Sababu za kuondolewa kwa sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu kutoka Kalenda Kuu ya Kanisa Katoliki
Utangulizi:
Kwa muda wa miaka 36,
kuanzia mwaka 1933 hadi mwaka 1969, Sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu ilikuwa
ikisherehekewa tarehe kama hii ya leo yaani tarehe ya kwanza ya mwezi
Julai kila mwaka kwa mbwembwe, kote ulimwenguni katika makanisa ya
Kikatoliki. Kuanzia hapo, Kanisa Katoliki halina tena sherehe ya pekee kwa
heshima ya Damu Takatifu ya Yesu na badala yake kunakuwa na misa ya
kawaida tu.
Chanzo cha Sherehe ya
Sikukuu ya Damu Takatifu ya Yesu:
Sikukuu hii ya Damu
Takatifu ya Yesu ilianza kusherehekewa kwanza huko Uhispania kwenye karne ya 16
hivi. Baada ya muda kupita Mtakatifu Gaspari de Bufalo aliipeleka sikukuu hii
huko Italia ambako nako ilianza pia kusherehekewa.
Wakati wa fujo za kisiasa
na mapigano yaliyokuwa yamezuka mjini Roma, Papa Pius wa X1 alipelekwa
uhamishoni Gaeta, mji mmoja katika Visiwa vile viwili vya Sicili hapo mwaka
1849. Katika safari yake hii ya kuhamishwa alikuwa amefuatana na mwenzi wake
Padri Giovanni Merlini, aliyekuwa Mkuu wa mapadri wa Shirika la Damu Takatifu
ya Yesu.
Baada ya kuwasili kule
Gaeta, Don Merlini alimshauri Papa Pius wa X1 ahaidi kwa kiapo kuwa ataifanya
Sikukuu ya Damu Takatifu ya Yesu isherehekewe na Kanisa Katoliki kote
ulimwenguni iwapo atafanikiwa kuyatwaa tena Majimbo yake ya Kipapa.
Papa alilifikiria ombi
lile kwa makini sana lakini hakumpa jibu la papo kwa papo. Siku chache baadaye,
ilipofika siku ya tarehe ya 30 ya mwezi wa Juni, mwaka wa 1849, Jeshi la
Kifaransa liliishinda Roma na likawasambaratisha askari wote waasi wa Jamhuri
ya Kirumi na hivyo kuwafanya wasalimu amri.
Baada ya tukio hilo, Papa
Pius wa X1 alimpelekea ujumbe Padri Merlini, yule aliyemshauri atoe ahadi ya
kiapo ukiwa kama jibu kwa ombi alilokuwa amempa. Ujumbe huu ulipelekwa na
Askofu Yosefu Stella, aliyekuwa wakati huo akishughulika na masuala ya mambo ya
ndani ya ofisi ya Papa Pius wa X1.
Ujumbe wenyewe ulikuwa na
maneno kama haya yafuatayo: ‘ Papa haoni kuwa ni jambo la kufaa kutoa ahadi kwa
kiapo. Hata hivyo, Papa yuko radhi kutoa kibali mara moja cha kueneza sherehe
ya Damu Takatifu ya Yesu kwa mataifa yote ya Kikristo kote ulimwenguni’.
Tarehe ya 10 ya mwezi
Agosti ya mwaka ule ule wa 1849 Sikukuu ya kusherehekea Damu Takatifu ya Yesu
iliorodheshwa katika Kalenda Kuu ya Kanisa Katoliki.
Kalenda hiyo ilikuwa
imeonyesha kuwa Sikukuu ya kusherehekea Damu Takatifu ya Yesu iwe
Jumapili ya Kwanza ya mwezi Julai, ambayo ni Jumapili ya Kwanza baada ya tarehe
30 ya mwezi Juni ili iwe kumbukumbu ya ukombozi wa Roma kutoka kwa askari
waasi.
Wakati wa kipindi cha
utawala wa Papa Pius wa X, tarehe ya kusherehekea Sikukuu hiyo ya Damu Takatifu
ya Yesu ilibadilishwa na kuwa tarehe 1 ya mwezi Julai. Badiliko hili lilitokana
na nia ya Papa ya kupunguza idadi ya sherehe zinazoangukia siku za Jumapili.
Mwaka wa 1933, Papa Pius
wa X1 alipandisha hadhi ya sikukuu hiyo kwa kumbukumbu ya kutimiza miaka 1900
tangu Bwana wetu Yesu Kristo asulubiwe na kufa msalabani.
Wakati wa mapitio ya
Kalenda Kuu ya Kanisa Katoliki yaliyofanywa na Papa Yohani wa XX111 hapo mwaka
1960, Sikukuu hiyo ya Damu Takatifutika ya Yesu iliongezewa hadhi tena na
kuwekwa katika daraja la Kwanza la sherehe muhimu za Kanisa Katoliki.
Hata hivyo, ilipofika
mwaka 1969 Sikukuu hii ya Damu Takatifu ya Yesu iliondolewa kabisa kutoka
Kalenda Kuu ya Kanisa Katoliki. Uamuzi huu ulitokana na ukweli uliofika
kuafikiwa na Viongozi wa Kanisa Katoliki kuwa Damu Takatifu ya Mwokozi, Bwana
wetu Yesu Kristo inaunganishwa na kusherehekewa katika sikukuu za ibada zingine
za hadhi ya juu kama zile za Mateso yake, Sherehe ya Mwili Wake pamoja na
Damu yake Takatifu, Sherehe ya Moyo wake Mtakatifu, na sherehe ya Kutukuka kwa
Msalaba. Kwa hiyo haikuonekana kama kulikuwa na ulazima wa kuwa na sikukuu ya
pekee tena kwa heshima ya Damu Takatifu ya Yesu.
Umhimu wa Damu Takatifu ya Yesu:
Kwa mujibu wa imani
ya Kanisa Katoliki, Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ina thamani kubwa sana kwa
sababu Damu hiyo ni malipo yake Yeye Mwenyewe Bwana wetu Yesu Kristo ya
ukombozi wa wanadamu. Bila kule kumwagika kwa damu hiyo, kusingekuwa na
maondoleo ya dhambi. Yesu Kristo, ‘Neno lililogeuka kuwa Mwili’ hakuutoa mwili
wake kwa ukombozi wa ulimwengu huu kwa namna nyepesi nyepesi tu; bali alikuwa
tayari kuutoa huo Mwili wake kwa kifo cha msalabani, kifo cha umwagikaji wa
damu kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu wote.
Tunaamini kuwa Bwana wetu Yesu
Kristo aliutoa mwili wake na damu yake ambavyo sote tunakiri kuwa
ni vya thamani kubwa sana kwa ajili ya wanadamu wote, bila kujali madhehebu yao
ya dini au tofauti za imani zao. Yeye alilipia kila aina ya dhambi zilizokuwa
zimetendwa na wanadamu wote kwa jumla kwa umwajikaji wa hiyo damu.
0754 054 004 kwa msaada
wa mtandao.
Comments
Post a Comment