KANISA LATOA MSAADA WA MADAWATI 50 MUSOMA



Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma limetoa madawati 50 yenye thamani ya shilingi Milioni 4, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuri na Serikali ya Mkoa wa Mara, na kuwapatia wanafunzi elimu  katika mazingira bora ya kujifunzia.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk Charles Mlingwa katika eneo la Musoma dayosisi(diocese of Musoma),Naibu wa Askofu,kwa niaba ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila padre Julius Ogolla alisema kuwa,Kanisa Katoliki limeweza kutoa kiasi hicho cha fedha  ambazo ni michango na sadaka za waamini wa Kanisa hilo,ili kuunga mkono juhudi za Rais za kutaka kuboresha mazingira mazuri ya wanafunzi kujifunzia shuleni.

Katibu wa Elimu Jimbo la Musoma Padri Julius Magere alisema kuwa,  Kanisa Katoliki ni Miongoni mwa wadau wa elimu katika Mkoa wa Mara,na wameendelea kuwa wachangiaji wakubwa wa maendeleo na ustawi wa jamii kwa ujumla, ili kuweka mazingira ya kuvutia kwa wanafunzi,kwani Kanisa lina shule za awali na msingi takribani 20,shule za Sekondari 6,vyuo vya ufundi viatu 4 na chuo cha Ualimu cha St.Alberto kimoja ,ambapo huduma ya elimu na malezi bora kwa vijana wa Taifa letu katika Taasisi hizo za Kanisa ni mchango dhahiri wa Kanisa katika Jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa madawati hayo,Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk Charles Mlingwa alilishukuru kanisa Katoliki kwa mchango wake huo mkubwa  katika Nyanja mbalimbali,elimu,afya ustawi wa jamii na maendeleo kwa ujumla,pamoja na madhebu mengine ya dini ya mkoa wa Mara kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa, katika kutafuta namna ya kusaidiana kutatua changamoto ya ukosefu wa madawati katika mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa amefurahishwa sana kuona taarifa ya michango ya madawati ofisini kwake, aliyokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa aliyeondoka Magesa Mulongo ambayo inaonyesha  jinsi madhehebu  ya dini yanavyojitolea,madhehebu ya dini yamekuwa ndiyo yanayoisaidia Serikali badala ya Serikali kusaidia madhehebu ya dini,huku akiwaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha zaidi akiomba kanisa liendelee kumkumbuka katika sala.

Naye mkuu wa Wilaya hiyo Vicent Naano alilishukuru Kanisa Katoliki kwa Mchango wake,na kusema kuwa ameanza kupata faraja moyoni kwa sababu kuna wadau wa maendeleo, kama Kanisa Katoliki ambao wanaguswa sana na tatizo la wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini na kuamua kutoa mchango wao wa madawati 50 yenye thamani ya milioni 4 ,hali inayoonyesha moyo wa Kibinadamu,kwa kuwa wakati wa kuapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma alipewa changamoto hiyo ya kuwa Wilaya yake  ni kati ya wilaya ambazo hazijatimiza lengo la madawati pamoja na Wilaya ya Serengeti.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Asteria Luzangi alisema kuwa, Manispaa ya Musoma ni moja kati ya halmashauri ambazo hazijatimiza lengo la madawati,na kwamba msaada huyo umesaidia kupunguza sehemu ya  madawati kwani  hadi sasa wana upungufu wa madawati 1545 na madawati hayo 50 waliyoyapata upungufu umebakia  1495.

 Na.Veronica Modest,Musoma




Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt Charles Mlingwa akikabidhiwa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 4,na Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Padri Julius Ogolla,Kwa niaba ya Mhashamu Baba Askofu  Michael Msonganzila, ikiwa ni sehemu  ya Kanisa Katoliki kutoa mchango, katika kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt John Pombe Magufuri  ya wadau wa maendeleo kila mkoa kuchangia madawati ili kuondoa tatizo la wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa chini yaliyofanyika katika eneo la Musoma Dayosisi(Picha na Veronica Modest

Viongozi kutoka Serikalini akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt Charles Mlingwa,Mkuu wa Wilaya ya Musoma Vicent Naano,Meya wa Manispaa ya Musoma Patrick Gumbo,Afisa Elimu Mkoa wa Mara Hamisi Lissu,Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Asteria Ruzangi na Naibu Askofu padri Julius Ogolla,Murugenzi wa Elimu Jimbo la Musoma Padri Julius Magere,Katibu wa Askofu Padri William Bahitwa,na watumishi wengine wa idara mbalimbali zilizopo katika Jimbo hilo(picha na Veronica Modest)

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU