Papa Francisko: Jifunzeni kuonja na kuguswa na mateso ya wengine!

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Machi 2017, Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, anatarajiwa kufanya hija ya kitume Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia. Walengwa wakuu wakati wa safari hii ya Baba Mtakatifu Francisko ni maskini, watu wasiokuwa na makazi; wakimbizi na wahamiaji ambao anapenda kuwaonjesha furaha ya Injili kwa kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa. Hiki ndicho kiini cha mahojiano maalum yaliyofanywa na Jarida la “Scarp dè tenis” kwa Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni. Hili ni Jarida linalosaidiana na Shirika la Msaada la Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Milano kwa ajili ya kuwahabarisha watu shughuli mbali mbali zinazofanywa na Kanisa katika kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali.
Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu wanaopaswa kupokelewa, kusaidiwa na hatimaye kuingizwa katika mfumo mzima wa maisha ya kijamii bila ya kutengwa wala kunyanyaswa. Tunu msingi za maisha ya Kikristo ziwawezeshe waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutekeleza dhamana hii kwa hekima na busara. Wakristo wanapaswa kujifunza kuwa na unyenyenyekevu kwa kuonja na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengine.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema, si rahisi “kuvaa viatu” vya watu wengine kutokana na utumwa unaowafunga watu katika ubinafsi wao. Kwa mtu ambaye ametikiswa kutoka katika undani wa maisha yake kwa msiba mzito, kwa magonjwa, mahangaiko au mateso ya maisha, ni rahisi sana kusema pole! Lakini, wakati mwingine ni vigumu sana kuingia na kuonja magumu anayokabiliana nayo mtu kama huyo! Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni watu wa matendo zaidi, kwani “maneno matupu kamwe hayawezi kuvunja mfupa”!
Wakristo wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili hatimaye, waweze kuwafariji wale wanaoteseka kwa njia ya huduma makini inayorutubishwa kwa unyenyekevu, upendo na moyo mkuu. Baba Mtakatifu anasema, wakati mwingine, maskini wanaonesha moyo wa mshikamano zaidi katika kukabiliana na changamoto za maisha ikilinganishwa na watu wenye maisha bora zaidi kwenye miji mikubwa kama vile Milano.
Kwa bahati mbaya katika maeneo ya maskini, ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na utumwa mamboleo ndiyo mambo makubwa zaidi yanayoonekana, lakini ushuhuda wa upendo, ukarimu na mshikamano kati ya watu, si rahisi sana kuonekana. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, huko kwenye majumba makubwa na kwa watu maarufu ndiko kunakoshamiri mambo haya, lakini, wengi wanayafumbia macho! Watu wajifunze kuheshimiana kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wajifunze kuthaminiana kama binadamu na kamwe si kuwageuza maskini na kuwaona kuwa si mali kitu, kiasi hata cha kuwalinganisha na mbwa koko wa mtaani! Hawa ni watu wanaopaswa kusaidiwa katika shida na mahangaiko yao, ili kutambua kwamba, wao pia ni binadamu. Maskini hawa mara nyingi wanatuhumiwa kuchafua mazingira, lakini uchafuzi mkubwa ni ule unaotoka katik moyo wa binadamu, hawa maskini wana utu na heshima yao inayopaswa kudumishwa bila kuona kinyaa!
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa namna ya pekee, anayapongeza Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, ambayo daima yamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anazipongeza Parokia mbali mbali nchini Italia ambazo zimefungua malango yake kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaofika kwa wingi nchini Italia.
Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwasaidia makini kwa kuwaangalia usoni, ili kuonesha kwamba, wanawajali na kuwathamini kama binadamu! Wasiwe na wasi wasi kuhusu matumizi ya fedha wanayowapatia maskini kwa kuogopa kwamba, watakwenda kunywea pombe! Baba Mtakatifu anakaza kusema, pengine, glasi ya mvinyo ndiyo furaha peke yake waliyobakia nayo katika maisha! Waamini waoneshe upendo, ukarimu na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.
Hawa ni watu wanaokimbia vita, njaa, majanga asilia, nyanyaso na dhuluma. Watu hawa wanayo haki ya kukimbia nchi zao, kupokelewa na kusaidiwa. Ukarimu ufanywe kwa kuongoza na fadhila ya Kikristo yaani busara, kadiri ya nafasi na uwezo wa Jumuiya husika. Wahamiaji na wakimbizi, wasipothaminiwa na kushirikishwa kikamilifu katika jamii husika, watajisikia kutengwa na kupuuzwa na matokeo yake ni watu hawa kugeuka na kuwa ni hatari kubwa kwa Jamii inayowazunguka. Vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kutokea Barani Ulaya ni matokeo ya baadhi ya raia wake kujisikia kuwa si mali kitu au raia wa daraja la pili. Sweden ni mfano bora sana wa kuigwa kwa huduma na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji anasema Baba Mtakatifu Francisko.
Papa Francisko anakaza kusema, hata yeye amezaliwa katika familia ya wahamiaji kutoka Italia, wanaoishi nchini Argentina; mahali ambapo majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya watu. Ndugu zake walikuwa wahamie nchini Argentina kunako mwaka 1928, kwani walikuwa wamekwishakatiwa tiketi kwenye Meli ya “Malkia Mafalda” ambayo kwa bahati mbaya ilizama kwenye Pwani ya Brazil kunako mwaka 1928. Safari yao ikaanza tena kunako tarehe 1 Februari 1929 kwa kupanda Meli iliyojulikana kama “Gulio Cesare”. Kama kuna jambo ambalo analikosa kwa wakati huu ni nchi yake ya Argentina na uhuru wa kutoka kwenda kutembea na kupunga upepo mtaani! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wakati wa hija yake ya kitume Jimbo kuu la Milano hapo tarehe 25 Machi 2017 atabahatika kukutana na kuzungumza na watu wengi zaidi. Anasema, amewahi kupita Milano mara moja tu katika maisha yake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI