SECAM YATOA UJUMBE KWA FAMILIA ZA MUNGU BARANI AFRIKA


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, baada ya kuhitimisha mkutano wake mkuu wa 17 uliokuwa unafanyika huko Luanda, Angola kuanzia tarehe 18- 25 Julai 2016, limetoa ujumbe kwa familia ya Mungu na watu wote wenye mapenzi mema Barani Afrika. SECAM pamoja na mambo mengine, inakazia umuhimu, ukuu na utakatifu wa ndoa na familia; changamoto; furaja ya upendo na familia kama madhabahu ya uhai. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho haya yameongozwa na kauli mbiu “Familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya mwanga wa Injili”.
Wajumbe wa SECAM wanatoa shukrani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu na familia ya Mungu Barani Afrika. Wanamshukuru kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia pamoja na Wosia wake wa kitume “Furaha ya upendo ndani y afamilia”. Wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa hija yake ya kitume Barani Afrika. SECAM inawashukuru wananchi wa Angola kwa upendo na ukarimu wao kwa wajumbe wa SECAM wakati wa maadhimisho ya mkutano wao.
SECAM bado inakumbuka hija ya kitume ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2009 wakati Angola ilipokuwa inaadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Uinjilishaji na kwamba, maadhimisho ya mkutano wa SECAM ni kielelezo cha mshikamano wa upendo na familia ya Mungu nchini Angola. Wanazikumbuka na kuziombea nchi ambazo kwa sasa zinaogelea katika: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kama vile: Sudan ya Kusini, Somalia, Lesotho, Burundi, Nigeria, Mali, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri na Libya.
SECAM inawakumbuka na kuwaombea waathirika wa machafuko yote haya na kuwataka wahusika kujikita katika mchakato wa majadiliano ili kukuza na kudumisha amani! Wajumbe wanawashukuru wadau mbali mbali wa maendeleo kwa moyo wao wa upendo na mshikamano kwa familia ya Mungu Barani Afrika.
SECAM inaendelea kukazia kwa namna ya pekee umuhimu, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia Barani Afrika, kwani hili ndilo Kanisa la nyumbani na msingi wa maisha ya kijamii na kwamba,  ubora wa maisha ya jamii yoyote ile unapimwa na afya ya familia. Ni katika familia watu wanapata elimu na majiundo ya awali; tunu msingi za maisha zinazomwezesha mtu kutekeleza majukumu yake ndani ya jamii na katika Kanisa katika ujumla wake. Familia ni muhimu sana katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu.
SECAM inasema, ndoa na familia ni chanda na pete na kwamba, ndoa ya Kikristo inajikita katika uhusiano wa dhati kati ya mwanaume na mwanamke wanaounganishwa kwa kifungo cha Sakramenti ya Ndoa na kuwa mwili mmoja. Ndoa kadiri ya mpango wa Mungu inajikita katika udumifu pamoja na kuendeleza kazi ya uumbaji na malezi kwa watoto. Ndoa za jinsia moja ni kinyume kabisa cha mpango wa Mungu kwa mwanadamu.
SECAM inaorodhesha litania ya changamoto za shughuli za kichungaji katika utume wa familia kwa kutaja: Umaskini, utengano wa kijamii; utandawazi na njia za mawasiliano ya kijamii; dhana ya usawa wa kijinsia; familia tenge, utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika utoaji mimba na kifo laini; mahari; wajane; wahamiaji na wakimbizi kutokana na vita na kinzani za kijamii; mipasuko ya kifamilia na imani za kishirikina na hali ya utengano wa muda kati ya wanandoa kutokana na kazi au masomo.
Mambo yote haya yanaathari kubwa kwa familia ikiwa kama hakuna mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na utume wa familia. SECAM inapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa matumaini.
SECAM inapenda kumuunga mkono Baba Mtakatifu Francisko katika wosia wake wake wa kitume kuhusu ”Furaha ya upendo ndani ya familia” kwa kukazia uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia na kwamba, huu si mzigo bali ni jumuiya ya upendo, furaha kwa ajili ya ustawi na maendeleo wanandoa na familia katika ujumla wake. Familia ni chemchemi ya furaha inayobubujisha zawadi na furaha ya maisha mapya na kwamba, binadamu ameumbwa ili kupenda na kupendwa kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika upendo wa dhati, familia inaweza kutekeleza kikamilifu wito na utume wake.
SECAM inakaza kusema, familia ni ”madhabahu ya uhai” na mahali pa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upendo; utii pamoja na kuhudumiana; tayari kuwakubali na kuwapokea wengine na pale inapobidi kuwasamehe. Familia za Kiafrika zinaalikwa kwa namna ya pekee kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani; mahali pa kukuza na kudumisha maendeleo ya mtu: kiroho na kimwili, ili kuziwezesha familia kuwa kweli ni Jumuiya za uhai, sala, upendo na wakala wa mabadiliko katika jamii. Kwa njia hii, familia zinaweza kutekeleza kwa uaminifu wito wake wa kuelimisha, kupyaisha pamoja na kuleta mwamko na ari ya kimissionari kati ya wajumbe wake.
SECAM inavitaka vyama vya kitume pamoja na wadau mbali mbali wa Utume wa familia kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasindikiza wanandoa watarajiwa kabla, wakati na baada ya maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa. Wadau hawa wasaidie kukuza na kudumisha ndoa ya Kikristo pamoja na tunu msingi za maisha ya kifamilia hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.
SECAM inautaka Umoja wa Afrika kusimama kidete kupinga shinikizo kutoka kwa Serikali wahisani zinazotaka kulazimisha sera ambazo zinapingana kimsingi na tunu bora za kifamilia na utu mwema. SECAM inazipongeza Serikali ambazo zimesimama imara kupinga sera hizi dhidi ya tunu msingi za kifamilia. Inazitaka Serikali kutunga na kudumisha sera ambazo zinaheshimu tunu msingi za utamaduni wa kiafrika, haki msingi za binadamu na familia; haki pamoja kukuza mafao ya wengi ili kuboresha maisha ya watu Barani Afrika. Ni matumaini ya SECAM kwamba, Serikali zitapitisha sheria pamoja na kukuza fursa za ajira kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana wa kizazi kipya kutoka Barani Afrika, ili kuweza kuendeleza ujenzi wa familia.
SECAM inahitimisha ujumbe wake kwa familia ya Mungu na kwa watu wote wenye mapenzi mema kwa kusema: matumaini ya familia kwa siku za usoni ni kiini cha Utume wake. Familia itaendelea kuwa ni madhabahu ya uhai, ukuaji na maendeleo ya binadamu. Familia ni zawadi kutoka kwa huruma na upendo wa Mungu. Familia zinapaswa kulindwa na kuendelezwa. Familia za Kikristo zithubutu kumweka Kristo kuwa ni kiini cha maisha yake pamoja na kumtumainia.
Utume kwa familia ni dhamana nyeti, kumbe, kuna haja ya kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Mababa wa SECAM wanaziweka familia zote Barani Afrika chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ili kuziinua familia na hatimaye, kuondokana na ubinafsi, migawanyiko na vipigo. Familia ziwe ni Jumuiya za upatanisho, haki na amani na kisima cha furaha ya upendo!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI