TANZIA:MUASISI WA UKATEKUMENI MPYA AFARIKI DUNIA


Mama Carmen Hermandez, aliyekuwa na umri wa miaka 85 muasisi mwenza wa Chama cha Kitume cha Ukatekumeni mpya pamoja na Bwana Kiko Arguello, amefariki duniani, Jumanne tarehe 19 Julai 2016 na maziko yake ni Alhamisi, tarehe 21 Julai 2016 yatakayoongozwa na Askofu mkuu Carlos Osoro Sierra wa Jimbo Kuu la Madrid, Hispania. Carmen, Kiko la Padre Mario Pezzi katika miaka 1960 walianzisha Chama cha Kitume cha Ukatekumene Mpya na sasa kuna zaidi ya Jumuiya 30, 000 zilizoenea katika nchi 120 duniani. Hayati Carmen alikuwa  na upendo mkubwa kwa karama yake, Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Itakumbukwa kwamba, Carmen Hermandez alizaliwa kunako tarehe 24 Novemba 1930 huko Olvega, Navarra nchini Hispania. Alipata elimu yake ya msingi kutoka katika shule iliyokuwa inasimamiwa na kuongozwa na Wayesuit na huko alibajatika kupata majiundo ya kimissionari yaliyoacha chapa ya kudumu katika maisha na wito wake katika Kanisa. Akajipatia elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Madrid, katika masuala ya Kemi ana kubahatika kufanya kazi katika kiwanda cha familia.
Baada ya alilazimika kuachana na kazi hii na kuanza hija ndefu ya maisha ya kimissionari, akajiunga na Shirika la kitawa lililojulikana kama “Wamissionari wa Kristo Yesu” ili kuweza kutekeleza ndoto yake ya kuwa mtawa! Akajiandaa kwenda kwenye utume nchini India lakini kabla ya hapo akapelekwa nchini Uingereza ili kujifunza lugha, lakini kwa bahati mbaya Shirika hili litakumbwa na mgogoro na hatimaye, kufutika katika historia ya Kanisa.
Katika maisha yake akabahatika kukutana na Magwiji wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu na Liturujia waliokuwa wanashiriki katika utekelezaji wa mchakato wa mageuzi yaliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, hapo akagundua umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kama kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; Umuhimu wa Katekesi na Majiundo makini k wa waamini walei ndani ya Parokia bila kusahau umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini. Alibahatika kutembelea Nchi Takatifu huko akajifunza zaidi Neno la Mungu, akalitafakari na kulimwilisha katika Sala..
Aliporejea nchini Hispania alikuwa na shauku ya kutaka kuwakusanya vijana waliokuwa na shauku ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hususan nchini Bolivia na kubahatika kukutana na kijana Kiko Arguello, thabiti katika imani aliyetamani kulihudumia Kanisa miongoni mwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapo wakaanzisha Jumuiya ya Kikristo iliyojikita katika Uinjilishaji wa kina uliokuwa unagusa undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika Neno la Mungu, Katekesi makini, Sala na Maisha ya Kisakramenti.
Mwelekeo huu wa maisha ukawagusa watu wengi na kuwa ni njia ya Uinjilishaji kati ya watu, hasa miongoni mwa Wakristo baada ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Mama Carmen akajikita katika ujenzi wa msingi wa Katekesi inayojikita katika Liturujia, Katekesi, Upendo kwa Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya wanawake. Katika safari nzima ya Chama hiki cha kitume, akatoa mchango na karama yake ya kimama na kunako mwaka 2011 wakafanikiwa kuandika “Mwongozo wa Katekesi ya Safari ya Ukatekumeni Mpya”.
Kunako mwaka 2015 akatunukiwa Shahada ya heshima katika masuala ya kitaalimungu kutoka katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Washington, nchini Marekani. Hadi dakika ya mwisho ya maisha yake, aliendelea kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kusema na kusimamia ukweli bila kuzunguka mbuyu. Alikuwa ni nguzo kuu katika maisha na utume wa Chama cha Ukatekumeni Mpya, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo; akanonesha upendo mkuu kwa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro anasema Kiko Arguello.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI