TANZIA
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, amefariki dunia, Jumatano tarehe 13 Julai 2016 akiwa nchini Poland ambako alikuwa anatibiwa kutokana na kusumbuliwa kwa Saratani ya ini, Hayati Askofu mkuu Zimowski alizaliwa kunako tarehe 7 Aprili 1949 na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 67. Alipewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 25 Mei 1973 na Askofu Jerzy Karol Ablewicz wa Jimbo Katoliki la Tarnow.
Tarehe 28 Machi 2002 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Radom, nchini Poland na kuwekwa wakfu tarehe 25 Mei 2002 kwa wakati huo na Kardinali Joseph Ratzinger. Kunako tarehe 18 Aprili 2009, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu.
Kuanzia Mwezi Desemba 2014, Askofu mkuu Zimowski afya yake ikaanza kuingia mgogoro na kulazimika kulazwa mjini Varsavia na huko akagundulika kwamba, alikuwa anasumbuliwa na saratani ya ini. Akapata matibabu na baadaye akarejea mjini Vatican kuendelea na utume wake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment