SIKU YA VIJANA DUNIANI:TUKIO LA IMANI NA MATUMAINI KWA VIJANA


Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kujinoa tayari kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Cracovia, Poland inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Hiki ni kipindi cha sala, tafakari na furaha inayomwilishwa katika misingi ya imani, matumaini na mapendo miongoni mwa vijana kumzunguka Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa namna ya pekee kwa mwaka huu katika nchi alimozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa Maadhimisho ya Vijana Duniani pamoja na Mtakatifu Sr. Faustina Kowalska, mtume hodari wa Ibada ya huruma ya Mungu.
Matukio yote haya yanafumbatwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini na katika tukio hili vijana kutubu na kumwongokea Kristo Yesu, tayari kuambata njia ya ukamilifu na utakatifu wa maisha unaoshuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.  Vijana wanakwenda nchini Poland anasema Padre Andrezej Majewski, Mkurugenzi wa Vipindi wa Radio Vatican, kujiandaa kikamilifu ili waweze kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa linawatambua na kuwathamini vijana ambao ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, lakini vijana hawa wanapaswa kuandaliwa vyema ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma na matumaini kwa wale wanaowazunguka.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanafanyika nchini Poland kama Jubilei ya miaka 25 tangu maadhimisho haya yalipofanyika nchini Poland, kukiwa an mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa familia ya Mungu nchini Poland. Vijana wengi kutoka katika nchi za Ulaya ya Mashariki wanajisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu nao wanataka kushiriki kikamilifu katika tuklio hili la imani na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.
Padre Majewski anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II daima alitaka kuwaona vijana wakisimama kidete katika misingi ya maisha bora ya Kikristo, kiutu, kitamaduni na kijamii, dhamana ambayo si lele mama katika ulimwengu mamboleo. Vijana wanayo ndoto ya kutaka kutenda makuu katika maisha yao, lakini wanapaswa kuwa na nidhamu, ari na mwamko mpya katika maisha kwa kujiwekea malengo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ili kutekeleza changamoto hii, vijana wanapaswa kujiachilia katika mpango wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Mzee Ibrahimu, Baba wa imani.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya kujitajirisha zaidi na zaidi katika maisha ya kiroho kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu katika vipaumbele vya maisha yao. Tarehe 27 Julai 2016, Jimbo kuu la Cracovia litaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya heshima ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kuambata Injili ya huruma ya Mungu, dhana ambayo itafanyiwa kazi katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka huu. Vijana watapata nafasi ya kutembelea katika maeneo walimozaliwa mitume wa huruma ya Mungu yaani Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska.
Kumbe, maadhimisho haya yatakuwa ni kilele cha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana. Kwa wale wote watakaokuwa wamejiandaa vyema, wataweza kupata rehema kamili inayotolewa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu. Hapa vijana wanakumbushwa kwamba, Siku ya Vijana Duniani ni tukio la imani na wala si wakati wa kuvinjari tu!
Padre Andrzej Majewski anasema, kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Poland kunako mwaka 1979, Poland ilikuwa bado chini ya utawala wa Kikomunisti, hapo familia ya Mungu nchini Poland ikapata ujasiri wa kujiamini na kuanza kujitengenezea mustakabali wake kwa siku za usoni. Kunako mwaka 1983 Yohane Paulo II alipotembelea Poland, wananchi wakawa na matumaini na matokeo yake ni kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti. Mwaka 1991 Yohane Paulo II alipotembelea Poland aliitaka familia ya Mungu nchini humo kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru kwani ulikuwa na gharama zake. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipotembelea Poland aliwataka wakleri kuwa karibu zaidi na waamini kwa kuwaonesha dira na mwongozo wa maisha.
Padre Andrzej Majewski anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Poland wakati huu ambako kuna mipasuko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kanisa linaendelea kusimama kidete ili kuganga na kuponya mipasuko hii, tayari kuambata dhamana ya Ukristo kwa kushiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo. Itakumbukwa kwamba, Papa Francisko anatembelea Poland kama kilele cha maadhimisho ya Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Kunako mwaka 1966 wakati ambapo Kanisa nchini Poland lilikuwa inaadhimisha Jubilei ya miaka 1000 ya Ukkristo, Utawala wa Kikomunisti hakumruhusu Mwenyeheri Paulo VI kutembelea nchini Poland ili kushiriki maadhimisho hayo.
Khalifa wa Mtakatifu Petro anatembelea Poland ili kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050, yaani miaka 50 tangu utawala wa Kikomunisti, ulipoweka Pazia la chuma dhidi ya Mwenyeheri Paulo VI. Baba Mtakatifu Francisko atapata fursa ya kutembelea kambi za mateso ili kupata nafasi ya kuweza kulia peke yake kutokana na uchungu na ukatili dhidi ya ukuu wa Mungu, utu na heshima ya binadamu. Radio Vatican anasema Padre Andrzej Majewski itakuwa bega kwa bega na wasikilizaji pamoja na wasomaji wa tovuti yake kwa lugha mbali mbali, ili kuwajulisha yale yanayojiri katika maadhimisho haya ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko nchini Poland.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI