VILIO VYATAWALA MAZIKO YA MAPADRI WATATU NA SISTA JIMBO KATOLIKI MBEYA



askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda Mhashamu Gervas Nyaisonga amewataka waamini kumshukuru Mungu kwa  msiba wa mapadri watatu na mtawa mmoja wote wa Jimbo Katoliki Mbeya huku akiwataka wafahamu kwamba vifo ni kielelezo cha maisha ya duniani  kwa waliobaki.
Akizungumza katika mahubiri  ya ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Mbeya iliyoongozwa na  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Dalu, Askofu Nyaisonga  amesema  kuwa waamini hawana budi kufurahia safari ya mwisho ya   mapadri hao na sista kwa kuzingatia ujumbe wa Baba Mtakatifu Fransisko alioutoa wakati wa Kwaresima na kwamba kila mmoja anawajibika kutekeleza mema kutokana na karama aliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga amemshukuru Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya kwa kumlea marehemu Padri John Mahundi hadi mauti yalipomfika na akatumia nafasi hiyo kutoa pole kwa  Askofu Chengula na wana Mbeya.
KIONGOZI imezungumza  na  waamini  kwa nyakati tofauti  akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri Ya Walei Jimbo Katoliki Mbeya Bw.Martin Nkala, Bw.Maico Ngairo na  Bi.Pascalina  Malekela ambao wameelezea majonzi yao kutokana na kuondokewa na  mababa mapadri pamoja na Sista  na kwamba katika historia ya Jimbo Katoliki Mbeya  haijawahi kutokea vifo vya mfululizo hivyo.
Wamesema sifa zao katika utume zitabaki katika kumbukumbu kwani walitoa mchango mkubwa katika kuinjilisha na kuisaidia jamii katika masuala mbalimbali.
 Wengine walieleza jinsi walivyowafahamu marehemu mapadri na Sista ni pamoja na Katekista Angelo Chapaligino, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ukarabati Jimbo Katoliki Mbeya Edphonce Wambali, Mwenyekiti na Katibu mstaafu wa Halmashauri Ya Walei Jimbo Katoliki Mbeya Angelus Magoma.
Msiba huo umeacha majonzi  kwa Maaskofu, mapadri, masista na waamini  wa Kanisa Katoliki nchini hasa ikizingatiwa umetokea katika kipindi cha wiki moja tu.
Waliofariki ni Padri Roland  Dubourt aliyefariki Machi 22 majira ya alfajiri akiwa anafanya mazoezi na baiskeli yake katika Parokia ya Nzovwe, Padri Godfrey Sichundwe aliyefariki  Machi 25 majira ya saa 3 usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Padri  John Mahundi ambaye amefariki  Machi 27 na Sista Winfrida Mwambipile aliyefariki Machi 25.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Mawasiliano Jimbo Katoliki Mbeya, Mama mkuu wa shirika la Bikira Maria Malkia wa mitume wa Mbeya, Sista Immakulatha Mirambo, mwili wa marehemu Sista Winfrida Mwambipile umepumzishwa katika makaburi yao yaliyopo Hasamba,Wilaya ya Mbozi katika Mkoa wa Songwe.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI