ZINGATIA HAYA BAADA YA MWAKA WA HURUMA YA MUNGU


Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume katika hotuba yake elekezi kwa mafunzo ya ndani ya wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu na kwa namna ya pekee Sakramenti ya Upatanisho  hapo tarehe 14 Machi 2017 na yanatarajiwa kufungwa hapo tarehe 17 Machi 2017 anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yameacha utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni utajiri ambao unapaswa kuendelezwa mbele katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kumekuwepo na ari na mwamko mkubwa kwa waamini kukimbilia tena kiti cha huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.
Waamini wamejitahidi kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kuna waamini ambao wameguswa kutoka katika undani wa maisha yao kiasi hata cha kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa toba na wongofu wa ndani, leo hii ni watu wapya wanaotembea katika mwanga wa huruma na neema ya Mungu! Lakini, Kardinali Piacenza anakaza kusema, si rahisi sana kuweza kuorodhesha mafanikio yaliyopatikana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, jambo la msingi ni kumshukuru Roho Mtakatifu aliyeliwezesha Kanisa kusoma alama za nyakati na kutenda kwa hekima na busara.
Toba na wongofu wa ndani ni mchakato unaomwezesha mwamini kuwa karibu na Mwenyezi Mungu tayari kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, kwani hapa Mwenyezi Mungu anaugusa undani wa maisha ya mwanadamu. Huruma ya Mungu inamwezesha mwanadamu kukumbuka kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, katika maisha yake, anakabiliwa na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi, vinginevyo anaweza kuelemewa na udhaifu wake wa kibinadamu. Huruma ya Mungu ni dawa pekee inayopyaisha tena maisha ya mwanadamu na hivyo kumpatia mwelekeo mpya.
Kardinali Piacenza anasema, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, waamini wamegundua kwa mara nyingine tena kwamba, mwanadamu na mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili ni jukwaa la watu kukutana na kusaidiana; sanjari na kushikamana katika huduma makini inayojali na kuguswa na  mahangaiko ya watu wengine. Kwa njia hii, waamini wanaweza kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao; ubaridi wa imani; kutopea katika imani na hatimaye mwamini kujikuta akiyatukuza na kumezwa na malimwengu! Kumbe, mt una utu wake; mahitaji yake msingi ni kielelezo cha utukufu wa Mungu.
Kardinali Piacenza baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anapenda kukazia mambo makuu matatu: wongofu wa kimissionari wenye uwezo wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu kwa uhuru zaidi unaobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu. Jambo la pili ni majiundo ya awali na endelevu, ili kuwasaidia waamini kutambua dhana ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kumbe, waamini wanapaswa kuelimishwa ili kuweza kuitambua na kuimwilisha ili kweli huruma hii iweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao. Jambo la tatu ni kuwa waaminifu katika huduma ya huruma na upendo inayovuka mipaka kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi unaowakumbatia na kuwaambata walimwengu wote.
Kwa upande wake, Monsinyo Krzystof  Nykiel, Hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume, moja ya vitengo vya kale kabisa ndani ya Kanisa Katoliki amefafanua kwa kina na mapana lengo kuu la Kanisa ni kwa ajili ya wokovu wa roho za watu “Salus animarum”. Kumbe, Mahakama ya Toba ya Kitume ni mahakama ya huruma ya Mungu inayotoa  huduma kwa wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho na waamini wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; watu wanaotaka kujipatanisha na Mungu, Kanisa pamoja na jirani zao, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo mfufuka! Majiundo makini ya wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Mama Kanisa kwa wakati huu, ili kuwawezesha kuwa na nyenzo msingi katika huduma ya huruma ya Mungu kwa waja wake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI