UFUNGUZI SIKU YA 31 YA VIJANA DUNIANI
Baada ya maandalizi ya kiroho kwa muda wa miaka mitatu, hatimaye, maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, huko Cracovia, Poland yanayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema” yamezinduliwa rasmi na Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia nchini Poland kwa Ibada ya Misa Takatìfu. Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wako Poland kuzungumza lugha ya Injili, inayofumbatwa katika upendo, udugu, mshikamano na amani. Wako Jimbo kuu la Cracovia mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, Muasisi wa Siku ya Vijana Duniani, ili kufuata nyayo zake katika kutangaza na kushuhudia Injili na zawadi ya huruma ya Mungu. Hiki ni kipindi cha Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.
Katika mahubiri yake, Kardinali Stanislaw Dziwisz amekazia kwa namna ya pekee: majadiliano na Kristo Yesu; Mahali wanapotoka; mahali walipo kwa sasa na kwamba, ni mambo yepi wanayotarajia baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yanayokwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Majadiliano kati ya Yesu na Mtakatifu Petro, yanaonesha jinsi alivyoacha yote na kuamua kumfuasa Kristo. Akashuhudia Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni kwa Baba, alimuuliza Petro ikiwa kama alikuwa anampenda kuliko mitume wengine wote!
Mtume Petro alionja upendo wa kina kutoka kwa Kristo Yesu, akaimarishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, akawa ni chombo madhubuti na shuhuda mahiri wa Fumbo la Pasaka, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Damu ya mashuhuda wa imani kama akina Petro Mtume, imekuwa daima ni mbegu ya Ukristo na ukuaji wa Kanisa, mang’amuzi ambayo vijana wanayafanyia kazi kwa wakati huu wanapoadhimisha Siku ya Vijana Duniani.
Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wako Poland, kama ilivyokuwa takribani miaka elfu mbili iliyopita, wakati Roho Mtakatifu alipowashukia Wakristo wa Kanisa la mwanzo, wakatangaza imani yao kwa Kristo Mfufuka kwa njia ya utakatifu wa maisha. Leo hii vijana hawa wanatoka katika maeneo ambamo amani, upendo na mshikamano vinatawala na kudumishwa, lakini kuna baadhi yao wanatoka pia katika maeneo ya vita, baa la njaa na umaskini; wanatoka katika nchi ambamo kuna nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo; vitendo vya kigaidi vinaendelea kushamiri siku kwa siku na baadhi ya Serikali kupandikiza sera ambazo ni kinyume cha haki msingi za binadamu.
Kardinali Stanislaw anasema, vijana wamebeba ndani mwao mang’amuzi binafsi ya Kiinjili, wasi wasi na mashaka; matumaini na matarajio ya kuona dunia ikiwa imekijita zaidi katika utu, udugu na mshikamano na kwamba, yote haya yanawezekana kwa yule awatiaye nguvu! Vijana wanaweza kupambana na changamoto za maisha kwa kujikita katika imani na tunu msingi za Kiinjili; kwa kutambua mema na mabaya katika maisha yao; upendo na chuki. Vijana wako Jimbo kuu la Cracovia, chemchemi ya Ukristo, yapata miaka 1050 iliyopita.
Historia ya familia ya Mungu nchini Poland inaonesha ugumu, lakini waamini wamejitahidi kwa miaka yote hii kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu na Injili ya Kristo! Vijana wamekutana ili kumzunguka Kristo Yesu, Mwanga wa ulimwengu ili kamwe wasitembee katika giza na uvuli wa mauti. Kristo ni ukweli, njia na uzima na anayo maneno ya uzima wa milele.
Kristo Yesu anawasindikiza vijana katika hija ya maisha yao kama alivyofanya kwa wanafunzi wa Emmau, changamoto ni kujiaminisha kwake, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo, kwa kutambua kwamba, wote wamekombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu. Mama Kanisa anategemea kwa kiasi kikubwa ushuhuda wa imani na utakatifu wa maisha ya vijana, ambao watakuwa ni vyombo na mashuhufa wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Wakati huu, vijana wanapata nafasi ya kusikiliza kwa makini changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Imani.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni fursa ya kujitajirisha katika maisha ya kiroho, ili utajiri hatimaye, waweze kuwashirikisha vijana wenzao utajiri ambao watakuwa wamejichotea katika maadhimisho haya. Ni wakati wa kusikiliza kwa makini sauti ya Kristo Yesu! Kuangalia changamoto za maisha kwa jicho la imani; kushirikishana imani, matumaini na mapendo na vijana wengine; kwa kusikiliza Katekesi kwa makini kutoka kwa Maaskofu; kwa kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Vijana wanahamasishwa kuthamini utamaduni na ukarimu wa familia ya Mungu kutoka Poland.
Jimbo kuu la Cracovia ni chemchemi ya Ibada ya huruma ya Mungu iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska, changamoto kwa vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; Imani, Matumaini na Mapendo; tayari kushikamana katika ujenzi wa utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano, dhidi ya ubinafsi, chuki na uhasama. Hii ndiyo dhamana ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alitamani kuipandikiza katika nyoyo za vijana wakati alipokuwa anaanzisha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani! Vijana wanahamasishwa kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Comments
Post a Comment