Askofu mkuu Celli: nguli katika huduma na mawasiliano!
Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican, Alhamisi, tarehe 21 Julai 2016 amemshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Claudio Maria Celli, aliyeng’atuka kutoka madarakani kutokana na huduma yake kwa Kanisa kama Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano lililovunjwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko na kuundwa kwa Sekretarieti ya Mawasiliano inayoratibu na kusimamia vyombo vyote vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa sasa.
Tukio hili limehudhuriwa pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ambaye pia amemshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Celli kwa huduma makini aliyoitoa katika masuala ya kidplomasia katika nchi mbali mbali duniani, utume katika Sekretarieti kuu ya Vatican kama Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican kunako mwaka 1990. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, ataendelea kujifunza kutoka kwa Askofu mkuu Celli mambo muhimu katika kukuza na kudumisha majadiliano na China.
Monsinyo Viganò anamtambua Askofu mkuu Celli tangu alipotumwa na Jimbo kuu la Milano kuja Roma ili kusomea masuala ya mawasiliano ya jamii kwenye miaka 1991 alionesha mvuto mkubwa na kupendwa na wanafunzi wengi kutokana na uwezo wake mkubwa kwa masuala mbali mbali. Anamshukuru kwa kusaidia mchakato wa uundaji wa Sekretarieti ya Mawasiliano kunako Juni, 2015.
Majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi yamesaidia kurahisisha mchakato wa mageuzi unaopania kuunganisha Radio Vatican, Kituo cha Televisheni cha Vatican na Gazeti la L’Osservatore Romano kuwa chini ya Sekretarieti ya mawasiliano. Wakati wa uongozi wake, Askofu mkuu Celli ameiwezesha Vatican kuweza kutoa huduma makini katika mitandao ya kijamii kwa kusoma alama za nyakati, tayari kuinjilisha kwa kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari.
Kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akaandika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii hapo tarehe 12 Desemba 2012. Kulikuwa na changamoto kubwa katika matumizi ya mitandao hii ya kijamii, lakini Askofu mkuu Celli hakukatishwa tamaa na leo hii ni chombo makini sana kinachomwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kukutana na watumiaji wa mitandao hii!
Kwa upande wake, Askofu mkuu Claudio Maria Celli anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kufikia katika umri wa kung’atuka kutoka madarakani, anamwomba aendelee kumsimamia katika uzee wake anapomshukuru kwa kumkirimia miaka 75 tangu alipozaliwa. Itakumbukwa kwamba, alizaliwa Jimboni Rimini, Italia kunako tarehe 20 Julai 1941. Akapadrishwa tarehe 19 Machi 1965. Akajiendeleza katika masomo ya Falsafa, Taalimungu na Sheria za Kanisa na huko kote akajipatia Shahada ya uzamili na uzamivu na kubahatika kufundisha katika Taasisi ya Kidiplomasia ya Kanisa pamoja na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano.
Tarehe 16 Desemba 1995 akateuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu sanjari na kuteuliwa kuwa ni Mkurugenzi na msimamizi mkuu wa mali ya Kanisa (Apsa). Tarehe 27 Juni 2007 akateuliwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Tareje 28 Aprili 2009 akateuliwa kuwa ni Rais wa Baraza la Utawala la Kituo cha Televisheni cha Vatican. Tukio la kumshukuru na kumpongeza Askofu mkuu Claudio Maria Celli limehudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka katika Sekretarieti ya Mawasiliano pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Vatican.
Comments
Post a Comment