Vatican: Mradi wa huduma ya afya kwa wananchi wa Syria
Monsinyo Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu mwakilishi wa Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu kwa kushirikiana na Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria, Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na wadau mbali mbali wanaopenda kushuhudia Injili ya huduma kwa maskini na wagonjwa, wamezindua mpango mkakati wa kusaidia huduma ya afya nchini Syria ambako watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na vita ambayo imedumu sasa zaidi ya miaka saba.
Mpango mkakati huu, umezinduliwa hivi karibuni mjini Roma kwa mtaji wa Euro milioni moja, kwa lengo la kuhakikisha kwamba, hata maskini katika umaskini wao, wanapata huduma bora ya afya, jibu makini linalotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika kusikiliza kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wananchi milioni kumi na moja na nusu ambao hawapati huduma ya afya na kwamba, watoto ni sawa na asilimia 40% ya idadi ya watu wote hawa. Wanawake zaidi ya laki tatu, hawana uhakika wa kupata mahali salama kwa ajili ya kujifungua na matokeo yake, ni vifo vya watoto wengi wachanga.
Mpango mkakati huu, umezinduliwa hivi karibuni mjini Roma kwa mtaji wa Euro milioni moja, kwa lengo la kuhakikisha kwamba, hata maskini katika umaskini wao, wanapata huduma bora ya afya, jibu makini linalotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika kusikiliza kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wananchi milioni kumi na moja na nusu ambao hawapati huduma ya afya na kwamba, watoto ni sawa na asilimia 40% ya idadi ya watu wote hawa. Wanawake zaidi ya laki tatu, hawana uhakika wa kupata mahali salama kwa ajili ya kujifungua na matokeo yake, ni vifo vya watoto wengi wachanga.
Vatican tangu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2012 ilifuatilia kwa karibu sana mateso na mahangaiko ya wananchi huko Mashariki ya Kati, lakini Syria kwa namna ya pekee ili kuweza kuratibu mpango mkakati wa kutoa msaada kwa waathirika waliokuwa wanapata hifadhi nchini Lebanon. Papa Francisko kwa ari na moyo mkuu, ameendelea kuonesha upendeleo wa pekee kwa wananchi wanaoteseka huko Mashariki ya Kati, kiasi cha kuhakikisha kwamba, “Cor unum” kwa wakati huo inaratibu shughuli zote za misaada ili iweze kuwafikia walengwa kwa wakati.
Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni kumi na nne wanaohitaji msaada wa dharura katika sekta ya afya nchini Syria. Kardinali Mario Zenari anakaza kusema kwamba, watu wengi wanapoteza maisha nchini Syria kwa kukosa huduma bora ya afya kutokana na vita inayoendelea huko nchini Syria. Anapenda kuchukua nafasi hii, kuwapongeza mashuhuda na wasamaria wema, walioamua kujisadaka kwa ajili ya kuzindua mpango mkakati wa huduma ya afya kwa wanachi wa Syria. Huduma ya hospitali wazi kwa wote ni mradi uliobuniwa na Kardinali Mario Zenari, ili kujibu kilio na mahangaiko ya maskini huko Syria.
Hapa ni mahali pa huduma na tiba ya maisha ya kiroho na kimwili, changamoto pevu, inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuhakikisha kwamba, mpango mkakati wa huduma ya tiba kwa maskini unafanikiwa, kama kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Baba Mtakatifu Francisko katika mateso na mahangaiko ya wananchi wa Syria. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Syria imeendelea kupandikiza utamaduni wa kifo, hofu, mashaka na hali ya kutoaminiana. Msaada na huduma ya upendo inayotolewa na Kanisa Katoliki nchini Syria umekuwa ni faraja katika kuganga na kutibu madonda ya maisha ya watu wengi, kwa kushinda upweke hasi uliokuwa unawatumbukiza watu wengi katika hali ya kukata na kujikatia tamaa, na hivyo kuanza tena mchakato wa matumaini mapya.
Msaada wa hali na mali ni muhimu sana kwa wananchi wa Syria wakati huu wanapoendelea kukabiliana na changamoto kubwa katika maisha na historia ya nchi yao ambayo kwa sasa imegeuka kuwa kama kichwa cha mwendawazimu! Ujenzi na ukarabati wa hospitali zilizobomolewa kutokana na vita huko Syria ni kielelezo makini cha kutaka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya mwanadamu kwa njia ya huduma makini ya maendeleo endelevu ya binadamu anasema Monsinyo Giampietro Dal Toso katika uzinduzi wa mradi wa huduma ya afya nchini Syria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment