VIJANA WANA NAFASI KUBWA KATIKA MABADILIKO
Siku ya Vijana Duniani ni maadhimisho ya imani, matumaini na mapendo kumzunguka Yesu Kristo Mfufuka ambaye yuko kati ya watu wake. Vijana wanahamasishwa kuwa na ari na mwamko mpya wa kutaka kumfuasa, kuishi pamoja na kupyaisha urafiki wao na Kristo Yesu kwa njia ya kuimarisha mahusiano mema kati ya vijana pamoja na huduma makini kwa jirani, ili kuonja na kuonjeshana Injili ya furaha hata katika hali tete za maisha!
Ni Kristo Yesu anayewaalika vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kuungana pamoja kuadhimisha Siku ya XXXI ya Vijana Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Heri wenye kusamehe, wenye moyo wa huruma na wanaoweza kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zao. Maadhimisho haya nchini Poland, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II anayeendelea kuwaangalia vijana kutoka mbinguni ili kuonesha ile sura ya huruma ya ujana wa Poland. Maadhimisho haya ni kilele cha Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana wa kizazi kipya.
Ni maneno yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 28 Julai 2016 wakati wa hotuba yake kwenye mapokezi rasmi ya vijana kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani. Kati ya mambo ambayo amejifunza katika maisha na utume wake kama Askofu ni kutafakari kwa kina: matamanio, dhamana, mateso na nguvu ambayo vijana wanaimwilisha katika maisha yao ya kila siku, baada ya kuguswa na Yesu kutoka katika undani wa maisha yao, tayari kushirikishana na wengine ndoto na vipaumbele vya maisha yao, ili kuleta mageuzi duniani.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana ni chachu ya mageuzi duniani, zawadi ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kanisa na Ulimwengu unawaangalia vijana na wanataka kujifunza kutoka kwao ili kupyaisha imani katika matumaini ya huruma ya Baba wa milele ambayo daima inaonesha sura ya ujana, mwaliko kwa vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, furaha, upendo na mshikamano.
Vijana wanaonesha ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa kwani wamekirimiwa moyo wa huruma unaothubutu kujisadaka, kutoa huduma na kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi. Moyo wenye huruma ni kimbilio kwa watu wasiokuwa na makazi; una uwezo wa kujenga mazingira ya kifamilia kwa wakimbizi na wahamiaji; unaonesha wema na upendo kwa wote wenye njaa na mahangaiko ya maisha.
Huruma ya Mungu maana yake ni kuwa na fursa ya maisha, kwa leo na kesho yenye matumaini zaidi inayojikita katika: dhamana ya maisha, imani, uwazi, ukarimu, upendo na ndoto katika maisha ya ujana. Katika mwelekeo huu, vijana wanaweza kuwa na upendo na huruma kwa wale wanaoteseka; kwa maskini na watu wasiokuwa na amani na utulivu katika maisha; lakini zaidi kwa wale wanaokosa zawadi ya imani.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, anaumia sana moyoni mwake, anapokutana na vijana waliozeeeka hata kabla ya wakati; vijana ambao wanakula pensheni hata kabla ya kuzeeka; vijana waliokata tamaa wanaotembea huku wakiwa wamejiinamia kana kwamba, maisha hayana tena thamani! Hawa ni vijana walichoka na wanataka pia kuwachosha wengine. Inasikitisha kuona vijana wakiteleza katika tunu msingi za maisha na kuogelea katika matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo; mambo yanayowapatia vijana furaha ya mpito, lakini gharama yake ni kubwa kwani vijana wanapokwa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.
Baba Mtakatifu anawataka vijana kusimama kidete na kamwe wasiwapatie mwanya wale wale wanaotaka kuwapoka furaha na ndoto ya maisha bora zaidi kwa kuwapandikizia machungu katika maisha. Vijana wanapaswa kujiaminisha kwa Kristo Yesu, zawadi ya Baba wa milele aliyejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa binadamu, tayari kuwanyanyua wale walioanguka! Hata pale wanapoanguka, vijana wawe na ujasiri wa kusimama tena na kuendelea na safari bila woga na makunyanzi, kwani Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo. Yesu yuko tayari kuwanyooshea mikono na kuwainua pale wanapoanguka!
Baba Mtakatifu kwa sauti kubwa akawauliza vijana kama wameelewa ujumbe wake! Hii ni kwa sababu, wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu asubuhi, alijikwaa na kuanguka, lakini akasimama na kuendelea na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujenga utamaduni wa ukarimu pamoja na kusikiliza kwa makini kama alivyofanya Maria, Yesu alipoitembelea familia yake.
Katika maadhimisho haya, Yesu anataka kuingia katika maisha na vipaumbele vya vijana, kumbe wajibu wa vijana ni kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya iwe ni fursa ya kusikiliza Neno, Kuadhimisha Mafumbo ya Imani; Kusali na Kuadhimisha Injili ya furaha. Kijana anayempokea Yesu, anajifunza pia kupenda ili kupata utimilifu wa maisha unaofumbatwa katika huruma ya Mungu. Kwa kumsikiliza Yesu, vijana watapata amani na utulivu wa ndani. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu, awasaidie vijana katika hija ya kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha yao.
Vijana wawaombee hata wale wanaotaka kuwatendea mabaya; watu wanaotoka katika tamaduni tofauti. Wawe na uso wa huruma kwa wazee ili kuweza kujifunza hekima ya maisha kutoka kwao. Hatimaye, vijana wamwombe Mwenyezi Mungu ili awasaidie kushirikishana upendo wenye huruma, ili mwisho wa siku waweze kupata utimilifu wa maisha kwa kuanza na kuhitimisha kwa huruma, kwani hili ndilo fungu bora zaidi, ambalo kamwe halitaondolewa kutoka kwao!
This comment has been removed by the author.
ReplyDeleteTushukuru sana TEC kwa kutuhabarisha, kutuelimisha, kutuburudisha na kutuonya.
ReplyDeleteTushukuru sana TEC kwa kutuhabarisha, kutuelimisha, kutuburudisha na kutuonya.
ReplyDeleteTunawashukuru TEC kwa kutuhabarisha, kutuelimisha, kutuburudisha na kutupatia.
ReplyDelete