Dumisheni utamaduni wa ukarimu na huduma kwa wagonjwa!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 29 Julai 2016 akiwa nchini Poland kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani ametembelea na kuwasalimia watoto waliolazwa kwenye Hospitali ya Watoto ya Prokocim, Jimbo kuu la Cracovia, kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa watoto wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia. Akiungana na wote waliofuatana naye, anapenda kuwasikiliza watoto katika shida na mahangaiko yao katika hali ya ukimya, hata kama hana majibu ya mkato! Jambo la msingi ni kusali pamoja nao!
Maandiko Matakatifu yanaonesha kwamba, Yesu katika maisha na utume wake alikutana, aliwapokea na kuwakaribisha wagonjwa na wakati mwingine aliwafuata huko walikokuwa ili kukutana nao, kuwaonesha na hatimaye, kuwaonjesha huruma na upendo wake kama mama mzazi afanyavyo kwa mtoto wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ukaribu, huruma na upendo kwa wagonjwa; kwa njia ya ukimya na sala ili kujenga na kudumisha utamaduni wa ukarimu, kwani waathirika wakubwa wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine ni wagonjwa, hali inayoonesha ukatili mkubwa.
Baba Mtakatifu anawashukuru wafanyakazi wa Hospitali hii ya watoto wanaowapokea na kuwahudumia watoto wagonjwa, alama ya upendo na ustaarabu wa kibinadamu na Kikristo: changamoto na mwaliko wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa sera za kijamii na kisiasa kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa. Inasikitisha kuona kwamba, wakati mwingine, familia zinalazimika kubeba mzigo wote wa huduma kwa wagonjwa.
Hapa Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa ukarimu na matendo yanayobubujika kutoka katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, upendo wa Kristo Mfufuka na Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Huduma kwa wagonjwa inapaswa kufumbatwa katika huruma na mapendo, ili kukua na kukomaa katika utu na kuwafungulia njia ya maisha ya uzima wa milele. Mwamini anayemwilisha matendo ya huruma katika maisha yake, hana sababu ya kuogopa kifo!
Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wale wote ambao wamechagua huduma kwa wagonjwa kuwa ni sehemu ya utume na maisha yao na anawaombea ili Mwenyezi Mungu awasaidie kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika hospitali mbali mbali. Awajalie upendo, amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wale wote walioandaa na kuwezesha ziara yake hospitalini hapo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI