MASOMO YA LEO
JUMAMOSI WIKI YA 13 YA MWAKA-C
Somo: Amo 9:11-15
Zab: 85:9, 11-12
Injili: Mt 9:14-17
Nukuu:
“Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka,
na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama
siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa
jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo,” Amo 9:11-12
“Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo
alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye
mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka,” Amo 9:13
“Yesu akawaambia,
Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao?
Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga,” Mt
9:15
“Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi
kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale
palipotatuka huzidi,” Mt 9:16
“Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na
kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika;
bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote,” Mt 9:17
TAFAKARI: “Katika Kristo na ndani ya Kristo, yote
yatafanywa upya. Tusife moyo huyu ni Mungu pamoja nasi, Imanueli, Mt 1:23.”
Wapendwa wana wa Mungu, ‘unabii licha ya kubeba ujumbe wa
Mungu katika misingi ya kufundisha, kuonya na kutoa angalizo, sehemu kubwa ya ujumbe
huu wa Mungu hubeba tumaini jipya la kule tunapokutamani ambapo ndipo kusudi
zima la Mungu katika ukamilifu wake. Na wito wetu kila siku kama Yesu
anavyotuamuri ni kwamba,
‘tuwewakamilifu, kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu,’ Mt 5:48.
Kuwa mkamilifu kama Mungu alivyo ni kuwa Mtakatifu. Bila utakatifu huwezi kuwa
katika himaya ya Mungu. Kuwa mwenyeji wa Mbinguni lazima uwe mtakatifu. Na hivi
ndivyo asemavyo Mtume Paulo kwamba, “tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji,
bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu,” Efe
2:19. Maneno haya ya Mtume Paulo yanatufikirisha uwepo wetu hapa duniani. Hapa
tulipo, yaani, duniani, siyo makazi yetu ya kudumu. Tupo hapa kwa kujiandaa tu
kwa uzima wa milele. “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko
tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa
unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo
aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake,” Flp 3:19-20
Hili ndilo tumaini la Mungu na la kinabii kwa wale
aliowaridhia kuupitisha ujumbe wake, yaani, manabii. Nabii Amosi anafikisha
ujumbe huu wa Mungu wenye matumaini ambao ni uthibitisho wa Mungu aliye hai na
mwenye kuiona historia ya watu, na mwenye kutembea nao katika historia hiyo
yenye kila aina ya dhoruba. Dhoruba na misukosuko aipatayo mwanadamu katika
historia yake na kuyakabili katika matumaini huwa ndiyo ponya yake ya mwili na
roho. Na huu ndio ujembe wa kinabii na matumaini kwa wana wa Israeli baada ya
mateso waliyoyapata ndani ya utawala wao, na nje ya utawala wao. Na “Siku hiyo
nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka;
nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki
mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye
hayo,” Amo 9:11-12. Mungu hachoki kufanya nasi agano pale tunapomrudia katika
kweli na haki.
Hata pamoja na kufanya agano hilo la kweli na haki kama
alama ya kujirudi na kufuata njia iliyo salama, Mungu haachi kutupa angalizo
ilihali akijua fika hali zetu na ubinadamu wetu, yaani, ‘maanguko yetu.’ Naye
mjumbe wa Mungu, Nabii Amosi, anasema, “Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana,
ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia
apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka,”
Amo 9:13. Neema na baraka tuzipatazo katika maisha si kitu cha kubeza, bali ni
kitu cha kuthamini na kulindwa katika maana ya kukipigania kisipotee. Hata
hivyo, ni vyema tuelewe tunda la amani ni haki hasa pale tunapoishi zaidi ya
mtu mmoja. Na haki ni tunda la wajibu. Haki na amani huwepo pale kila mmoja
anapotimiza wajibu wake kadiri ya nafasi na wito wake.
Mungu hatochoka kutuletea na kutukirimia yanayofaa kadiri
ya mahitaji yetu pale tunapodumisha amani ambayo ni tunda la haki, na haki
ikiwa ni tunda la wajibu. Na hivi ndivyo alivyowahaidia wana wa Israeli na
kusema, “Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao
wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu
katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda
yake,” Amo 9:14. Ndugu yangu, ni ndoto ya mchana kweupe kutabiri kuijenga nchi
ya maziwa na asali kwa kukanyaga haki za watu ambao kwa njia moja au nyingine
wana wajibika kwa taifa lao kadiri ya wito na nafasi zao. Huwezi kuwa na amani
kama hakuna haki. Na pasipo haki na amani hapana maendeleo. Na maendeleo
yasiyotokana na utashi wa watu hukosa thamani mbele zao hata kama machoni mwako
yatakuwa ya gharama kubwa. Na mwisho wa siku maendeleo hayo hufifia kama moshi
wa mabua kwa sababu hayakugusa maisha ya watu na hayana maana kwao. Lolote lile
lenye kugusa utashi wa watu ndilo lijengalo na kukuza maisha ya watu kwa sababu
ni zao la kile walicho.
Pamoja na uwezo wako kama kiongozi wa kuona mbele kule
wasipokuona sawa sawa wale unaowaongoza, jaribu mara zote kutembea nao na
kuwaonyesha kule unapopaona. La siyo utafika kule utakapo ilihali wao bado hata
hawajajianda kwa safari hiyo uliyokwisha imaliza. Unapotembea hatua kwa hatua
na wale unaowaongoza Mungu anakuhakikishia hili kama kiongozi, “Nami nitawapanda katika nchi yao, wala
hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu
wako,” Amo 9:15. Na hivi ndivyo uzalendo unavyojengwa. Uzalendo wa watu kamwe
haujengwi kwa shuruti za kiimla, bali uhuru na utashi uliokomaa wenye kuthamini
siyo tu kwamba hiki ni changu bali ni chetu na kina thamani kwa wote na umma.
Zaidi ya hapo ni mbwembwe tu. Na mwisho wa mbwembe ni pale sherehe inapofikia
kikomo chake. Je, maisha si zaidi ya sherehe? Tunahitaji tafakuri ya kina. Na
ndiyo maana katika maisha tunahitaji nyakati za mafungo, yaani, kuyapitia yale
tuliyokwisha yaishi (uzuri na ubaya wake), kuona pale tulipokosea, na kuanza upya
kwa nguvu ili kutokurudia makosa na kufika pale tunapopatamani, yaani,
ukamilifu ambao ndio maisha ya umilele na kusudi la kumbwa kwetu.
Hivyo wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya Injili ya leo,
kufunga ilikuwa moja ya mambo makuu matatu kadiri ya Imani, mila na desturi za
kiyahudu. Kufunga iliendana na kusali, pamoja na kutoa sadaka. Haya mambo
matatu yalikuwa ya msingi sana. Kitendo cha wanafunzi wa Yesu kuonekana
kutokufunga kiliwashangaza na kuwakwaza wengi, na hasa wanafunzi wa Yohane
Mbatizaji. Yesu anapoulizwa swali hili: kwa nini wanafunzi wako hawafungi,
anajibu na kusema, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi
akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo
watakapofunga,” Mt 9:15. Uhusiano wetu na Kristo una sura mbili; kuna wakati wa
furaha na wakati wa huzuni, itupelekayo kwenye utukufu. Tukiwa na Yesu tu wana
wa Bwana harusi na yatupasa kufurahi naye kuliko haki.
Kwa upande wa pili wa uhusianao wetu na Yesu
unatukumbusha upo wakati wa kutoa ushuhuda wa kweli juu ya kile tunachoamini
kuhusu Yesu. Huu ndio wakati wa kuteseka na hata kufa kwa ajili ya Kristo. Huu
ndio wakati wa kufanya toba ya kweli kwa ajili ya maaondoleo ya dhambi zetu.
Huu ndiyo wakati wa kufanywa upya ndani na katika Kristo. Na huu ndio wakati wa
kutakaswa na kubeba bendera ya ushindi ya mwanakondoo.
Nyakati hizi mbili za mahusiano yetu na Kristo ndizo
zitupazo kiini cha imani yatu. Sisi si Wakristo wa Jumapili tu, yaani, pasaka,
bali tu wafuasi wa Kristo siku zote na hasa siku ile ya Ijumaa, yaani mateso na
kufa kifo dini. Tunakufa kifo dini kwa kuIfia kweli siku zote za maisha yetu.
Yatupasa kusimama katika kweli, kufundisha iliyo kweli, kuishi yaliyo kweli, na
kushuhudia lililo kweli, hata kama litagharimu uhai wetu. Haya ndiyo maisha ya
ufuasi wa Kristo ambao tuliowengi hatutaki kusikia.
Jambo lingine la muhimu kujua ni hili: Yatupasa kuelewa
lile lililo la zamani ambalo kwa sasa linakamilishwa na hili jipya, mbalo
tangia awali lilikuwa limejificha ndani ya lile la zamani.“Hakuna mtu atiaye
kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande
cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi,” Mt 9:16. Maana yake nini? Ndugu
yangu, katika safari ya ukombozi wa mwanadamu, katika hatua ya mwanzo ya safari
hiyo, imebebwa katika agano la mwanzo. Agano hili kama lilivyo laelezea
historia ya mwanadamu hatua kwa hatua. Kwa lenyewe agano hili kama lilivyo lina
maana ila limekosa ukamilisho au hitimisho. Ukamilisho wa Agano la kwanza ni
Upya wa Agano jipya, ikiwa ni ufunuo wa wazi wa Mungu kwa tukio la neno
kufanyika mwili. Agano hili jipya licha ya kwamba ni ukamilisho wa agano la
kale, tangu mwanzo lilikuwa limejificha ndani ya agano la kale. Hivyo Yesu
anatutaka kulijua jambo hilo na pia kutenganisha maagano haya mawili katika
“ufahamu wake,” “umaana wake” na “nafasi
zake.” Na hii ndiyo maana ya maneno haya, “Wala watu hawatii divai mpya katika
viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na
viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika
vyote,” Mt 9:17. Hivyo katika jambo hili twapaswa kumfuata Kristo katika
ukamilifu wote na kuachana na michanganyo. Ni heri kuwa baridi au joto, kuliko
kuwa vuguvugu katika Imani. Hili vuguvugu kiimani ndilo litakalo pasua hekalu
hili la Roho Mtakatifu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi
kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale
palipotatuka huzidi,” Mt 9:16
Comments
Post a Comment