HURUMA YA MUNGU NI NINI?


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” anatumia picha ya Yesu Kristo kukutana na mwanamke Msamaria kama msingi wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, huruma ambayo inagusa na kuleta mabadiliko katika maisha ya mtu. Katika shida, changamoto na magumu ya maisha ya ndoa na familia, Mama Kanisa anapaswa kukabiliana na mambo yote haya akiwa na mwelekeo chanya katika maisha na utume wa familia.
Lengo ni kuzijengea familia uwezo wa kusimama kidete, kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia yenye mvuto na mashiko kwa jirani. Ushuhuda wa Yesu kwa mwanamke Msamaria pale kisimani, uleta mageuzi makubwa kwa maisha ya mwanamke yule Msamaria. Kanisa halina budi kuwahudumia wanafamilia wanaoishi katika utakatifu bila kuwasahau wale wanaoogelea katika dimbwi la myumbo wa tunu bora za maisha ya ndoa na familia. Lakini kwa bahati mbaya watu wanachechemea katika maisha ya ndoa na familia wanaangaliwa kwa jicho la kengeza na hata wakati mwingine kunyooshewa kidole.
Baba Mtakatifu Francisko katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo analitaka Kanisa kutoka kifua  mbele kuwahudumia watoto wake wote pasi na ubaguzi kwa kujikita katika huduma ya upendo shirikishi. Kanisa linapaswa kutambua kwamba liko sawa na hospitali katika uwanja wa vita, linapaswa kuganga na kuponya majeraha ya wanandoa kwa kujikita katika sanaa ya kuwasindikiza wanandoa hawa kugundua mapenzi ya Mungu katika maisha yao, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, aliye asili ya wema, huruma, msamaha na upendo. Kwa njia hii, wanandoa wataweza kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu wakati wa kuadhimisha mkesha wa Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Jimbo Katoliki la Mesina, Kusini mwa Italia. Anasema, kila mwaka, Mama Kanisa ifikapo tarehe 16 Julai, anaadhimisha kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli.
Hii ni siku maalum ya kuomba neema ya upatanisho, msamaha na huruma ya Mungu katika maisha. Kwa namna ya pekee wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, linamwomba Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini  kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, inayowawezesha waamini kupata utakatifu wa maisha. Maisha ya Kikristo hayana budi kusimikwa katika tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma.
Kardinali Baldisseri anakaza kusema,  Waraka wa kitume Furaha ya Injili, Evangelii gaudium ni dira na mwelekeo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linakuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha yao kwa kuwa na ari na mwelekeo mpana zaidi wa kimissionari na shughuli za kichungaji; dhamana ambayo Jumuiya ya Kikristo inapaswa kushiriki kikamilifu. Tasaufi ya maisha ya Kikristo haina budi kurutubishwa na Neno la Mungu, mahali ambapo waamini wanapata fursa ya kukutana na kuzungumza na Mungu kutoka katika undani wa maisha yao bila kusahau kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini nguvu ya maisha ya kiroho tayari kuambata utakatifu wa maisha.
Waamini wajenge utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu katika maisha yao ili kujenga na kudumisha umoja na udugu ndani ya Kanisa kama ushuhuda wa upendo kwa watu wa mataifa. Waamini wajifunze kumwabudu Mungu katika roho na ukweli; katika umoja na upendo; katika mshikamano na huduma makini kwa watu wenye shida na mhangaiko mbali mbali. Yesu alitambua na kuheshimu utakatifu wa Hekalu la Yerusalemu, lakini akawahimiza wafuasi wake kumtafuta na kumhudumia Mungu kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa maneno mengine, waamini wanaalikwa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha anasema Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI