Tokyo. Papa ameonyesha masikitiko yake kwa maisha ya watu kupotezwa katika kituo hiki, kwa ajili ya walemavu, na ameonyesha ukaribu wake na wote walioathirika na janga, kwa ndugu wa marehemu na waliojeruhiwa. Ameomba msaada wa Bwana kwa ajili ya uponyaji wa kiroho na faraja , katika wakati huu mgumu. Na pia analiombea taifa la Japan baraka za Mungu, maridhiano na amani.
Comments
Post a Comment