FAMILIA,KAZI NA MAPUMZIKO VINA UMUHIMU MKUBWA SANA..


Kazi ni utimilifu wa maisha ya binadamu; kazi inatoa uhakika na usalama wa maisha ya familia; kazi na familia ni mambo makuu mawili yanayotegemeana na kukamilishana. Tangu kuumbwa kwa ulimwengu mwanadamu alipewa dhamana ya kufanya kazi kama sehemu ya mchakato wa kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji. Kazi inapaswa kuheshimu na kuzingatia utuwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kazi inapaswa kuwa ni utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake anawataka Wakristo kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa na kwamba, asiyefanya kazi na asile.
Ukosefu wa fursa za ajira ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa hata Yesu katika Agano Jipya aliwaonea huruma wale watu waliokuwa wamekaa “kijiweni” siku nzima, hali inayoonesha mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na fursa za ajira katika jamii; matokeo yake ni watu kukosa mahitaji yao msingi na umaskini wa hali na kipato kuendelea kuongezeka maradufu. Ukosefu wa fursa za ajira unaathiri amani na utulivu wa maisha ya ndoa na familia.
Lakini utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya kazi, kama sehemu ya ujenzi wa jamii inayowajibika. Kimsingi haya ndiyo mawazo makuu ambayo Mama Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni amejitahidi kuyapatia msukumo wa pekee katika tafakari zake kuhusu familia na kazi. Haya yamesemwa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia wakati alipokuwa anachangia mada kuhusu: Familia na Kazi; mambo msingi yanayoiwezesha jamii kujisimika katika utu, Alhamisi, tarehe 30 Juni 2015 kwenye Tamasha la Sita la Kazi nchini Italia.
Askofu mkuu Paglia anafafanua kwamba, dhana ya kazi inafumbata masuala ya uchumi na soko; kanuni, sheria na maadili. Hapa familia zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kuzingatia haki na mahitaji yake msingi kwa kuondokana na ubinafsi ambao unaendelea kuvuruga tunu msingi za maisha ya kifamilia. Lakini ikumbukwe kwamba, familia na jamii ni chanda na pete ni mambo ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa. Kuna uhusiano wa dhati kati ya: mtu, familia na jamii na kwamba, wote hawa wanaunganishwa na kufungamanishwa na kazi ambayo kimsingi ni wajibu wa binadamu katika kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji.
Pale familia inapoondolewa kutoka katika kazi, hapo kunakosekana uwiano na matokeo yake, utu na heshima ya binadamu vinakuwa mashakani. Familia ni kitovu cha ustawi na maendeleo ya wote. Kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa katika jamii nyingi kwenye nchi zinazoendelea sanjari na malezi tenge ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kutikisha nguzo msingi za maisha ya kifamilia. Matokeo yake ni jamii kuendelea kukumbatia utamaduni wa kifo.
Vijana wanapaswa kuwa na uhakika wa fursa za ajira ili kujiwekea sera na mikakati ya maisha kwa siku za usoni, vinginevyo vijana wengi watashindwa kufanya maamuzi magumu ya maisha kwa kuchagua wenzi wao na hatimaye kufunga ndoa. Inasikitisha kuona sera nyingi za kiuchumi hazitoi kipaumbele cha pekee kwa familia na matokeo yake familia inaonekana kuwa ni mzigo mzito huu ni mwelekeo potofu kuhusu familia. Hapa, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kupewa uzito wa hali ya juu. Familia, sherehe na kazi ni mambo ambayo yanapaswa kuwa ni sehemu ya maisha ya binadamu.
Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha kazi yake ya uumbaji alijipatia siku ya mapumziko, changamoto kwa binadamu kufurahia siku za mapumziko ili kupata nafasi ya kutafakari na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za usoni. Lakini kutokana na uchu wa mali na faida ya haraka haraka, leo hii binadamu amegeuzwa kuwa ni mtumwa wa kazi na wala hana hata wakati wa kujipumzisha. Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Sherehe inakuwa ni fursa ya  kutukuza na kuendeleza utakatifu wa binadamu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Askofu mkuu Vincenzo Paglia anawataka wajumbe wa tamasha la kazi nchini Italia kusaidia mchakato wa maboresho ya dhana ya kazi na fursa za ajira; umuhimu wa kujikita katika welezi, juhudi na maarifa ili kuongeza tija na ufanisi zaidi. Kanuni, sheria, miiko na maadili ya kazi yanapaswa kuzingatiwa, ili kumwezesha mwanadamu kufurahia kazi, Utu na heshima ya binadamu vilindwe na kuendelezwa kwa kupambana na kazi za suluba, dhuluma na nyanyaso dhidi ya wafanyakazi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI