JIFUNZENI KUSIKILIZA KWA UMAKINI
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Julai 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aligusia kuhusu Injili ya Luka inayoonesha jinsi familia ya Maria na Martha ilivyompokea na kumhudumia Yesu alipokuwa njiani kuelekea Yerusalemu. Maria alikuwa ameketi miguuni pa Yesu akimsikiliza kwa makini wakati ambapo Martha alikuwa anachakarika jikoni ili kumkirimia mgeni wao. Lakini, Martha alipoelemewa na kazi za jikoni alikwenda na kumwambia Yesu amwambie Martha ili aende kumsaidia kazi za jikoni, lakini Yesu akamjibu kwamba, Maria alikuwa amechagua fungu jema ambalo kamwe halitaondolewa kwake!
Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kutokana na shughuli nyingi alizokuwa nazo Martha pale jikoni alikuwa anajisahau kwamba ndani ya familia alikuwepo Yesu kama mgeni wao ambaye kimsingi alipaswa kuhudumiwa, kupatiwa chakula na hifadhi, lakini zaidi alipaswa kusikilizwa. Hapa Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha sanaa ya kusikiliza kwani mgeni anapaswa kukirimiwa kwa kuzingatia pia historia, mawazo na mchango wake ili kweli aweze kujisikia kwamba amepokelewa na kukirimiwa kwa ukarimu kiasi hata cha kujisikia kuwa yuko nyumbani kati ya watu.
Pale mgeni anapopokelewa lakini wenyeji wake wakaendelea na shughuli zao za kila siku anaweza kujisikia kuwa ni nguzo ya jiwe, mahali ambapo hakuna mawasiliano hata kidogo, kila mtu anachakarika kivyake vyake. Yesu anamwambia Martha kwamba, mgeni anapaswa kusikilizwa kwa makini na kwamba, Maria alikuwa amechagua fungu bora zaidi la kumsikiliza Yesu kwa makini. Neno la Yesu ni mwanga na nuru ya maisha ya mwamini. Kumbe waamini wanapaswa kujifunza kumsikiliza Yesu kwa makini na kumwachia nafasi ili aweze kuwagusa kutoka katika undani wa maisha yao.
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Yesu kabla ya kupokelewa na kukirimiwa kwenye familia ya Maria na Martha kama Bwana na Mwalimu alikuwa ni hujaji na mgeni. Kumbe, Yesu anapomwita Martha mara mbili anamkumbusha kwamba, anafanya mambo mengi kiasi hata cha kusahau kwamba kumsikiliza Yesu ndilo jambo muhimu sana kulilo mambo mengine yote. Sanaa ya kusikiliza inaonesha upendo wa kidugu unaomkirimia mtu furaha ya ndani kiasi cha kujisikia kuwa kweli ni mgeni na wala hayuko kwenye nyumba ya wazee waliotelekezwa au kwenye nyumba ya wageni bali yuko kwenye familia!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, ukarimu kwa wageni ni sehemu ya matendo ya huruma kimwili na ni fadhila ya Kikristo na kiutu ambayo katika ulimwengu mamboleo inaanza kusahaulika hata pengine kupotea kabisa. Leo hii kuna taasisi na miundo mbinu inayoanzishwa kwa ajili ya kuwahudumia wazee na wagonjwa lakini kwa bahati mbaya, taasisi nyingi hazina ndani mwake huruma, ukarimu na upendo na matokeo yake, watu wengi wanajisikia kuwa wametelekezwa kama magari mabovu na wapweke.
Hii ndiyo hali inayowakumba hata wageni, wakimbizi na wahamiaji wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kiasi kwamba, hakuna mtu anayetaka kujisumbua kuwasikiliza kwa makini ili kuguswa na kubadilishwa na historia pamoja na mang’amuzi yao ya maisha. Inasikitisha kuona kwamba, hata ndani ya familia zenyewe kuna baadhi ya familia hazina chembe hata kidogo ya ukarimu na utamaduni wa kusikiliza. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu katika ulimwengu mamboleo wanayo mambo mengi ya kufanya kiasi hata cha kukosa nafasi ya kusikilizana na kuonjeshana ukarimu na mapendo.
Baba Mtakatifu anawataka wanafamilia kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana kwa makini ndani ya familia na kamwe asiwepo mtu anayetengwa katika sanaa na utamaduni huu. Waaamini wajifunze sanaa na kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa kutenga muda wa kutosha kwani katika sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini, hapo kuna mzizi wa amani. Bikira Maria ni mfano wa mwanamke wa shoka aliyesikiliza na kutenda, awasaidie waamini kuwa na ukarimu kwa jirani zao.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment