PAPA ALIPOZURU KAMBI YA MATESO NA MAUAJI
Mama Noemi di Segni, Rais wa Jumuiya za Wayahudi nchini Italia amemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko akimtakia safari njema huko Poland anakokwenda kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016. Poland ni nchi ambayo imebarikiwa kwa mambo mengi, lakini pia palikuwa ni mahali ambapo Wayahudi wengi kutoka Italia walikumbana na mateso na hatimaye kuuwawa kikatili kwenye kambi za Auschwitz- Birkenau.
Nia ya Baba Mtakatifu Francisko kutembelea katika kambi hizi za mateso katika hali ya ukimya, ili aweze kupata nafasi ya kulia peke yake dhidi ya ukatili wa utu na heshima ya binadamu ni tukio ambalo linasubiriwa na watu wengi duniani. Huu ni ukurasa mchungu wa historia na donda ambalo liko wazi katika historia ya Bara la Ulaya. Ni tukio ambalo linaendelea kusuta dhamiri za watu wengi duniani kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, uhuru na demokrasia ya kweli.
Mama Noemi di Segni anapenda kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uamuzi wake wa busara wa kwenda katika eneo hili katika hali ya ukimya pasi na hotuba ni alama ya sala na tafakari ya kina, lakini yenye mwangi mkubwa kwa maisha ya watu waliokwenda kwenye kambi hizi, lakini hawakupata nafasi ya kurejea tena kuungana na ndugu zao kutokana na mateso na kifo, wakapotelea huko kama ndoto ya mchana! Sala ya Baba Mtakatifu pamoja na sala za watu wenye mapenzi mema zinalifanya eneo hili la mateso kuwa ni eneo la Ibada.
Hii ni changamoto kwa binadamu kugundua tena ndani mwake tunu msingi za maisha ya kiutu, ili kuweza kusimama kidete: kuzilinda, kuzitetea na kuzidumisha; kwa kuheshimiana na kutunza uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata leo, kuna changamoto kubwa zinazoendelea kutishia usalama wa maisha na tunu msingi za kiutu na kitamaduni zilizoibuliwa mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Hapa katika majivu ya kambi za mateso na maeneo mengine yanayokumbatia utamaduni wa kifo, kuliweza kuibuliwa demokrasia, umoja wa Ulaya na uwepo wa taifa la Israeli.
Kambi hizi ni mahali ambapo panapaswa kukumbukwa kuhusu mauaji ya Shoah ili kuhakikisha kwamba, kina mtu bila ubaguzi anapata fursa ya maendeleo na maisha bora kwa sasa na kwa siku za usoni. Dini na viongozi wake, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba wanakuwa ni mfano bora wa kuigwa na waamini wao kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kitamaduni.
Hii ni dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa na viongozi wa kidini kwa kushirikiana na kushikamana kwa dhati, huku wakitambua kwamba, tunu msingi zinazowaunganisha ni nyingi zaidi, ikilinganishwa na yale mambo yanayowagawa na kuwavuruga. Ni katika mwelekeo huu, nchi hii ambayo imelaaniwa kutokana na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia inaweza kugeuka kuwa ni chemchemi ya utakatifu wa mashuhuda walioyamimina maisha yao kwa ajili ya upendo na maridhiano kati ya watu. Kumbukumbu ya maisha yao, ibarikiwe! Mama Noemi di Segni, Rais wa Jumuiya za Kiyahudi Italia, anahitimisha barua yake kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu akiyaelekeza mawazo yake nchini Poland.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment