JUBILEI YA MIAKA 50 YA SECAM KUADHIMISHWA KAMPALA,UGANDA 2019


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, Jumapili tarehe 24 Julai 2017  limehitimisha mkutano wake wa 17 huko Luanda, Angola kwa Ibada ya Misa Takatifu. Mkutano wa 18 utaadhimisha Jimbo kuu la Kampala, Uganda, kunako mwaka 2019, SECAM itakapokuwa inaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Askofu mkuu Gabrieli Mbilingi amechaguliwa tena kuwa Rais wa SECAM kwa awamu ya pili mfululizo. Makamu wa Rais ni Askofu Anton Sithembele Sipuka kutoka Jimbo Katoliki la Umtata, Afrika ya Kusini. Askofu mkuu Charles G. Palmer-Bucker amechaguliwa kuendelea kuwa ni mweka hazina wa SECAM wakati Askofu Emmanuel Badejo ataendelea kuwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya SECAM, ijulikanayo kama CEPACS.
Wajumbe wengine wa Kamati ya kudumu ya SECAM ni pamoja na Askofu mkuu Samuel Kleda kutoka Jimbo kuu la Douala, Cameroon anayewakilisha Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, ACERAC pamoja na Askofu mkuu Thomas Msusa wa Jimbo kuu la Blantyre, Malawi anayewakilisha Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Mashariki na Kati, AMECEA.
Itakumbukwa kwamba, mkutano wa 17 wa SECAM huko Luanda, Angola ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu ”Familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya Mwanga wa Injili” Mada hii ililenga kwa namna ya pekee, kuibua mbinu mkakati wa utume wa familia Barani Afrika kwa kuzingatia Wosia wa kitume uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ”Furaha ya upendo ndani ya familia” ”Amoris laetitia”.
Wajumbe wamejadili pamoja na mambo mengine changamoto zinazoendelea kuzikabili familia Barani Afrika pamoja na kutafuta mbinu mkakati wa kuinjilisha familia ili kweli familia ziweze kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.  Kardinali Philippe Ouedraogo amekazia umuhimu wa kuimarisha SECAM ili iweze kuihudumia familia ya Mungu Barani Afrika kwa umakini mkubwa zaidi.
Wajumbe wa SECAM wameangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa mawasiliano na utandawazi katika maisha na utume wa familia Barani Afrika. Majadiliano ya kidini na kiekumene; demokrasia, utawala bora na wa sheria; hali ya kisiasa na kiuchumi Barani Afrika; ukosefu wa amani na usalama huko Sudan ya Kusini na Burundi. Wajumbe pia wamepata nafasi ya kusikiliza taarifa kutoka katika Tume na vitengo mbali mbali vya SECAM.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI