HUDUMA ZA KIROHO KWA WAHAMIAJI NA WAKIMBIZI


Kanisa linapenda kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa wahamiaji na wakimbizi kwa kutambua kwamba, hii rasilimali kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni watu wenye utajiri wa maisha ya kiroho na kitamaduni, ingawa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha zinazowalazimisha kuyakimbia makazi yao. Wahudumu wa maisha ya kiroho kwa wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kutambua dhamana hii nyeti ambayo wanakabidhiwa na Mama Kanisa ili kuweza kuitekeleza, ili kuwaingiza wahamiaji na wakimbizi hawa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi na udumishaji wa Kanisa la kiulimwengu.
Huu ni mwelekeo ambao umetolewa hivi karibuni na Monsinyo Gabriele Bentoglio, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum wakati wa semina elekezi iliyoandaliwa mjini Roma na Mfuko wa Wakimbizi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Semina hii ilihudhuriwa na wakuu wa idara ya wakimbizi kutoka majimbo mbali mbali nchini Italia, walioteuliwa hivi karibuni katika wadhifa huu kutambua: sera, miongozo na mikakati ya Mama Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa wanaonekana kana kwamba, ni tishio la amani, usalama na mafungamano ya kijamii.
Wajumbe wengine waliohudhuria semina hii elekezi ni wadau mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaowasili nchini Italia kwa ajili ya kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Wote hawa wamefafanuliwa kwa kina mapana dira na miongozo ya Mama Kanisa kwa ajili ya utume kwa wakimbizi na wahamiaji. Wameangalia pia kwa undani miundo mbinu inayotakiwa kutumiwa kwa ajili ya huduma ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji.
Wamissionari wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaangalishwa na Mama Kanisa kuwa makini, ili katika huduma zao, wasiwageuze waamini hao kuunda Kanisa lao jipya, bali wasaidiwe kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia ili kuendeleza umoja na mshikamano wa Kanisa unaoshuhudiwa hata katika utofauti wa lugha, tamaduni na mahali anapotoka mtu, kwani wote hawa wamekombolewa kwa njia ya Damu Azizi ya Mwanakondoo. Kundi hili lisitengwe hata mara moja na hivyo kudhani kwamba, wao ni kisiwa katika bahari kubwa ya familia ya Mungu, hali ambayo pia inaweza kupelekea waamini wa Makanisa mahalia kuwatenga pia.
Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kujishughulisha zaidi na mchakato wa ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano kati ya watu ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano! Padre Bentoglio anakaza kusema, waamini wahamasishwe kujenga na kuimarisha umoja unaoshuhudiwa katika mshikamano wa upendo pamoja na kusimama kidete kupinga mambo yote yanayopelekea nyanyaso na dhuluma dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.
Kwa bahati mbaya wakimbizi na wahamiaji hawa wanaponusurika kifo maji na utupu jangwani, wakati mwingine wanaangukia mikononi mwa wafanyabiashara haramu ya binadamu na hivyo wanageuzwa kuwa ni bidhaa sokoni au hata wakati mwingine, wanachomolewa viungo kwa ajili ya kukidhi soko la viungo vya binadamu ambalo kwa sasa linaendelea kupanuka na kuongezeka kwa kasi!
Tafiti zinaonesha kwamba, hata leo hii bado kuna ubaguzi wa rangi na kwa namna ya pekee kwenye miaka ya hivi karibuni ambamo kumekuwepo na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, hali inayopelekea baadhi ya wananchi kujenga hisia potofu kwa kudhani kwamba, hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo ni matokeo ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambao wanaendelea “kukomba” uchumi wa nchi yao.
Padre Bentoglio baada ya kufafanua malengo na changamoto wanazoweza kukabiliana nazo katika utume kwa wakimbizi na wahamiaji, anasema wimbi la wakimbizi duniani si tatizo mtambuka bali ni changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa sera na mikakati makini, ili kuhakikisha kwamba, kundi hili linahudumiwa vyema: kiroho na kimwili. Mwelekeo wa sasa wa wimbi kubwa la wakimbizi ni kama lile lilojitokeza kwenye Karne ya 20, lakini hali ya sasa ni changamani zaidi.
Hapa kuna makundi makubwa ya watu wanaotofautiana kwa dini na imani; tamaduni na mahali anapotoka mtu; sababu na malengo. Kuna idadi kubwa ya watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa, watu ambao wanakimbia vita, nyanyaso na dhuluma za kidini: Hawa ni waathirika wa mipasuko ya kidini, kisiasa na kijamii na kwamba, baadhi ya wao ni watu ambao wametikiswa na kuguswa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna waamini wa dini mbali mbali duniani wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha katika nchi ambazo zinatambulika kihistoria kuwa ni nchi za Kikristo! Hapa changamoto ni majadiliano ya kidini ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu, vinginevyo hasira na chuki za kidini zinaweza kuibuka mara moja!
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji katika karne ya ishirini na moja ni matokeo ya umaskini mkubwa na matumizi mabaya ya rasilimali ya dunia ambako kuna sehemu wanakula na kusaza na sehemu nyingine ya dunia wanaambulia pakavu ingawa wana rasilimali ambayo ingeweza kusaidia kupambana na umaskini. Ni makundi ya watu wanaoteseka kutokana na biashara haramu ya silaha inayowaneemesha watu wachache kwa mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia!
Padre Bentoglio anakaza kusema, leo hii sura ya wakimbizi na wahamiaji inamwonesha mwanadamu mwenye kiu ya kutaka kuonja huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wamissionari wa wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kujenga misingi ya: upendo na ukarimu; kwa kutambua na kuheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi bila kusahau tofauti za kidini na kitamaduni zinazoweza kujitokeza. Wasaidie mchakato wa ugiribishaji ili serikali pamoja na taasisi zake ziweze kusimama kidete katika kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Hii ni dhamana nyeti ambayo wakati mwingine itawasababishia magumu na changamoto katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao kati wakimbizi na wahamiaji, lakini hawana budi kupiga moyo konde na kusimamia kanuni msingi zinazoheshimu na kuthamini utu wa binadamu! Dhamana hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la kiulimwengu hali inayoshuhudiwa kwa njia ya Makanisa mahalia. Hapa wamisionari wanaweza kushuhudia umoja katika utofauti, kielelezo makini cha Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.
Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji hata kama si sehemu ya karama na vipaumbele vyao, kwani lengo ni kujenga familia ya binadamu inayowajika, kwa kusikiliza kilio cha maskini na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Bado kuna kilio kikubwa cha maskini ambacho hakijasikilizwa na wengi na watu wanaendelea kuishi kana kwamba hakuna kinachotendeka. Dhamiri za watu zinaonekana kufa kwa kuelemewa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI