VIKOBA iboreshe afya za watoto vijijini-TEC
IMEELEZWA kuwa mafanikio ya kiuchumi
yaliyofikiwa na Vikundi vya Benki za
Kijamii Vijijini vinavyoendeshwa chini ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali
(IR-VICOBA), yaende sambamba na utoaji wa lishe bora kwa watoto katika familia
ili kuwajenga kiafya na kiakili.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba,
wakati akizungumza na Kamati ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali,wawezeshaji na
wawakilishi wa vikundi vya IR-VICOBA pamoja na wawezeshaji wakuu wa Mfumo wa
Ufuatiliaji wa Rasilimali za Umma (PETS) wilayani Mbozi.
Padri Saba aliyekuwa ziarani wilayani
humo kutembelea shughuli zinazotekelezwa chini ya Kamati ya Mahusiano ya Dini
Mbalimbali kupitia TEC kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway
(NCA), alisema pamoja na kufikiria kujiongezea kipato kutokana na shughuli za
uzalishaji wanazozifanya kutokana na fedha wanayokopa kwenye vikundi vyao,
lakini hawanabudi pia kujali afya za familia hususani watoto.
“Kama ni ufugaji wa kuku basi pale
wanapoanza kutaga ni vyema kuwapatia
watoto mayai ili kuwajenga kiakili badala ya kupeleka mayai yote kuyauza,”
alisema.
Katibu Mkuu huyo wa TEC pia
amewapongeza wana IR-VICOBA kwa utaratibu waliojiwekea katika kuwasaidia watoto
yatima na wale wanaoishi mazingira hatarishi wilayani humo; hivyo akasema hii
ni moja ya tunu ya vikundi hivyo na kielelezo tosha cha Upendo na Amani kama
inavyosisitiza kaulimbiu ya Mahusiano baina ya Dini Mbalimbali.
Sanjari na hayo Padri Saba
aliwasisitiza Wanambozi kuwa na uchumi wa kimapinduzi hasa kwa kufanya shughuli
zao kwa kupiga hatua mbele zaidi badala ya kutegemea misaada toka kwa wafadhili
wa nchi za Magharibi.
“Fanyeni shughuli zenu kwa kipiga hatua
mbele zaidi na si kutegemea misaada toka
Ulaya, misaada toka Ulaya kwa sasa imepungua na itafikia hatua itaisha
kabisa,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine Afisa Miradi
Mwandamizi wa NCA-Tanzania, Bi. Agustina Mosha, ambaye aliongozana na Katibu
Mkuu huyo wa TEC katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine alisisitiza umuhimu
wa utoaji wa taarifa kwa wakati ikiwa ni kuanzia kwenye ngazi ya vikundi, wilaya hadi Taifa.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na chini ya Kamati ya Mahusiano
ya Dini Mbalimbali wilayani Mbozi kupitia TEC, Mratibu wa Miradi hiyo Bw. John
Mwallah, kwa sasa vikundi vya IR-VICOBA wilayani humo vina vikundi vipatavyo
228 vyenye hisa zenye thamani ya shilingi takribani bilioni tatu.
Licha ya huduma za kiroho, Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) chini ya Ufadhili wa NCA linatekeleza miradi ya maendeleo kwa kupitia Kamati za
Mahusiano baina ya Dini Mbalimbali katika wilaya za Mbozi, Njombe, Ludewa,
Kasulu, Karatu, Babati, Mtwara na Temeke.
Miongoni mwa miradi hiyo ni vikundi vya Benki za Kijamii Vijijini
(IR-VICOBA), utoaji elimu ya utawala bora na ufuatiliaji wa matumizi ya
Rasilimali za Umma (PETS), miradi ambayo
ndani yake pia kuna masuala mtambuka kama Jinsia, Usaidizi wa Kisheria na Mabadiliko ya
Tabia nchi.
Hadi kufikia katikati ya mwaka jana TEC
kupitia kamati hizo za Mahusiano ya Dini Mbalimbali ilikuwa na jumla 751 vya
IR-VICOBA wanachama 19,324 kati ya yao wanawake ni 12,874 sawa na asilimia 67
huku idadi ya wanaume ikiwa ni 6,446 sawa na asilimia 33 ya wanachama wote.
Comments
Post a Comment