PAPA AADHIMISHA IBADA MIAKA 1050 UKRISTO POLAND.
Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 28 Julai 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Jasna Gòra kama sehemu ya kilele cha Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland, ibada ambayo imehudhuriwa na umati mkubw wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Poland wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani. Akiwa njiani kuelekea kwenye maadhimisho haya, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kuwasalimia Watawa wa Shirika la kutolewa Bikira Maria Jimbo kuu la Cracovia.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye Ibada hii ya Misa Takatifu ametafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili, akaja kukaa kati ya watu wake, lakini kwa bahati mbaya watu wake hawakumpokea. Lakini Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, wakati ulipotimia, akaujaza ulimwengu kwa wena na huruma yake na hapo akazaliwa Mwana wa Mungu katika hali ya umaskini na unyenyekevu mkuu. Yesu aliwafunulia watu huruma ya Mungu kwa kutenda miujiza. Kwenye harusi ya Kana, Yesu akatenda muujiza wake wa kwanza, kwa kuwarejeshea wanaharusi furaha baada ya kutindikiwa na divai!
Hiki ni kielelezo cha uwepo na ukaribu wa Mungu anayewajali na kuwatunza watu wake tofauti kabisa na binadamu mwenye uchu wa madaraka anayetaka kujikuza na kuonekana; kishawishi kikubwa cha binadamu. Mwenyezi Mungu anataka kujipenyeza katika maisha ya watu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza; kwa kuondoa kuta za utengano pamoja na kuendelea kujionesha katika hali ya unyenyekevu. Kimsingi Mwenyezi Mungu anaokoa kwa kujifanya mdogo, karibu na katika uhalisia wa maisha ya watu kama njia ya kuufunua Ufalme wake.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendo unawawezesha waamini kuwa huru, tayari kuwajibika na kushiriki katika ufunuo wa jina na siri iliyofichama moyoni mwa Mwenyezi Mungu. Kwa namna ya pekee, mashuhuda wa imani na wafiadini kutoka Poland wameonesha na kushuhudia nguvu ya Injili na huruma ya Mungu kama walivyofanya Watakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina na kwa njia yao, huruma na upendo wa Mungu umeweza kulifikia Kanisa na walimwengu wote katika ujumla wao. Kumbe, maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland si haba kwamba, yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.
Mwenyezi Mungu yupo na ufalme wake uko karibu na watu na anapenda kujishughulisha na maisha ya watu kwa kutembea nao kila siku! Kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa zawadi ya imani na maadhimisho ya Miaka 1050 ya Ukristo ni jambo muhimu sana. Mama Kanisa anahamasishwa pia kuwa msikivu, kujihusisha na maisha ya watu na kuwa jirani na binadamu wote wakati wa shida na magumu, ili Injili ya Kristo iweze kumwilishwa katika ulimwengu wa watu halisi na hatimaye, kuzaa matunda yenye kuleta mwanga angavu na uwazi katika maisha.
Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, uwepo wa Mungu ni jambo halisi kwani anatenda kwa njia ya Neno wake aliyefanyika mwili, akashuhudia huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu kama ilivyokuwa hata kwa historia ya familia ya Mungu nchini Poland iliyokita maisha yake katika Injili, Msalaba na uaminifu kwa Kanisa; ikafanikiwa kurithisha imani hata kwa vijana wa kizazi kipya. Ndiyo maana anashiriki pamoja nao katika hija ya kumshukuru Mama wa Mungu kwenye Madhabahu ya Jasna Gòra.
Baba Mtakatifu Francisko anaipongeza familia ya Mungu nchini Poland kwa kwa kuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria aliyekubali kuwa ni Mama wa Mungu, ambaye waamini nchini Poland wanakimbilia huruma na tunza yake ya kimama. Mama huyu aendelee kuwaonesha njia na kuwasaidia kushikamana kikamilifu katika maisha, kielelezo makini cha Injili. Bikira Maria anapenda kuonesha ukaribu wake ili kujikita katika mambo msingi ya maisha; kwa kulinda familia; kukuza na kudumisha umoja wa kitaifa; kwa kuwa ni shule ya sala na kujenga mshikamano na watu wote bila upendeleo wala ubaguzi. Bikira Maria awe ni chemchemi ya furaha, amani na karama za Roho Mtakatifu, ili kuwa waamini na watumishi wema.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment