Changamoto za kihistoria katika Kanisa:Skapulari ya Bibi Yetu wa Mlima Karmeli
Changamoto za kihistoria katika Kanisa
Skapulari ya
Bibi Yetu wa Mlima Karmeli
Na Philip Komba
Skapulari ya kwanza kuanzishwa:
Skapulari ya Bibi
Yetu wa Mlima Karmeli, au inayoitwa pia kwa kifupi ‘Skapulari Kahawia’ au
inayojulikana vilevile kwa jina moja tu ‘Skapulari’ ni skapulari inayojulikana
zaidi kuliko aina zingine zote za skapulari. Aina hii ya skapulari ni pia ya kwanza kuanzishwa kati ya
skapulari zote zinazotumiwa na wakristo wakatoliki wakati huu. Baadhi ya skapulari
hizo zingine ni kama hizi zifuatazo: Skapulari ya Moyo Mtakatifu wa Yesu,
Skapulari ya Utatu, Skapulari ya Njia Tano, Skapulari Nyeupe, Skapulari Nyeusi,
Skapulari Buluu, Skapulari ya Kijani, Skapulari ya Mtakatifu Mikaeli n.k.
Kwa
kuthibitisha umaarufu wa skapulari hii, hata kama ukiandika neno hili moja tu
‘Skapulari’ kama ilivyodokezwa hapo juu, kwa mfano, ‘Sherehe ya Skapulari’ itaeleweka ni skapulari hii tu ya Bibi Yetu
wa Mlima Karmeli. Kwa kuzipambanua skapulari zile zingine ni lazima uonyeshe kwa kutaja jina la skapulari hiyo, kwa mfano,
Skapulari ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, au Skapulari ya Mtakatifu Mikaeli au
Skapulari Nyeusi au Skapulari Buluu n.k.
Historia ya uanzishwaji
wa Skapulari hiyo ya Bibi Yetu wa Mlima Karmeli :
Kwa mujibu wa
mapokeo matakatifu, Mama Bikira Maria alimtokea Mtakatifu Simoni Stock tarehe
ya 16 ya Mwezi wa Julai, mwaka wa 1251 huko Uingereza akiwa ameshika skapulari
mkononi mwake na akamwambia Mtakatifu Simoni Stock kama ifuatavyo: ‘Chukua
skapulari hii mtoto wangu mpendwa kwa ajili ya Shirika lako la Kitawa la
Karmeli; skapulari hii iwe kama beji ya Kikundi changu cha kutoa sadaka kwa
jamii na pia kama alama maalum ya neema kwako na kwa wanachama wote wa Shirika
la Wakarmeli. Yeyote anayekufa amevaa vazi hili hataunguzwa na moto wa milele.
Hii ni alama ya wokovu, kinga ya majanga yote, ahadi ya amani na hati ya
mapatano.’
Pamoja na maneno
hayo kuwekwa katika mtiririko huu tunaouona mahali pengi katika maandishi, kwa
kweli hakuna mwenye uhakika wa maneno
yenyewe hasa yaliyokuwa yametamkwa na Mama Yetu wa Mlima Karmeli. Kwa mujibu wa
ensaiklopidia ya masuala ya Kanisa Katoliki, maneno yanayosemekana yalitamkwa na
Bibi Yetu wa Mlima Karmeli yalikuwa
yameonekana katika hati moja hapo mwaka 1642 iliyosema kuwa maneno hayo
yalikuwa yamesemwa kwa sauti na Simoni stock kwa katibu wake ili huyu katibu
ayaandike kama alivyokuwa anayasikia yakitamkwa na simoni Stock mwenyewe.
Ingawa nyaraka za kihistoria hazina uthibitisho
wa maneno halisi yaliyokuwa yametamkwa na Bibi Yetu wa Mlima Karmeli,
maudhui ya maneno yenyewe yanaaminika kuwa ni ya kweli. Hii ni kusema kuwa, ni
kweli kwamba Bibi Yetu wa Mlima Karmeli alimhakikishia Mtakatifu Simoni Stock kimwujiza
juu ya ulinzi wake maalum kwa Shirika lake la Wakarmeli na kwa wale wote ambao hujiunga
na shirika hilo kwa njia ya ibada hata kama hatuwezi kuyapata maneno yenyewe
halisi yaliyosemwa na huyu Bibi Yetu wa Mlima Karmeli.
Masharti ya Kupata
Manufaa ya Neema za Skapulari:
Uhalisia wa maneno
aliyopewa Mtakatifu Simoni Stock na Mama Yetu wa Mlima Karmeli:
Ahadi na masharti yafuatayo
yana uhusiano wa karibu na amri au tangazo linalosemekana lilitolewa na Papa
Yohane wa XX11. Tangazo rasmi kuhusu ahadi
hizo lililokuwa limetolewa, inavyoaminika, tangu miaka ya 1400, halikuwa
limesikika kutajwa kwa zaidi ya miaka 100 baada ya kutangazwa kwake hapo mwaka
1322 na hakukuwa na waraka wowote ulioandikwa na Papa Yohane wa XX11 kuhusu
suala hili. Imefika baadaye kusadikika
tu kwa jumla kwamba ingawa huo waraka
unaosemekana uliandikwa na Papa Yohane wa XX11 hauonekani, zile ahadi na
masharti ni halali na mapapa wengi wamewaruhusu Wakarmeli kuzitangaza ahadi
hizo.
Ahadi zenyewe ni kama hizi zifuatazo:
Mkristo
aliyekwisha kupokelewa rasmi kama mwanachama wa Shirika la Karmeli ni lazima:
·
avae
skapulari muda wote,
·
atunze
usafi wa moyo kulingana na hali ya maisha yake,
·
asali
kila siku sala kwa heshima ya Mama
Bikira Maria: Baba yetu moja, Salamu Maria moja, na Atukuzwe Baba na Mwana na
Roho Mtakatifu au,
azingatie siku zote za kufunga kwa
mujibu wa maelekezo ya Kanisa Katoliki na pia ajinyime kula nyama siku za
Jumatano na Jumamosi au
1) asali Rozari kila siku au
2) afanye shughuli nyingine yenye
manufaa ya kiroho; lakini sharti hili libadilishwe tu baada ya kuruhusiwa na padri
aliyepewa madaraka ya kubadili sharti hili.
Umbo na mwonekano wa
Skapulari:
Skapulari ya Bibi Yetu wa Mlima Karmeli, kwa kawaida, huwa ni
ya rangi ya kahawia ingawa ya rangi nyeusi huwa pia inakubalika. Skapulari hiyo
ni lazima itengenezwe kwa kipande cha kitambaa cha sufu. Picha inayoonekana
katika skapulari hiyo ni ile ya Bibi Yetu wa Mlima Karmeli akimpa skapulari
Mtakatifu Simoni Stock. Skapulari inaweza pia kuwa na michoro ya picha tofauti
na hiyo. Kwa mfano , inaweza kuwa na picha ya Bibi Yetu wa Guadalupe, picha ya
Moyo Mtakatifu, picha ya Mtakatifu Benedikti au inaweza kutokuwa na picha
yoyote yoyote. Ni jambo la kawaida sana skapulari kuandikwa maneno ya zile
ahadi za Bibi Yetu wa Mlima Karmeli.
0754 054 004 kwa msaada wa mtandao.
Comments
Post a Comment